October 7, 2024

Mabango ya kielektroniki KIA kukuza utalii kaskazini

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Bodi ya Kampuni ya Uendeshaji wa Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (Kadco) kuweka mabango ya kielektroniki yanayoonyesha vivutio vya utalii katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifurahia jambo na watalii kutoka Israeli mara baada ya kuwaaga katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA). Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.


  • Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Bodi ya Kampuni ya Uendeshaji wa Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (Kadco) kuweka mabango ya kielektroniki yanayoonyesha vivutio vya utalii katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Dar es Salaam. Huenda utalii katika mikoa ya kaskazini mwa Tanzania ukapata msukumo wa aina yake, baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuiagiza Bodi ya Kampuni ya Uendeshaji wa Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (Kadco) kuweka mabango ya kielektroniki yanayoonyesha vivutio vya utalii katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Majaliwa aliyekua akikagua miundombinu ya uwanja wa ndege wa KIA mara baada ya kuwaaga watalii 274 kutoka Israeli waliowawakilisha wenzao 1,000 kuondoka nchini juzi (Aprili 27, 2019) kurejea kwao, amesema Kadco washirikiane na Wizara ya Maliasili na Utalii kuweka utaratibu mzuri wa kutangaza vivutio katika uwanja huo ili kuongeza mapato kwa Serikali.

“Kadco na Wizara ya Maliasili na Utalii, shirikianeni kuweka utaratibu wa kutangaza vivutio vyetu vya utalii hasa wanyama kwenye viwanja vyote vya ndege. Tunazo mbuga, milima, fukwe za bahari na ngoma za makabila mbalimbali, wekeni mabango yanayobadilisha picha,” amesema Majaliwa. 


Zinazohusiana: 


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, uongozi wa kampuni hiyo umetakiwa uangalie namna ya kutumia kuta zake kwa kuweka picha zinazoonyesha makabila na shughuli za utamaduni wa Tanzania ili kuwawezesha wageni wanaotumia uwanja huo kufahamu kwa undani fursa za utalii zilizopo nchini.

“Nimezunguka humu ndani, kuta zote ni nyeupe tu, tumieni fursa hiyo kutangaza tamaduni zetu na vivutio tulivyonavyo,” amesema Majaliwa wakati akimpa maelekezo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kadco, Mhandisi Christopher Mukoma. 

Akiwa uwanjani hapo, Waziri Mkuu amekagua eneo la mapokezi, sehemu ya abiria wanaoondoka na wanaowasili, sehemu ya uhamiaji, mashine za kukagua mizigo ya wanaoondoka na wanaowasili, sehemu za kutolea huduma na maduka.

Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji wa KIA, Filbert Ndege ameagizwa awasiliane na makao makuu ya Idara ya Uhamiaji ili waangalie uwezekano wa kuongeza madirisha ya kutolea huduma za uhamiaji (counters) ili huduma hiyo itolewe kwa kasi zaidi hasa msimu ambao watalii wengi huingia nchini.