Rais Magufuli awaweka kitanzini wakuu wa mikoa wasiojenga vituo vya kuuzia madini
Ni wale ambao hawajatekeleza agizo la kujenga vituo hivyo alilolitoa Januari 9, 2019 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akiwaapisha mawaziri, makatibu wakuu na manaibu makatibu wakuu wa wizara.
Rais John Magufuli amesema hayuko tayari kufanya kazi na viongozi ambao hawatekelezi maagizo yake kwa wakati. Picha|Mtandao.
- Ni wale ambao hawajatekeleza agizo la kujenga vituo hivyo alilolitoa Januari 9, 2019 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akiwaapisha mawaziri, makatibu wakuu na manaibu makatibu wakuu wa wizara.
- Amesema hayuko tayari kufanya kazi na viongozi ambao hawatekelezi maagizo yake kwa wakati.
- Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Albert Chalamila apewa siku saba kutekeleza agizo hilo.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli amewaonya baadhi ya wakuu wa mikoa inayochimbaji madini ambao bado hawajatekeleza agizo la kujenga vituo vya ununuzi wa madini, kufanya hivyo mara moja kabla hajachukua hatua kali dhidi yao.
Alitoa agizo hilo Januari 09, 2019 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akiwaapisha mawaziri, makatibu wakuu na manaibu makatibu wakuu wa wizara ambapo alimuagiza Waziri wa Madini Dotto Biteko kusimamia uanzishwaji wa vituo vya ununuzi wa madini katika maeneo yenye migodi ukiwemo mji wa Geita ambao una wachimbaji wengi wadogo wadogo wa dhahabu.
Rais Magufuli aliyekuwa akizungumza na wananchi katika viwanja vya Sabasaba wilayani Chunya mkoa wa Mbeya leo (Aprili 27, 2019), amesema alitoa maagizo ya kujengwa vituo hivyo lakini bado ipo mikoa ambayo haijatekeleza kwa sababu viongozi wao hawataki kufanya kazi kwa bidiii na wakati.
“Siwezi kuwa na wakuu wa mikoa ambao hawatekelezi, kwangu hapana. Ukuu wako wa mkoa ni kufanya kazi na kazi yenyewe ni kuwatumikia wananchi hawa wanyonge,” amesema Rais Magufuli huku akionyesha kutofurahishwa na kasi ndogo ya utekelezaji wa maagizo anayoyatoa kwa watendaji walio chini yake.
Tangu atoe agizo hilo, ni mkoa wa Geita ndiyo umejenga kituo cha kuuzia madini ya dhahabu ambapo amehoji mikoa mingine inasubiri nini kwa sababu ina rasilimali na viongozi wanaolipwa mishahara.
“Ninalisema hili kwa dhati ninajua wako wakuu wa mikoa mingine wananisikiliza hawataki kufanya kazi. Sheria imeshapitishwa na Bunge, sheria ya madini ipo. Kama Mkuu wa Mkoa wa Geita (Mhandisi Robert Luhumbi) ameweza wakuu wa mikoa mingine mnasubiri nini? Chukua hata gari la Mkuu wa Mkoa liweke mle ndio liwe sehemu ya dhahabu,” amesisitiza Rais Magufuli.
Sheria ya madini ya mwaka 2017 inatoa maelekezo ya kujengwa kwa vituo vya ununuzi wa madini katika maeneo yanakochimbwa ili kurahisisha upatikanaji na biashara ya madini.
Zinazohusiana:
- Sekta binafsi yazungumzia Kairuki kuteuliwa kusimamia uwekezaji
- Rais Magufuli awafuta kazi Tizeba, Mwijage, joto la korosho likipanda
- Maagizo makuu 3 ya Rais Magufuli kwa watendaji serikalini
Wakati akiwatahadharisha wakuu wa mikoa hiyo, Rais Magufuli ametoa siku saba kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Albert Chalamila kujenga kituo cha ununuzi wa madini ya dhahabu katika Wilaya ya Chunya ndani ya siku saba hata kama ni chumba kimoja.
“Sasa ninataka katika mwendo huohuo wa kuhakikisha mambo mnayatimiza ndani ya siku saba hili soko liwe limefunguliwa. Nimeshatoa maelekezo ni kutimiza,” amesisitiza Rais Magufuli.
Amesema kuchelewa kujengwa kwa kituo hicho kutaendeleza matatizo kwa wachimbaji wadogo ambao wanatarajia kufaidika na rasilimali hiyo muhimu.
Sekta ya madini inachangia karibu asilimia 4.8 ya Pato la Taifa ambapo Tanzania inashika nafasi ya nne kwa uzalishaji wa dhahabu duniani lakini bado wananchi wake hawajafaidika na rasilimali hiyo.