October 7, 2024

UDSM yatakiwa kuongeza kasi utoaji haki miliki kwa wavumbuzi

Hatua hiyo inakuja baada ya CAG kubaini kuwa kuna usimamizi na utangazaji duni wa Mali-Akili chuoni hapo.

Sera ya umiliki wa Mali-Akili ya mwaka 2008 inataka Chuo Kikuu kupata kinga ya kisheria katika kutangaza na kuuza kibiashara bidhaa zinazohusiana na Mali-Akili kadri itakavyokuwa inafaa kwa maslahi ya Chuo, mtafiti na umma kwa jumla. Picha|Mtandao.


  • Hatua hiyo inakuja baada ya CAG kubaini kuwa kuna usimamizi na utangazaji duni wa Mali-Akili chuoni hapo.
  • Tangu mwaka 1981 hadi Januari 2018 Chuo kiliweza kutengeneza mashine 66, lakini uvumbuzi mmoja tu ndiyo ulikuwa na haki miliki.
  • Imeshauriwa kutengeneza mifumo imara ya kuchunguza vumbuzi zinazokidhi kupata haki miliki na kufikiria kutoa motisha kwa wavumbuzi bora.

Dar es Salaam. Wakati watanzania wakiungana na wenzao duniani kuadhimisha Siku ya Mali-Akili Duniani (World Intellectual Property Day), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimetakiwa kutengeneza mfumo mzuri wa usimamizi na kuendeleza vumbuzi mbalimbali zenye sifa ya kupata haki miliki. 

Siku ya Mali-Akili Duniani huadhimisha Aprili 26 ya kila mwaka ikiwa na lengo la kuchochea uvumbuzi na ubunifu katika sekta mbalimbali zinazoweza kuchangia katika maendeleo ya dunia. 

Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Assad ya mwaka 2017/2018 kuhusu Serikali Kuu imesema kuna usimamizi na utangazaji duni wa Mali-Akili katika chuo hicho jambo linalokwamisha kasi ya ukuaji wa vumbuzi mbalimbali. 

“Tangu mwaka 1981 hadi Januari 2018, Chuo Kikuu kupitia Technology Development and Transfer Centre (TDTC) kiliweza kubuni, kutengeneza na kuhamisha mashine 66 za aina tofauti pamoja na vipengele 35,769 vya mashine. Hata hivyo, ni mvumbuzi mmoja tu alikuwa na haki miliki,’ inasomeka sehemu ya ripoti hiyo. 

Ripoti hiyo inaeleza kuwa kuanzia mwaka 2007 hadi 2018, UDSM ilitunza uvumbuzi mmoja kuhusu uchakataji wa juisi ya ndizi na utafiti huo ulihifadhiwa mnamo Septemba 16, 2009.


Soma zaidi: 


Chuo Kikuu kwa miaka mingi kiliweza kuchapisha tafiti 2,983 lakini zenye sifa ya kupata haki miliki ni chache. Hali hiyo inasababisha kushindwa kuweka wazi vumbuzi kwa ajili ya kupata haki miliki.  

“Hii ni dalili ya kuwa, Mali-Akili hazitangazwi vya kutosha na Chuo Kikuu. Hakuna namna nzuri na imara za kutathmini vumbuzi zenye matokeo yanayostahili kupewa Haki Miliki,” inaeleza ripoti hiyo.  

Sera ya umiliki wa Mali-Akili ya mwaka 2008 inataka Chuo Kikuu kupata kinga ya kisheria katika kutangaza na kuuza kibiashara bidhaa zinazohusiana na Mali-Akili kadri itakavyokuwa inafaa kwa maslahi ya Chuo, mtafiti na umma kwa jumla. 

CAG anapendekeza UDSM itengeneze mfumo madhubuti (database) ili kurahisisha ufuatiliaji na tathmini ya vumbuzi zinazofaa kupata haki miliki. 

Pia, kutengeneza mifumo imara ya kuchunguza vumbuzi zinazokidhi kupata haki miliki na kufikiria kutoa motisha kwa wavumbuzi bora katika eneo hili.