November 24, 2024

Wageni kufunzwa Kiswahili katika Chuo cha Diplomasia

ayari Chuo kimetayarisha mtaala wa kufundishia lugha ya Kiswahili na mafunzo hayo yataanza kutolewa kuanzia mwaka wa masomo 2019/2020 ambapo Kitasaidia kuitangaza Tanzania kimataifa na kufungua milango ya fursa nyingi ikiwemo utalii.

Kiswahili ni lugha ya utambulisho kwa watanzania na inatumika kama lugha ya kuimarisha utengamano, ushirikiano na umoja wa kitaifa. Picha|Mtandao.


  • Tayari Chuo kimetayarisha mtaala wa kufundishia lugha ya Kiswahili na mafunzo hayo yataanza kutolewa kuanzia mwaka wa masomo 2019/2020.
  • Kitasaidia kuitangaza Tanzania kimataifa na kufungua milango ya fursa nyingi ikiwemo utalii.

Dar es Salaam. Huenda lugha ya Kiswahili ikaendelea kujitanua kimataifa na kufungua fursa nyingi za utalii baada ya wanafunzi wa kigeni wanaopata fursa ya kusoma katika Chuo cha Diplomasia nchini kuanza kufundishwa lugha ya Kiswahili ili kusaidia kueneza lugha hiyo kimataifa.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Damas Ndumbaro ameeleza hayo leo (Aprili 23, 2019) bengeni Jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Malindi, Ally Salehe Ally aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kuongeza lugha zinazofundishwa chuoni hapo.

“Chuo kimetayarisha mtaala wa kufundishia lugha ya Kiswahili kwa wanafunzi wa kigeni ili kusaidia kueneza lugha hiyo kimataifa. Mafunzo hayo yataanza kutolewa kuanzia mwaka wa masomo 2019/2020,” amesema Dk Ndumbaro.

Kwa sasa chuo hicho kinafundisha lugha saba ambazo ni Kiarabu, Kichina, Kifaransa, Kihispania, Kiingereza, Kikorea na Kireno.

Aidha chuo kimekuwa  kikipokea wanafunzi kutoka nchi mbalimbali  za Afrika zikiwemo Afrika Kusini, Algeria, Angola, Botswana, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Guinea, Kenya, Komoro, Libya, Malawi, Msumbiji, Namibia, Palestina, Rwanda, Sudan, Zambia, Zimbabwe pamoja na Tanzania.


Soma zaidi:
Kiswahili ndiyo mpango mzima wa kusaka wateja Tanzania: Ripoti


Tangu kuanzishwa kwa chuo hicho mwaka 1978 hadi hivi sasa, Chuo kimetoa wahitimu 3,421 kati yao, wahitimu katika ngazi ya Shahada ni 72, Stashahada ya Uzamili katika Menejimenti ya Mahusiano ya Kimataifa ni 503, Stashahada ya Uzamili katika Diplomasia ya Uchumi ni 341, Stashahada ya Kawaida 2,084, ngazi ya cheti ni 347 na wahitimu 74 ni wa mafunzo ya Maafisa Waandamizi wa Mambo ya Nje.

Mnamo Mei 2018, mtandao wa kijamii wa Twitter ulitambua rasmi Kiswahili na kukifanya kuwa lugha ya kwanza ya Kiafrika kutambuliwa na mtandao huo baada ya kampeni iliyotumia hashtaga ya #TwitterRecognizeSwahili ikishinikizwa na wakenya kadhaa kwa muda mrefu , kuitaka Twitter iitambue lugha hiyo rasmi.

Kiswahili ni lugha ya utambulisho kwa watanzania na inatumika kama lugha ya kuimarisha utengamano, ushirikiano na umoja wa kitaifa.