Serikali yakana kuzuia uchapishaji ripoti ya IMF
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema Serikali haijazuia kuchapishwa kwa taarifa hiyo inayoelezea tathmini ya hali ya uchumi wa Tanzania bali inaendelea na mazungumzo na shirika hilo la fedha duniani.
- Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema Serikali haijazuia kuchapishwa kwa taarifa hiyo bali inaendelea na mazungumzo na shirika hilo la fedha duniani.
- Taarifa hiyo inaangazia tathmini ya hali ya uchumi wa Tanzania.
Dar es Salaam. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema Serikali haijazuia kuchapishwa kwa taarifa ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) inayozungumzia tathmini ya hali ya uchumi wa Tanzania bali inaendelea na mazungumzo na shirika hilo.
Kauli ya mpango inakuja ikiwa zimepita siku sita tangu IMF kueleza kuwa Serikali ya Tanzania imezuia kuchapishwa kwa taarifa hiyo.
Dk Mpango ametoa ufafanuzi huo leo (Aprili 23, 2019) wakati akijibu swali la Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka ambaye alitaka kufahamu kwa nini Tanzania imezuia uchapishaji wa taarifa hiyo.
Amesema kuna siku 14 za kujadiliana kufuatia wataalam waliotumwa awali kutozingatia hoja za upande wa Serikali kama ulivyo utaratibu.
“Serikali inakuwa na siku 14 kuijadili taarifa hiyo za kuipitia na kusema itolewe au isitolewe. Tuahirishe mjadala, Serikali bado inazungumza na IMF na hakuna sehemu ambayo tumezuia ni utaratibu wa IMF yenyewe,” amesema Dk Mpango.
Mwakajoka aliuliza swali hilo wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mwaka wa fedha 2019/2020.
Aprili 17 mwaka huu IMF ilitoa taarifa kuwa umezuiwa na Serikali kuchapisha ripoti hiyo, jambo lililoibua mjadala na maoni tofauti ya watu huku wengine wakitaka taarifa hiyo iwekwe hadharani ili kuimarisha uwazi na uwajibikaji wa taasisi za umma katika shughuli za ukuaji wa uchumi.
Hata hivyo, baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa vimeripoti maudhui ya taarifa hiyo.