Tafakari haya msimu wa sikukuu ya Pasaka
Pasaka itakuwa na maana kama itatumika kutafakari vionjo muhimu ya maisha ikiwemo kuzingatia uhuru usiopitiliza na kuwakumbuka walio chini yako.
- Pasaka itakuwa na maana kama itatumika kutafakari vionjo muhimu ya maisha ikiwemo kuzingatia uhuru usiopitiliza na kuwakumbuka walio chini yako.
- Lakini kumbuka kuongeza maarifa kwa kusoma vitabu na kuishi maisha yenye malengo.
Ni msimu wa sikukuu, kwa Wakristo wanakumbuka kifo cha Yesu Kristo aliyesulubiwa msalabani miaka zaidi ya 2000 iliyopita.
Ni sikukuu ya Pasaka ambayo mwaka huu inaadhimishwa Aprili 21, 2019 ambapo watanzania wanaungana na Wakristo wengine duniani kama siku ya mapumziko wakiwa nyumbani na kutembelea ndugu na marafiki ili kudumisha upendo.
Lakini Pasaka itakuwa na maana kama itatumika kutafakari vionjo muhimu ya maisha ambavyo vinaweza kuifanya dunia kuwa sehemu muhimu ya kuishi na kuendeleza mipango ya kuwa bora kila siku. Tafakari haya msimu wa sikukuu:
Beba kitabu kila unapokwenda
Unaweza kusoma kila unapopata muda ili kuongeza maarifa na ujuzi katika maisha. Kama uko nyumbani ni muda muafaka kuchagua kitabu kizuri kinachoendana na malengo yako.
Kama ni ngumu kusoma, basi sikiliza sauti za kitabu (Audio books). Hii ni njia rahisi ya kusoma vitabu vingi kwa muda mfupi hasa wakati huna kazi nyingi. Itumie Pasaka kuongeza maarifa hasa ukizingatia tumekamilisha robo ya kwanza ya mwaka 2019 na bado kuna mengi ya kujifunza kukamilisha ndoto za maisha.
Soma zaidi:
Usitishike na mafanikio ya wengine
Kila mtu ana wakati wake wa kufanikiwa, weka mipango yako vizuri kufikia kilele cha mafanikio yako. Mafanikio ni safari inayohitaji uvumilivu na kujituma zaidi kuliko kuhangaishwa na mafanikio ya wengine kwasababu kila mtu ana mbinu yake ya kufanikiwa.
Mafanikio ni pamoja na kuzingatia mipango yako na kuepuka kumpendeza kila mtu. Picha|Mtandao.
Usijaribu kumpendeza kila mtu
Katika maisha huwezi kumpendeza kila mtu, lakini unaweza kuwapendeza watu wachache kwa wakati fulani. Kama utampendeza kila mtu utafeli katika maisha.
Ishi maisha yako kwasababu hata wale unaotaka kuwapendeza itafika wakati watakugeuka. Maisha ni kufanya yale unayoona ni mema kwako na yanayokupa furaha wakati wote. Wafanyie mema watu wanaokuzunguka usilipe mabaya.
Uhuru siyo kufanya kila kitu
Tuna uhuru wa kuamua kufanya kila kitu katika maisha lakini uhuru una mipaka yake. Mipaka inakusaidia kuepuka madhara ya kufanya vitu visivyo na mpangilio. Tumepewa akili na utashi wa kufanya mambo mema yenye tija kila wakati, tuzitumie vizuri.
Kama ni kijana epuka starehe na maisha ya anasa yanayoweza kukupotezea muda wa kufikia mipango ya kuwa na familia bora lakini kuharibu afya yako ambayo ni muhimu katika kuongeza tija ya maisha. Zingatia uhuru sio kufanya kila kitu!
Maisha ni kufanya yale unayoona ni mema kwako na yanayokupa furaha wakati wote. Picha|Mtandao.
Usiwasahau watu walio chini yako
Huenda umepata mafanikio makubwa ya kikazi au biashara ambayo yamekufanya upande juu na kufikia daraja la heshima. Unaambiwa usiwasahau watu walio chini yako ambao hawana uwezo kifedha au uwezo na ujuzi ulionao.
Kumbuka kuwainua marafiki na ndugu zako kwasababu unaweza kukutana nao ikiwa mambo yako hayajakuendea vizuri. Maisha ni kupanda na kushuka. Ishi maisha ya kawaida jiepushe na majivuno na kujikweza. Sisi wote ni wapitaji na wasafiri.
Uwe na mapumziko mema ya Pasaka!