November 24, 2024

Wazazi wafanye nini kudumisha mahusiano na watoto wawapo mbali?

Matumizi ya teknolojia ikiwemo simu za mezani na kamera maalum za CCTV yanaweza kusaidia kudumisha uhusiano na kufuatilia usalama wa mtoto akiwa nyumbani.

  • Matumizi ya teknolojia ikiwemo simu za mezani na kamera maalum za CCTV yanaweza kusaidia kufuatilia usalama wa mtoto akiwa nyumbani.
  • Mzazi anaweza pia kuwapigia simu ya sauti na video watoto ili kujua hali na maendeleo yao darasani. 

Dar es Salaam. Sandra Daudi (20) ambaye kutokana na kushindwa kuendelea na masomo ya sekondari ameajiliwa kama dada wa kazi za nyumbani jijini Daresalaam, lakini amekuwa chanzo cha furaha kwa James na Juliette, watoto ambao wazazi wao wanaishi mbali na jiji hilo. 

Sandra ambaye anaishi na watoto hao  Boko Magegeni anasema wazazi wa watoto hao wana shughuli nyingi za kikazi katika mikoa mingine na hurudi nyumbani wakati wa  likizo huku baba hurudi nyumbani mara mbili kwa mwaka.

“Nilianza kazi James akiwa ameanza darasa la kwanza na Juliette akiwa na miaka miwili akielekea kuanza shule ya awali. Wamekua ni zaidi ya familia yangu” amesema Sandra ambaye ameishi na watoto hao zaidi ya miaka minne.

James na Juliette ni miongoni mwa watoto wengi nchini Tanzania ambao wanaishi mbali na wazazi, jambo linaweza kuwa changamoto katika malezi yao kwa sababu wanakosa uangalizi wa karibu wa wazazi wote wawili. 

Hata hivyo, watoto hao wamepata bahati ya kulelewa vizuri na Sandra ambaye anahakikisha wanapata mahitaji yao yote bila hata kuwepo wazazi wao.


Zaidi, soma:


Teresia Mzee, mama wa watoto hao anasema majukumu ya kikazi ndiyo yamemuweka mbali na watoto wake lakini bado anawapenda na kufuatilia kwa karibu malezi yao. 

Anasema alihamishiwa kituo cha kazi katika mkoa wa Kigoma baada ya kampuni iliyomwajiri kufungua tawi jipya katika mkoa huo na amejaribu kuomba uhamisho arudi Dar es Salaam bila mafanikio. 

“Uhamisho nimeomba mara nyingi tu lakini kila ninapoomba sipati majibu yanayonipa tabasamu. Nilijaribu hata kuhama kampuni bila mafanikio,” anasema ambaye anamshukuru Sandra kwa upendo na malezi mazuri kwa watoto wake. 

Malezi mazuri yanayoambatana na ukaribu kwa watoto husaidia kudumisha upenda kati ya watoto na wazazi. Picha|Mtandao.

Wazazi walio mbali na watoto wao wafanye nini?

Kutokana na ukweli kuwa kutafuta pesa ni muhimu kwa ajili ya familia, wazazi bado wana nafasi ya kudumisha mahusiano na watoto wao hata wakiwa mbali kwa kutumia mifumo ya kidijitari ambayo haitatizwi na umbali wa watumiaji. 

Mhandisi wa programu za kompyuta na mfanyabiashara anayeishi Kawe jijini hapa, Taurus Charles ambaye muda mwingi husafiri na kuwaacha watoto wake nyumbani, anasema kwenye nyumba yake amefunga kamera maalum za CCTV ambazo zinarekodi matukio yote yanayoendelea nyumbani. 

Anasema hiyo ni njia mojawapo anayotumia kuhakikisha watoto wake wako salama anapokuwa safarini. 

“Hauishi mwezi nakua nimerudi na hata nikisafiri, nimeweka kamera za CCTV nyumbani pamoja na simu ya mezani inayonisaidia kuwasiliana na watoto wangu,” amesema

Kupitia simu ya mezani, amesema inamsaidia kufahamu kama watoto wake wapo nyumbani kwa sababu  ndiyo wanapokea simu hiyo huku akibainisha kuwa wafanyakazi wa ndani siyo watu wa kuwategemea sana. 

“Wasikilize watoto wanajua vitu vingi sana na wanajua nani anafaa kubaki nao, ukiangalia kesi nyingi za unyanyasaji za watoto zinafanywa na ndugu. Nashauri wabaki na ndugu wa kike na mzazi awe anamchunguza,” ameshauri Taurus.

Kwa upande wake, Teressia anasema ni vema wazazi  kuwapigia watoto simu ya sauti na  video walau mara mbili kwa wiki ambapo  imemsaidia  kujenga ukaribu na watoto wake na hata kufuatilia maendeleo yao shuleni na nyumbani.