November 24, 2024

Yaliyofichika ndani ya hifadhi ya Taifa ya Udzungwa

Licha ya kuwa haifahamiki sana na watu wengi, ni hifadhi yenye hazina ya aina nyingi za mimea, ndege na wanyama ambao hawapatikani katika sehemu nyingine duniani.

  • Licha ya kuwa haifahamiki sana na watu wengi, ni hifadhi yenye hazina ya aina nyingi za mimea, ndege na wanyama ambao hawapatikani katika sehemu nyingine duniani.
  • Ni chanzo muhimu cha uzalishaji wa umeme wa maji kutoka maporomoko ya mto Ruaha.
  • Ina ukubwa wa kilomita za mraba 1990 na inapatikana katika Wilaya ya Kilombero mkoani Mrogoro kiasi cha kilomita 60 kutoka Mji wa Mikumi, na sehemu kubwa ipo Iringa Vijijini mkoani Iringa.

Dar es Salaam. Ni mwendo wa kilomita 380 kutoka Jijini Dar es Salaam hadi katika Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa iliyosheheni maajabu mengi ikiwemo aina 400 za vipepeo na maporomoko yanayosaidia uzalishaji wa umeme wa maji. 

Licha ya kuwa haifahamiki sana na watu wengi, ni hifadhi yenye hazina ya aina nyingi za mimea, ndege na wanyama ambao hawapatikani katika sehemu nyingine duniani.

Kwa watu wanaopenda kusafiri na kupumzika katika eneo tulivu, basi milima ya Udzungwa inaweza kuwa sehemu sahihi kwao kutokana na mandhari nzuri ya miinuko na miteremko yenye uoto wa asili unaovutia kwa macho. 

Hifadhi hiyo yenye ukubwa wa kilomita za mraba 1990 kwa mujibu wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) iko Wilaya ya Kilombero kiasi cha kilomita 60 kutoka ulipo Mji wa Mikumi Mkoani Morogoro huku eneo lake kubwa lipo Iringa Vijijini mkoani Iringa.

Hifadhi  hiyo ya Taifa  ya milima  ya Udzungwa inaundwa  na mapori ya akiba  ya  misitu ya Mwanihana, Kilombero  Magharibi,  Nangaje,  Matundu  na Iwonde, ikiwa ni  hifadhi  pekee  nchini  inayopatikana  katika  milima  ya  Tao la Mashariki  (Eastern  arc). 

Jina Udzungwa asili yake limetokana na Kabila la Wahehe likimaanisha  watu waishio ngambo  ya pili  ya mlima. Ilizinduliwa rasmi na Rais na Mwanzilishi wa Shirika la Uhifadhi Wanyama pori (WWF),  Prince Bernhard wa Netherlands mwaka 1992.


 Zinazohusiana:


Yaliyofichika katika hifadhi hiyo

Licha ya kuwa haifahamiki na watu wengi wa  ndani na nje, Tanapa katika maelezo yake inabainisha kuwa  hifadhi ya Taifa ya Udzungwa itabaki kuwa ya kipekee kutokonana vivutio vingine vilivyomo ndani yake kama aina 11 za jamii ya nyani wakiwemo “Mbega Mwekundu wa Iringa” (Iringa red colobus monkey) na “Sanje Crested mangabey” ambaye alikuwa hajulikani mpaka mwaka 1979. 

Kufika kwako katika hifadhi hiyo kutakupa fursa ya kuwaona viumbe hai (species) wasio mimea ikijumuisha vipepeo aina 400 wakubwa kwa wadogo, mijusi, nyani na ndege aina 250 ambao kati yao hawapatikani katika maeneo mengine duniani. 

Wanyama wengine wanaopatikana ndani ya hifadhi hiyo ni pamoja na simba, chui, nyati na tembo na ua aina ya “African violet” ni linalopatikana katikati ya miti mirefu inayofikia mita 30.

Maporomo yanayopatikana katika hifadhi ya Taifa ya Udzungwa ambayo ni kivutio kikubwa kwa watalii. Picha|Mtandao.

Hifadhi hiyo ambayo asilimia 80 iko mkoa wa Iringa na 20 katika mkoa wa Morogoro, inakupatia maporomoko ya maji kutoka mlimani yenye kasi  kubwa katika eneo lenye urefu wa mita 170 la mto Sanje kwenda juu wakati ukipanda milima ya Udzungwa. 

Ili kufika katika milima Udzungwa unaweza kutumia   lango  la  kuingilia  upande  wa  Magharibi  la Msosa ambalo liko  kilomita 10 kutoka Mtandika (Iringa) na lango  la  Udekwa  ni  kilomita  63  kutoka  Ilula katika  barabara kuu  ya Dar es Salaam-Iringa.

Licha ya vivutio hivyo, bado hifadhi hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali za kuharibika kwa miundombinu ya barabara hasa wakati wa kipindi cha mvua. 

Licha ya kuwa na hoteli za utalii, bado kuna uhitaji wa hoteli za hadhi ya kimataifa ambazo zitakuwa na uwezo wa kupokea wageni wenye kipato kikubwa.