November 24, 2024

Posho zaibua utata Tume ya huduma za walimu

Tume hiyo ilifanya malipo ya posho yasiyo ya kawaida yanayofikia Sh721.05 milioni kwa wafanyakazi wake ikiwemo kuwalipa posho za safari kwa siku 324 huku rejista ikionesha kuwa walikuwapo ofisini katika kipindi hicho.

  • Tume hiyo ilifanya malipo ya posho yasiyo ya kawaida yanayofikia Sh721.05 milioni kwa wafanyakazi wake ikiwemo kuwalipa posho za safari kwa siku 324. 
  • Rejista ya mahudhurio imeonesha wafanyakazi hao walikuwapo ofisini kwa kipindi hicho.
  • Tamisemi yashauriwa kuchunguza kwa ukaribu suala hili na itakapohitimishwa wahusika wanapaswa kuwajibika.

Dar es Salaam. Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2017/2018 kuhusu Serikali Kuu imebaini kuwa Tume ya Huduma za Walimu (TCS) ilifanya malipo ya posho yasiyo ya kawaida yanayofikia Sh721.05 milioni kwa wafanyakazi wake ikiwemo kuwalipa posho za safari kwa siku 324. 

Ripoti hiyo iliyowekwa wazi kwa umma Aprili 10, 2019 na CAG Profesa Mussa Assad, imebaini kuwa wafanyakazi mbalimbali wa tume hiyo walilipwa posho za aina tatu kwa lengo la kutekeleza shughuli za ofisi ikiwemo posho ya safari kwa siku 324, posho ya kazi za ziada kwa siku 365 na posho za vikao kwa siku 127. 

Posho zote hizo ziligharimu kiasi cha Sh721.05 milioni, jambo lililoibua utata katika matumizi ya rasilimali za ofisi hiyo ya umma. 

CAG amebainisha kuwa hali hiyo si tu kwamba inaashiria matumizi yenye mashaka bali kutokuwa na uhakika kama wafanyakazi walikuwa nje ya kituo cha kazi kwa mwaka mzima wakati rejista ya mahudhurio imeonesha wafanyakazi hao walikuwapo ofisini kwa kipindi hicho. 

“Ni mtazamo wangu kwamba, mapungufu haya yamesababishwa na udhibiti wa ndani na uaminifu hafifu juu ya kulinda na kutumia fedha za umma, ambapo kama hatua hazitachukuliwa yanaweza kuchochea matumizi mabaya ya fedha za umma,” inasomeka sehemu ya ripoti ya CAG.


Zinazohusiana:


Kutokana na udhaifu ulioibuliwa, CAG imeishauri menejimenti ya TCS kuanzisha mifumo imara ya udhibiti wa ndani ikiwamo huduma za ukaguzi wa ndani yenye vitendea kazi vya kutosha na mgawanyo imara wa majukumu ambao unaweza kuwa na umuhimu katika kupunguza vihatarishi vilivyotambuliwa. 

Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa imetakiwa kuchunguza kwa ukaribu suala hili, na itakapohitimishwa wahusika wanapaswa kuwajibika.

TCS ilianzishwa kwa  Sheria namba 25 ya mwaka 2015 ambapo walimu wanaoshughulikiwa chini ya sheria hii ni walimu waajiriwa wa Serikali wanaofundisha katika shule za msingi na sekondari kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Pia tume hiyo inawajibika kutoa huduma bora na kwa wakati kwa walimu wa shule za msingi na sekondari kwa kusimamia masuala ya ajira na nidhamu ili kukuza kiwango cha elimu.