October 7, 2024

Magari ya kukodi yaongeza gharama za uendeshaji balozi

CAG Prof Mussa Assad amesema fedha hizo zimeongeza gharama za utendaji, jambo ambalo lingedhibitiwa na ununuzi wa magari mapya.

  • Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imetakiwa kuacha kukodi magari kwa ajili ya shughuli za balozi badala yake inunue magari yake ili kupunguza gharama.
  • Balozi mbili za Tanzania katika miji ya Moroni nchini Comoro na Brasilia (Brazil) katika mwaka 2017/2018 zilitumia Sh87.5 kukodi magari kwa ajili ya shughuli za kila siku za balozi hizo. 

Dar es Salaam. Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imetakiwa kuacha kukodi magari kwa ajili ya shughuli za balozi badala yake inunue magari yake ili kupunguza ongezeko la gharama za kukodi magari hayo. 

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Assad ametoa ushauri huo katika ripoti ya ukaguzi wa hesabu za Serikali Kuu katika mwaka wa 2017/2018 baada ya kubaini kuwa balozi mbili za Tanzania katika miji ya Moroni  nchini Comoro na Brasilia (Brazil) zimetumia Sh87.5 milioni kukodi magari kwa ajili ya shughuli za kila siku za balozi katika miji hiyo.

CAG amesema balozi hizo mbili zimekuwa zikikodi magari kwa ajili ya shughuli za kila siku za balozi, jambo linalokinzana na kanuni ya 84 ya kanuni za Huduma za Umma (Huduma za Nje ya Tanzania) ya mwaka 2016 inayotaka kutoa gari sahihi la uwakilishi kwa Mkuu wa Balozi na gari jingine linatolewa kwa ajili ya huduma za jumla. 

“Katika ukaguzi wa mwaka husika, Balozi zililipa Sh87.46 milioni kwa ajili ya kukodi magari,” imeeleza ripoti hiyo ambayo imeendelea kujadiliwa na wanawanchi katika maeneo mbalimbali nchini hususan kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari.

Hata hivyo, amebainisha kuwa menejimenti za balozi husika zimekuwa zikifanya ufuatiliaji wa karibu na wizara lakini hakuna dalili za kumaliza tatizo hilo ambalo linakiuka taratibu zilizowekwa. 

“Menejimenti za Balozi husika zimekuwa zikifanya ufuatiliaji wa karibu na Wizara mama kupitia barua yenye kumbukumbu Na. CJB111/162/02/16 ya tarehe 8 Novemba, 2017 na CKCA.41/65/01/III ya tarehe 15 Januari 2019, mtawalia, lakini hakuna kilichofanywa na wizara ili kumaliza tatizo hili,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo. 


Zinazohusiana:


CAG  ameishauri menejimenti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuachana na ongezeko la gharama za kukodi magari kwenye balozi kwa kuhakikisha inanunua magari yake.

Ubalozi wa Tanzania nchini Comoro unaongozwa na Balozi Sylvester Mabumba huku Ubalozi wa Brazil ukiongozwa na Dk Emmanuel Nchimbi ambapo nchi hizo zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu hasa katika nyanja za mawasiliano na biashara ikiwemo mazao ya biashara.