Ushauri wa wanafunzi bora Tanzania kuelekea mitihani ya kidato cha sita 2019
Wamesema wanafunzi wanatakiwa kujiona washindi, kujiamini, kushirikiana na kufanya marudio ya waliyosoma kwa miaka miwili.
- Wanafunzi hao ni wale waliofanya vizuri katika mitihani ya kidato cha sita ambao wameeleza mbinu mbalimbali zitakazowasaidia watahiniwa kufanya vizuri.
- Wamesema wanafunzi wanatakiwa kujiona washindi, kujiamini, kushirikiana na kufanya marudio ya waliyosoma kwa miaka miwili.
Dar es Salaam. Mafanikio ya elimu katika ngazi yoyote yanategemea kusoma kwa bidii na kuzingatia yale yanayofundishwa na walimu. Lakini ni zaidi ya hapo. Ni pamoja na kujifunza kutoka kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani yao ili kufahamu mbinu walizotumia kusoma na hata kufaulu.
Zimebaki siku chache kwa watahiniwa wa kidato cha sita waanze mitihani ya kitaifa hapo Mei 6, 2019. Yapo mengi ya kujifunza kutoka kwa wanafunzi bora waliofanya vizuri katika mitihani ya kidato cha sita ya miaka iliyopita.
Wanafunzi hawa ni wale waliokuwa wa kwanza kitaifa (Tanzania One-TO), waliokuwa miongoni mwa wanafunzi 10 bora kitaifa na wale waliofanya vizuri kwa somo moja moja.
Wana mengi ya kuwafunza watahiniwa wa mwaka huu ambao wana ndoto za kufanya vizuri katika mitihani yao kuwawezesha kuendelea na masomo ya elimu ya juu.
Tovuti ya nukta.co.tz, inayokupa yanayokuhusu, imefanya mahojiano na baadhi wanafunzi bora wa miaka iliyopita ambao wanasema ufaulu wa mitihani hiyo ni zaidi ya kukesha darasani. Yafuatayo ni baadhi ya mambo wanayoshauri kwa wanafunzi wanaojiandaa na mitihani hiyo nchini.
Zinazohusiana:
- Mbinu zitakazowasaidia watahiniwa darasa la saba kufanya vizuri
- Mbinu zinazoweza kuisaidia Temeke kutokomeza sifuri elimu ya sekondari.
- Udanganyifu mitihani darasa la saba kujirudia tena mwaka huu?
Jione mshindi tayari
Mwanafunzi bora wa kike katika mtihani wa kidato cha sita mwaka 2010 kutoka shule ya Sekondari ya Marian Girls iliyopo Bagamoyo mkoa wa Pwani Jacqueline Seni anasema mwanafunzi anayetarajia kufanya mtihani ni lazima awe na fikra za kushinda hata kabla ya kuingia kwenye chumba cha mtihani.
Seni, ambaye sasa ni Mkurugenzi katika taasisi ya World Possible Tanzania, anasema kama akili ya mwanafunzi itajengwa kwa fikra za kushinda ni rahisi kusoma kwa bidii katika kipindi hiki kifupi kilichobaki na kufaulu katika mitihani.
“Kwa mimi mafanikio (ya kielemu) yanategemea akili. Unatakiwa kufikiri, kuwa na nidhamu na kuamini kama wewe ni mshindi. Akili yako itakusogeza kusoma kwa bidii kama roboti na bila shaka utashinda kwa kila kitu,” amesema Seni mwenye Shahada ya Kwanza ya Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mouloud Mammeri cha nchini Algeria.
Jione mshindi kabla ya kuingia kwenye chumba cha mtihani. Picha| Mtandao.
Jiamini kwa kile ulichojifunza
Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo Cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Christopher Ntyangiri, aliyekuwa mwanafunzi bora katika somo la fizikia katika mtihani wa kidato cha sita mwaka 1997, anasema siri ya kufaulu ni kujiamini na mwanafunzi hapaswi kabisa ‘kupanic’ au kuwa na wasiwasi.
Ntyangiri, ambaye alisoma katika Shule Sekondari ya Mzumbe iliyopo mkoani Morogoro, ameiambia nukta.co.tz kuwa kipindi hiki watahiniwa wanatakiwa kufanya marejeo na mapitio ya mambo waliyosoma kwa miaka miwili ya elimu ya kidato cha tano na sita.
“Ni kipindi cha kuongeza kidogo na kufanya revision (marudio) zaidi. Wafanye revision za kutosha kiasi kwamba unachokifahamu kikupe ufaulu badala ya kubahatisha. Muhimu ni kuwa na self-belief (imani binafsi) ya yale ambayo wamekwishajifunza,” anasema Ntyangiri aliyebobea katika uhandisi umeme.
Umoja na ushirikiano wa wanafunzi katika kusoma pamoja unaweza kuwasaidia wanafunzi kutoboa mtihani wa kidato cha sita. Picha|Mtandao.
Wanafunzi wadumishe ushirikiano
Mtaalamu wa programu za kompyuta kutoka Shirika la Code for Africa, Khadija Mahanga anawakumbusha wanafunzi kusoma kwa pamoja na kuacha ubinafsi.
Khadija, ambaye alihitimu katika shule ya sekondari ya Marian Girls iliyo Bagamoyo mkoani Pwani, anasema ushirikiano ujikite zaidi katika kupitia maswali ya mitihani ya kitaifa iliyopita ili kuwawezesha wanafunzi kufahamu maswali yanavyotungwa na mbinu za kujibu kwa ufasaha.
Khadija, ambaye alikuwa mwanafunzi bora kitaifa katika somo la Fizikia katika mtihani wa kidato cha sita mwaka 2010, anasema wakati huu mwanafunzi hatakiwi kujifungia peke yake bali ashirikiane na wenzake kurahisisha kazi ya mambo mengi aliyosoma kwa miaka miwili.
“Itamsaidia mwanafunzi kupata uelewa, itamfungua mawazo wa vipi swali linatungwa. Nasisitiza kushirikiana na wenzake kwa sababu unapokuwa pekee yako huwezi kumaliza lakini mkiwa wote mnafanya maswali mnakuwa mnaenda kwa spidi yaani kidato cha sita ni nadharia na vitendo zaidi,” anasema Khadija ambaye baada ya kumaliza kidato cha sita alisoma katika Chuo Kikuu cha Cape Town cha Afrika Kusini.