November 24, 2024

Uzalishaji wa dhahabu Acacia washuka

Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo Peter Geleta amesema uzalishaji wa dhahabu katika robo ya kwanza ya mwaka 2019 umeshuka kwa asilimia 13 ikilinganishwa na mwaka jana.

  • Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo Peter Geleta amesema uzalishaji wa dhahabu katika robo ya kwanza ya mwaka 2019 umeshuka kwa asilimia 13.
  • Sababu kubwa ya kushuka kwa uzalishaji huo ni matatizo ya kiuzalishaji katika migodi ya North Mara na Buzwagi.

Dar es Salaam. Kampuni ya madini ya Acacia imesema kuwa uzalishaji wa dhahabu katika robo ya kwanza ya mwaka 2019 umeshuka kwa asilimia 13 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana kutokana na kuporomoka kwa uzalishaji katika migodi yake ya North Mara na Buzwagi.

Ofisi Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo Peter Geleta ameeleza katika taarifa yake kwa umma kuwa katika kipindi hicho cha Januari hadi Machi mwaka huu walifanikiwa kuzalisha wakia 104,899.

“Wakati kihistoria uzalishaji wetu ni imara zaidi wakati wa nusu ya pili ya mwaka, uzalishaji katika robo hiyo ya kwanza uliathiriwa na matatizo ya kiuzalishaji tuliyokuwa hatuyatarajii katika mgodi wa North Mara,” amesema Geleta.

Geleta, ambaye alichukua uongozi wa kampuni hiyo Januari mwaka jana baada ya aliyekuwa CEO wa Acacia Brad Gordon kuachia ngazi mwishoni mwa 2017, amesema wamechukua hatua za haraka kutatua matatizo hayo kwa kupitia upya mpango wao katikati ya Machi kwa migodi yote ya ardhini na ile ya wazi (open pit).

Kigogo huyo amesema uzalishaji wa dhahabu katika mgodi wa North Mara katika kipindi hicho ulikuwa ni wakia 66,324 kiwango ambacho ni chini kwa asilimia 14 ikilinganishwa na wakia 76,769 zilizozalishwa mwaka jana.


Soma zaidi: Uzalishaji wa kahawa kuimarika msimu wa 2019-2020?


Hali hiyo, kwa mujibu wa Acacia, liichangiwa zaidi na madhara ya kuporomoka kwa sehemu ya mgodi wa chini ya ardhi  wa Gokona mwishoni mwa 2018 na kuharibika kwa tingatinga katika mgodi wa wazi wa Nyabirama.

“Bado tuna imani kuwa tutatimiza malengo yetu ya kufikia uzalishaji wa wakia kati ya 500,000 hadi 550,000 kama ilivyoelezwa katika mwongozo wa kampuni,” amesema Geleta na kuongeza;

“Napenda kuwashukuru wafanyakazi wenzangu kwa kujitoa kwa hali na mali katika kutekeleza majukumu yao katika kipindi hiki kigumu.”

Kampuni hiyo iliyoorodheshwa katika Soko la Hisa la London (LSE) nchini Uingereza na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), imeeleza kuwa wakia 104,985 za dhahabu zilizouzwa katika robo ya kwanza ya mwaka huu ziliendana na kiwango cha uzalishaji.

Acacia imejikuta ikiwa katika kipindi kirefu cha sintofahamu baada ya kuingia katika mgogoro na Serikali mapema mwaka 2017 kutokana na madai ya ukwepaji kodi wa mabilioni ya shilingi tuhuma ambazo  kampuni hiyo kubwa ya madini nchini imekuwa ikizikanusha wakati wote.

Kampuni mama ya Acacia, Barrick Gold ya nchini Canada mapema mwaka huu iliafikiana na Serikali kuanza kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa mwaka 2017 ili kumaliza mgogoro huo ikiwemo kulipa Dola za Marekani milioni 300 (takriban Sh700 bilioni) kama ishara ya nia njema.