October 7, 2024

Madeni vyuo vikuu yaiweka njia panda Serikali

Madeni hayo ya wafanyakazi yanajumuisha malimbikizo ya posho za majukumu, kiinua mgongo, nyumba za kuishi yanazidi kuongezeka, jambo linaloweza kuathiri utoaji elimu bora kwa wanafunzi.

  • Madeni hayo wanayodai wafanyakazi wa taasisi hizo yanazidi kuongezeka, jambo linaloweza kuathiri utoaji elimu bora kwa wanafunzi.
  • Malimbikizo ya madeni hayo yanajumuisha malimbikizo ya posho za majukumu, kiinua mgongo, nyumba za kuishi na ongezeko la mishara.
  • Serikali imesema inaendelea na uhakiki wa madeni hayo na yatalipwa mchakato ukikamilika.

Dar es Salaam. Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2017/2018 kuhusu mashirika ya umma imeeleza kuwa madai ya watumishi ikiwemo posho za majukumu na kiinua mgongo katika taasisi za elimu ya juu ambayo hayajalipwa yanaweza kushusha morali ya utendaji kazi kwa wafanyakazi na kuathiri mwenendo wa utoaji elimu katika taasisi hizo. 

Kuanzia 2016/2017 hadi 2017/2018 madeni hayo yameongezeka kwa zaidi ya asilimia 40 katika vyuo vikuu vyote vilivyokaguliwa ambapo 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ambayo iliwekwa wazi kwa umma Aprili 10, 2019 na CAG Profesa Mussa Assad imeeleza kuwa ukaguzi wa shughuli mbalimbali za taasisi za elimu ya juu ulibaini kuwa madeni ya wafanyakazi yamebakia kuwa makubwa au kuzidi kuongezeka kwa muda. 

“Kwa mfano, kutoka mwaka 2016/2017 hadi 2017/2018 madeni yanayohusiana na malipo ya posho ya majukumu kwa Chuo Kikuu cha Mzumbe na Ardhi yameongezeka hadi kufikia Sh. bilioni 3.41 na Sh. bilioni 2.26 kutoka Sh. bilioni 1.49 na Sh. bilioni 1.48 mtawalia,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.

Wakati wafanyakazi wa Mzumbe na Ardhi wakidai malipo ya posho, wenzao wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) wanadai Sh5.59 bilioni za kiinua mgongo kwa wafanyakazi ambao wamekamilisha mikataba yao. 

Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kilikuwa na Sh6.80 bilioni kama madeni ya wafanyakazi tangu Juni 2017, ikiwa ni posho za nyumba na madeni mengineyo. 

Madeni ya vyuo hivyo vitano pekee ni takribani Sh19.10 bilioni ambayo hajalipwa hadi kufikia mwaka 2017/2018.

Hata hivyo, ripoti hiyo inaeleza kuwa kasi ya ulipaji madeni hayo ni ndogo jambo linaloacha manung’uniko kwa wafanyakazi wa taasisi hizo katika kutimiza majukumu yao ya kila siku. 

“Taasisi ya Uhasibu Arusha (IAA) pia ilikuwa na deni la Sh519 milioni, ikiwa ni madeni yatokanayo na posho za wafanyakazi. Hata hivyo, limeshuka kwa Sh6  milioni tu (2016/17) kutoka Sh 525 milioni). Madai ya watumishi ambayo hayajalipwa yanaweza kushusha morali ya utendaji kazi kwa wafanyakazi,” inaeeleza sehemu ya ripoti hiyo. 


Soma zaidi:


Kila taasisi ya elimu ya juu ina kanuni au sera zake zinazotoa miongozo ya stahiki mbalimbali zinazolipwa kwa wafanyakazi wake kama vile kiinua mgongo. 

Kanuni hizo zinatoa mwongozo juu ya malipo ya kiinua mgongo kwa wafanyakazi wa mikataba baada ya kukamilisha muda wao wa mkataba. 

Hata hivyo, Serikali kwa nyakati tofauti imekuwa ikisema inahakiki madeni ya wafanyakazi wa Serikali wakiwemo wa taasisi za juu na mchakato ukikamilika wote watalipwa stahiki zao. 

“Wakati ninakiri jitihada za Serikali kuhakiki madai ya wafanyakazi kabla ya kulipwa, ninaisihi Serikali kuangalia muda wa uhakiki wa madeni hayo, kwani kutumia muda mrefu kuhakiki madeni, kunazidisha ongezeko la madai na kuzidi kuongeza mzigo kwa Serikali,” amesema Prof Assad. 

Ukumbi wa Nkurumah uliopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambao umekuwa ukitumika kwa shughuli mbalimbali za kitaaluma. Picha|Mtandao.

Februari 2018, Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) walitishia kugomea kazi ikiwa malimbikizo ya madai yao hayatalipwa kwa wakati. Wanataaluma hao walisema kuwa wanadai zaidi ya Sh2 bilioni.

Mapema mwaka huu, Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udasa) ilisema italazimika kuingia kwenye mgogoro na Serikali ikiwa madai ya muda mrefu yanayofikia Sh11 bilioni hayatalipwa mwishoni mwa mwezi Januari, 2019. 

Madai hayo yanajumuisha malimbikizo ya posho ya nyumba ya kuishi na nyongeza ya mishahara.