November 24, 2024

Usiyoyajua kuhusu hifadhi ya Taifa ya Mkomazi

Imesheheni vivutio mbalimbali vya ndege, wanyama pori wakiwemo faru weusi ambao wako hatarini kutoweka duniani.

  • Imesheheni vivutio mbalimbali vya  ndege, wanyama pori wakiwemo faru weusi ambao wako hatarini kutoweka duniani.
  • Tafsiri kamili ya Mkomazi ni  kijiko cha kipare kisichokuwa na tone lolote la maji. Huenda neno hilo pia linathibitisha hali halisi ya upatikanaji wa maji katika eneo hilo ulivyo mgumu.
  • Hifadhi hiyo imewahi kutembelewa na Mjukuu wa Malkia Elizabeth II wa Uingereza, Prince William.

Dar es Salaam. Ni miaka zaidi ya nane imepita tangu pori la akiba la Mkomazi libadilishwe na kuwa Hifadhi ya Taifa. Yapo mengi ya kujivunia kutoka katika hifadhi hiyo ambayo imekuwa kiungo muhimu cha kuitangaza Tanzania kimataifa.

Lakini imekuwa kivutio kikubwa cha watalii wanaokuja kuangalia  aina mbalimbali za ndege na faru weusi ambao wanapatikana katika maeneo machache duniani.

Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi ambayo inapatikana katika mikoa miwili ya Kilimanjaro na Tanga ikiwa ndani ya wilaya za Same na Lushoto,  ilianzishwa kama Pori la Akiba lililomegwa kutoka katika Pori kubwa la Akiba la Ruvu mwaka 1951.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), hifadhi hiyo ina ukubwa wa kilomita za mraba 3,245 ambapo ilipendekezwa kuwa Hifadhi ya Taifa kwa misingi ya kunusuru maeneo na rasilimali zilizomo kutokana na matumizi yasiyoendana na uhifadhi endelevu.

Kama wewe umejipanga mwaka huu kutembelea hifadhi za Taifa basi huenda Mkomazi ikawa ni sehemu sahihi kwako kutokana na sifa za kipekee ambazo hazipatikani katika hifadhi zingine nchini. 

Mkomazi hutumika kama kituo kwa ndege ambao husafiri kati ya bara Ulaya na Afrika. Ni hifadhi inayowavutia wageni wa kimataifa wanaopenda kuangalia aina mbalimbali za ndege. 

Ndege hao wanaohama hutumia maeneo ya hifadhi kama vituo vyao vya kupumzikia wakiwa wanaelekea kusini mwa Afrika au kipindi wanapokuwa wanarudi makwao  katika Bara la Ulaya.

Lakini hifadhi ya Taifa ya Mkomazi imesheheni wanyama kama Swala, Twiga, Cholawa, Simba, Faru, Tembo, Pundamilia na Mbwa mwitu ambao hutembea kwa makundi na kuwa kivutio kikubwa kwa watalii. 

Ukiwa katika hifadhi hiyo unaweza kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo kutembelea maeneo ya kupumzika wageni (Picnic Site) na sehemu za kupiga mahema na kambi ya kulala wageni iliyopo karibu na Makao Makuu ya hifadhi hiyo iitwayo “Babu’s Camp”. 

Vipi kuhusu huduma za malazi na maeneo ya jirani kutembelea?

Ukiacha na huduma za malazi ndani ya hifadhi kupitia kambi za kuhamishika, Mji wa Same una huduma za hoteli ambazo zitakupa kufurahia hali ya hewa ya baridi na mandhari nzuri ya miinuko na miteremko ya milima inayopatikana katika hifadhi hiyo.

Kipindi kizuri cha kutembelea Mkomazi ni kiangazi ambacho huanza Juni hadi Septemba na ni wakati mzuri wa kuona wanyama na ndege hata na mandhari nzuri ya hifadhi baada ya kuisha kwa mvua za masika ambazo hunyesha Februari hadi Mei na kabla ya kuanza kwa mvua za vuli za Septemba hadi Novemba. 

Mjukuu wa Malkia Elizabeth II wa Uingereza, Prince William akifanya utalii katika hifadhi ya Mkomazi alipotembelea mwaka 2018. Picha|Mtandao.

Asili ya Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi

Kwa mujibu wa maelezo yaliyopo katika tovuti ya Tanapa, jina la ‘Mkomazi’ ni neno la kabila la Wapare, mojawapo ya makabila ya Tanzania ambapo wazungumzaji wengi wa kabila hilo wanapatikana mkoa wa Kilimanjaro.

Katika kabila la Wapare, neno ‘Mko’ maana yake ni kijiko na sehemu ya pili ya neno hilo ‘Mazi’ linamaanisha maji. 

Tafsiri kamili ya Mkomazi ni  kijiko cha kipare kisichokuwa na tone lolote la maji. Huenda neno hilo pia linathibitisha hali halisi ya upatikanaji wa maji katika eneo hilo ulivyo mgumu.


 Zinazohusiana:


Unafikaje katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi

Sifa nyingine ya Mkomazi ni uwezo wake wa kufikika kirahisi kutokana na kuwa karibu na barabara kuu ya Arusha-Dar es Salaam. 

Mtalii atatumia njia panda ya kuelekea Gonja, mwendo wa takribani kilomita 10 hadi kufika katika geti kuu la hifadhi ya Taifa ya Mkomazi la Zange huku akifaidi safu za milima ya Usambara zilizo pembezoni mwa barabara hiyo. 

Lakini lipo geti lingine la Gonja ambalo ni mwendo wa kilomita 66 hadi kufika katika hifadhi.

Barabara ya Arusha-Dar es Salaam ambayo inaunganisha njia panda ya Gonja hadi katika hifadhi ya Mkomazi ambapo pembeni ni milima ya Usambara. Picha|Mtandao.

 Watu maarufu waliowahi kutembelea hifadhi hiyo

Septemba 2018, Mjukuu wa Malkia Elizabeth II wa Uingereza, Prince William wakati wa ziara yake nchini, alitembelea Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi kujifunza zaidi juu ya juhudi zilizofanywa na hifadhi hiyo za kuwalinda Vifaru weusi.

Lakini pia akiwa Mkomazi alifanikiwa kuona jinsi hifadhi hiyo inavyofanya kazi katika  kuwatunza na kuwatengenezea mazingira mazuri vifaru hao wazaliane.

Idadi ya vifaru hao weusi wanakadiriwa kufikia 50  na uongozi wa hifadhi unafanya juhudi mbalimbali za kuhakikisha vifaru wengine wanaongezeka zaidi na kukabiliana na vitendo vya ujangili vinavyohatarisha uhai wa wanyama hao duniani. 

Pia imejenga mabwawa ya maji ili kukabiliana na tatizo la upatikanaji wa maji na kuwahakikishia wanyama pori maji ya uhakika.