Nukta Africa yateuliwa katika mpango wa Google
Mpango huo kuziwezesha kampuni za habari duniani zinazochipukia kuongeza ufanisi wa utendaji kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Kampuni nyingi za habari duniani huomba kuingia katika mpango huo lakini Google News Initiative huchagua zile zinazoonyesha mkazo katika matumizi ya teknolojia katika mchakato mzima wa uzalishaji habari. Picha|Mtandao.
- Mpango huo huziwezesha kampuni za habari duniani zinazochipukia kuongeza ufanisi wa utendaji kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
- Pia imepewa leseni ya miaka miwili bila malipo kutumia bidhaa zote za Google zinazosaidia uzalishaji, uchakataji na usambazaji wa habari zikiwemo Gmail, Google drawing, Sound Cloud.
- Nukta Africa inamiliki tovuti ya habari ya nukta.co.tz na hufanya mafunzo ya habari za takwimu na matumizi ya dijitali katika kuzalisha habari.
Dar es Salaam. Kampuni ya teknolojia na habari ya Nukta Africa imechaguliwa kuingia katika programu ya kampuni ya Marekani ya Google kupitia mpango wa Google News Initiative G Suite unaolenga kuziwezesha kampuni za habari duniani zinazochipukia kuongeza ufanisi wa utendaji kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Nukta Africa imechaguliwa katika programu hiyo na kupatiwa leseni ya miaka miwili bila malipo kutumia bidhaa zote za Google zinazosaidia uzalishaji, uchakataji na usambazaji wa habari zikiwemo Gmail, Google drawing, Sound Cloud kutokana na kuwekeza zaidi katika matumizi ya mifumo ya kidijitali na takwimu kuhabarisha umma.
Nukta Africa inamiliki tovuti ya habari ya nukta.co.tz na hufanya mafunzo kwa wanahabari na wadau wengine katika uandishi wa habari za takwimu na matumizi ya dijitali katika kuzalisha habari.
Kampuni nyingi za habari duniani huomba kuingia katika mpango huo lakini Google News Initiative huchagua zile zinazoonyesha mkazo katika matumizi ya teknolojia katika mchakato mzima wa uzalishaji habari.
Google News Initiative ni mradi wa kampuni ya teknolojia ya Google unaolenga kusaidia vyombo vya habari duniani kukua na kukabiliana na changamoto zilizopo katika kipindi hiki cha ukuaji wa kasi wa maudhui ya kidijitali.
“Hongera! Tunapenda kukujulisha kuwa Nukta Africa imechaguliwa kuwa miongoni wa wanufaika wa mpango wa Google News Initiative G Suite,” inasomeka sehemu ya taarifa kutoka Google News Initiative kwa Nukta Africa.
Programu hiyo itaiwezesha kampuni ya Nukta Africa iliyojikita katika uchambuzi wa habari za kina za teknolojia, safari, biashara, elimu na takwimu kuboresha utendaji kazi kwa kutumia mifumo ya dijitali kuanzia usakaji wa habari, uchakataji na usambazaji.
Pia ni fursa ya kuiwezesha kuwa na biashara endelevu na kuwafikia wasomaji kwa urahisi kwa kuwapa maudhui yenye ubora kulingana na mahitaji yao.
Soma zaidi:
Programu hiyo ya Google News Initiative G-Suite inayoishia Desemba 31, 2021 inatoa zana (tools) mbalimbali ikiwemo Cloud Speech to Text na Cloud Translation API ambazo zinasaidia katika kupata tafsiri sahihi ya maudhui yanayochapishwa mtandaoni.
Zana nyingine ni BigQuery iliyopo katika mfumo wa mashine ya kujifunzia ambayo ni mahususi kwa kufuatilia tabia za watumiaji wa mtandao na mambo wanayopenda.
“Hii ni heshima kubwa kwa Nukta Africa na tasnia ya habari kwa ujumla nchini,” amesema Nuzulack Dausen, Mkurugenzi Mtendaji na Mhariri Mkuu wa Nukta Africa.
“Kuna vyombo vingi vya habari duniani hupenda kuingia katika mpango huu lakini siyo vyote hufanikiwa…hii ni dhahiri kuwa nukta.co.tz pamoja na kuchapisha kwa lugha ya Kiswahili bado mchango wake unathaminika hata katika nyanja za kimataifa.”
Dausen amesema wataendelea kuhamasisha matumizi ya takwimu na zana za kidijitali kwa wanahabari na jamii nzima nchini kuhakikisha kuwa wanapata taarifa sahihi zinazochochea maendeleo na kwa njia za teknolojia ya kisasa kupitia mafunzo na habari.