November 24, 2024

Kanuni kuzuia matumizi mifuko ya plastiki zakamilika

Serikali imesema kanuni tayari zimeandaliwa na wanakamilisha majadiliano na wadau ili kutekeleza marufuku hiyo katika muda uliotajwa.

Mifuko ya plastiki imekuwa ikitumika katika shughuli mbalimbali lakini wadau wanasema siyo rafiki kwa mazingira. Picha|Mtandao.


  • Serikali imesema kanuni tayari zimeandaliwa na wanakamilisha majadiliano na wadau ili kutekeleza marufuku hiyo katika muda uliotajwa.
  • Viwanda vinavyozalisha mifuko ya plastiki na wadau wengine kujitayarisha kwa kubadili teknolojia na kutathmini fursa zinazojitokeza katika kuzalisha mifuko mbadala.

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amesema kanuni za kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki tayari zimeandaliwa na wanakamilisha majadiliano na wadau ili ikiwezekana ifikapo Julai 1 mwaka huu iwe mwisho wa matumizi ya mifuko hiyo nchini. 

Amesema kanuni hizo zitachapishwa kwenye gazeti la Serikali ili kuweka utaratibu mzuri wa utekelezaji na kuhakikisha marufuku hiyo inafanikiwa bila kikwazo. 

Makamba alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kaliua (CUF) Magdalena Sakaya aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa haraka kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki kama zilizofanya nchi zingine ikiwemo Zanzibar, Kenya na Rwanda kwa sababu imezuia ajira za watanzania wanaotengeneza mifuko mbadala na ni chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazingira. 

Makamba amesema katika majibu yake kuwa wanaendelea na majadiliano na wadau mbalimbali na kama itawezekana marufuku hiyo itatangazwa wakati wa usomaji wa bajeti ya Wizara ya Muungano na Mazingira Aprili 16, 2019 ambapo utekelezaji wake utaanza Julai 1 mwaka huu. 

“Wiki hii nimeelekezwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa nimeagizwa nikutane na taasisi za Serikali zinazohusika na jambo hili NEMC (Barza la Taifa la Mazingira), TBS (Shirika la Viwango Tanzania), TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania), Uhamiaji, Polisi, watu wa Customs (Forodha) ili kuweka utaratibi wa namna tunavyoweza kupiga marufuku,” 

“Hapa nilipo ninazo kanuni nimeshazitengeneza  ambazo zinangoja kuchapishwa kwenye gazeti la Serikali. Kwa hiyo inawezekana kabisa kama tutakubaliana katika vikao vya wiki hii na inayokuja basi tarehe 1 Julai ikawa mwisho wa matumizi ya plastiki hapa nchini,” amesema Makamba.


Zinazohusiana:


Amesema Serikali inalichukulia jambo hilo kwa uzito, inalifanyia kazi na hakuna sababu ya kuendelea kutumia plastiki hapa nchini na yeye kama Waziri wa Mazingira anakubali hilo. 

Hata hivyo, ametoa angalizo kuwa wanahitaji maandalizi ya kitaasisi na utaratibu mzuri ili kuhakikisha wanafanikiwa kwa sababu zipo baadhi ya nchi zilipiga marufuku lakini hakuna kilichofanyika.

Ikiwa marufuku hiyo itafanikiwa, huenda ikafungua milango ya ajira nyingi kwa vijana wanaojihusisha na utunzaji wa mazingira hasa kutengeneza mifuko mbadala ambayo imekuwa kivutio kwa shughuli za utalii na rafiki kwa mazingira. 

Naye Naibu Waziri Mussa Sima amehimiza viwanda vinavyozalisha mifuko ya plastiki na wadau wengine kujitayarisha kwa kubadili teknolojia na kutathmini fursa zinazojitokeza katika kuzalisha mifuko mbadala hasa katika kipindi hiki cha mpito wakati taratibu za maamuzi ya Serikali zikikamilishwa.