Tanzania ilivyojipanga kufaidika soko la kimataifa la muhogo
Serikali imesema itaendelea kutoa elimu kwa wakulima, kujenga viwanda vya kusindika zao hilo ili kuongeza usafirishaji wa bidhaa.
Mahitaji ya zao la muhogo na bidhaa zake katika soko la kimataifa ni makubwa kwa sababu matumizi yake katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji. Picha|Mtandao.
- Serikali imesema itaendelea kutoa elimu kwa wakulima, kujenga viwanda vya kusindika zao hilo ili kuongeza usafirishaji wa bidhaa.
- Muhogo hautumiki tu kwa chakula bali unatumika katika shughuli za kuunganisha chuma na mbao ambapo mahitaji makubwa yako Ulaya, Marekani na China.
- Hutumika kama zao la biashara na wakati huohuo ni zao la chakula.
Dar es Salaam. Katika kuhakikisha inatumia na kufaidika na soko la kimataifa la muhogo linalotumika kuunganisha chuma, Serikali imesema itaendelea kutoa elimu kwa wakulima, kujenga viwanda vya kusindika zao hilo ili kuongeza usafirishaji wa bidhaa.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda wakati akizungumza leo (Aprili 5, 2019) bungeni amesema mahitaji ya zao la muhogo na bidhaa zake katika soko la kimataifa ni kubwa kwa sababu matumizi yake katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji.
Kakunda alikuwa akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Tanga Mjini, Mussa Mbaruku kwa niaba ya Mbunge viti maalum mkoa wa Tanga, Sonia Magogo aliyetaka kujua Serikali ina mkakati gani wa kutafuta soko la uhakika kwa zao la muhogo ndani na nje ya nchi.
Amesema kwa sasa muhogo hautumiki tu kwa chakula bali unatumika katika shughuli za kuunganisha chuma na mbao ambapo mahitaji makubwa yako Ulaya, Marekani na China.
“Kwa sasa zao la muhogo limepewa kipaumbele maalum duniani, kutokana na muhogo hausindikwi kutengeneza unga wa ugali, uji, mkate na biskuti pekee yake. Unga wa muhogo siku hizi unatumikaa kwenye uunganishaji wa chuma, mbao, kutengeneza gundi na matumizi mengine mengi sana,” amesema Kakunda.
China pekee inahitaji tani 2.5 za muhogo kwa mwaka ambapo amesema wanaongeza kasi ya ujenzi wa viwanda vya kuchakata zao la muhogo ili kuongeza thamani ya zao hilo na biashara ya kimataifa.
“Mwaka huu pekee yake ukiacha viwanda vitano vinavyonunua muhogo wa mkulima ikiwemo kile kilichopo Handeni, viwanda viwili vitakuwa vimefunguliwa kabla ya Juni 2019, kimoja Lindi na kingine Pwani,” amesema Kakunda.
Soma zaidi:
- Wakulima washauriwa kutumia teknolojia ya kisasa kilimo cha umwagiliaji
- Rasmi:Tabora ndiyo makao ‘makuu ya kuku wa kienyeji Tanzania’
Katika kuhakikisha wanafikia hazma hiyo, Serikali inaendelea kuwawesha wakulima kwa mitaji na kutoa elimu ya kilimo bora cha muhogo, utafiti, kutumia mbegu bora ambapo Wizara ya Viwanda na Biashara na Kilimo zinashirikiana kuhakikisha mkulima anaongeza uzalishaji kutokana na elimu inayoipata.
Serikali imeweka vipaumbele vitatu ambavyo vimewekewa msisitizo wa uwekezaji kwenye sekta ya viwanda. Vipaumbele hivyo ni; viwanda vya kusindika mazao ya kilimo ili kuongeza thamani sambamba na kulinda jasho la mkulima.
Kipaumbele cha pili ni kutengeneza bidhaa za majumbani kama vyakula, nguo, mafuta ya kula, viatu, samaki na vifaa tegemezi katika sekta ya ujenzi kama thamani za viti, mabati ili kuharakisha ubora wa maisha na maendeleo. Na kibaumbele cha tatu ni viwanda vinavyoajiri watu wengi ili kuhakikisha ajira kwa vijana.
Kwa hapa Tanzania, muhogo hulimwa kwa wingi katika mikoa ya Mara, Mwanza, Kigoma, Mtwara, Lindi, Pwani, Ruvuna, Tanga, Morogoro, Shinyanga.
Kwa hapa Tanzania, muhogo hulimwa kwa wingi katika mikoa ya Mara, Mwanza, Kigoma, Mtwara, Lindi, Pwani, Ruvuna, Tanga, Morogoro, Shinyanga ambapo hutumika kama zao la biashara na wakati huohuo ni zao la chakula.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Uzalishaji wa Chakula kwa kipindi cha mwaka 2018/2019 iliyotolewa na Wizara ya Kilimo Februari 2019 inaeleza kuwa katika msimu wa kilimo wa 2017/2018 uzalishaji wa zao la muhogo ulikuwa tani 2.7 milioni ambapo mkoa wa Kigoma uliokongoza kwa kuzalisha tani 445,526 sawa na asilima 15.9 ya uzalishaji wote katika kipindi hicho.