October 6, 2024

Unayotakiwa kufanya kuepuka madhara ya mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini

Mambo hayo ni pamoja na kuepuka kukaa au kuegesha vyombo vya usafiri na usafirishaji chini ya miti mikubwa, kutokucheza kwenye kingo za mito na kutokuvuka katika madaraja na vivuko vilivyojaa maji.

  • Epuka kukaa au kuegesha vyombo vya usafiri na usafirishaji chini ya miti mikubwa maana matawi au mti vyaweza kuangukia chombo kutokana na ardhi kujaa maji.
  • Watoto, wanafunzi, watu wazima wanashauriwa kutokucheza kwenye kingo za mito kwa kuwa kipindi hiki cha mvua kingo hizo huwa dhaifu hivyo ni rahisi kubomoka au mtu kuteleza na kusombwa na maji.
  • Wananchi wanashauriwa kuendelea kufuatilia taarifa za utabiri kutoka TMA na kuzingatia tahadhari zilizotolewa na marejeo yake.

Dar es Salaam. Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limewataka wananchi kuchukua tahadhari mbalimbali ikiwemo kuepuka kukaa na kuegesha vyombo vya usafiri chini ya miti mikubwa maana wanaweza kuangukiwa na kusababisha madhara. 

Machi 29 mwaka huu, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitoa tahadhari ya kunyesha mvua kubwa katika kipindi cha wiki mbili za Aprili katika maeneo mengi yanayopata mvua za masika hasa mikoa ya mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa, Morogoro, Lindi, Mtwara, Pwani na Dar es Salaam.

Mvua hizo zimeanza kunyesha tayari katika maeneo tajwa baada ya athari ya upungufu wa mvua uliotokana na vimbunga vilivyojitokeza mfululizo katika bahari ya Hindi.

Kutokana na mvua hizo, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limewaelekeza wananchi wote waishio mabondeni na kandokando ya mito, wamiliki wa vyombo vya usafiri na usafirishaji kuchukua tahadhari ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea katika kipindi hicho. 

Katika taarifa iliyotolewa leo (Aprili 4, 2019) kwa umma na Kamishna wa Operesheni wa jeshi hilo, Billy Mwakatage imewataka watoto, wanafunzi, watu wazima kutokucheza kwenye kingo za mito kwa kuwa kipindi hiki cha mvua kingo hizo huwa dhaifu hivyo ni rahisi kubomoka au mtu kuteleza na kusombwa na maji.

Iwapo maji yatakuwa yamejaa kwenye kivuko au daraja kiasi kwamba daraja au kivuko hicho hakionekani, watu wasijaribu kuvuka kwa miguu au kwa yombo vya safiri na usafirishaji kwa sababu kuna uwezekano mkubwa kivuko au daraja litakuwa limesombwa na maji. 

Eneo la Victoria jijini Dar es Salaam wakati mvua kubwa ikiendelea kunyesha ambapo watumiaji wa vyombo vya moto wametahadharishwa kuwa makini wakati wakitumia miundombinu ya barabaraba. Picha|Daniel Samson.

Jambo nyingine ni ambalo Kamishna Mwakatage anatahadharisha ni  “kuepuka kukaa au kuegesha vyombo vya usafiri na usafirishaji chini ya miti mikubwa maana matawi au mti vyaweza kuangukia chombo kutokana na ardhi kujaa maji na hivyo mizizi kushindwa kuhimili uzito wa mti na kusababisha mti huo kuanguka na kusababisha uharibifu mkubwa wa mall hata kudhuru maisha.”

Kutokana na mvua hizo pia kuna uwezekano wa mawe makubwa au udongo kuporomoka kutoka milimani au miti kuanguka na kuziba barabara, madereva wanaaswa kuwa makini kwa kuendesha vyombo vyao kwa mwendo unaokubalika ili kuepuka ajali zisizo za lazima. 

“Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limejipanga na liko imara kuhakikisha linatoa huduma bora, sahihi na kwa wakati. Hivyo wananchi mnapoona hatari yoyote tafadhali toeni taarifa mapema kwa kupiga namba ya dharura 114,” ameeleza Kamishana Mwakatage katika taarifa hiyo. 


Soma zaidi: 


TMA ilisema kunyesha kwa mvua kubwa katika kipindi hiki kunaweza kuathiri shughuli za kiuchumi na kijamii katika baadhi ya maeneo nchini ikiwemo sekta ya usafiri hasa barabara zinazotumika kupitisha magari ya abiria na mizigo.

Wananchi wanashauriwa kuendelea kufuatilia taarifa za utabiri kutoka TMA na kuzingatia tahadhari zilizotolewa na marejeo yake pamoja na kupata na kuzingatia ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.