Ukwasi BOT wapunguza tatizo la mzunguko mdogo wa fedha
Serikali imesema kwa sasa nchi haina tatizo la mzunguko mdogo wa fedha katika soko kutokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa kukabiliana na tatizo hilo ikiwemo kuongeza ukwasi kwenye uchumi.
- Serikali imesema kwa sasa nchi haina tatizo la mzunguko mdogo wa fedha katika soko kutokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa kukabiliana na tatizo hilo ikiwemo kuongeza ukwasi kwenye uchumi.
- Utaratibu wa BoT wa kutoa mikopo ya muda maalum kwa mabenki pamoja na kununua fedha za kigeni kutoka kwenye soko la jumla la mabenki pia umesaidia.
Dar es Salaam. Serikali imesema kwa sasa nchi haina tatizo la mzunguko mdogo wa fedha katika soko kutokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa kukabiliana na tatizo hilo ikiwemo kuongeza ukwasi kwenye uchumi.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji ametoa ufafanuzi huo leo (April 3, 2019) bungeni mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Momba, David Silinde (Chadema) aliyetaka kujua sababu za mzunguko mdogo wa fedha katika soko.
Dk Kijaji amesema katika kutatua changamoto ya kupungua kwa mzunguko wa fedha katika soko, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilichukua hatua mbalimbali za kuongeza ukwasi kwenye uchumi ikiwemo kushusha riba inayotumika kuzikopesha benki za biashara nchini (discount rate) kutoka asilimia 16 Machi, 2017 hadi asilimia 7, Agosti 2018.
“Benki Kuu ilipunguza kiwango cha kisheria cha sehemu ya amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu na mabenki ya biashara (Statutory Minimum Reserve Requirement (SMR) kutoka asilimia 10 hadi asilimia nane mwezi April 2017 pamoja na kuruhusu mabenki kutumia asilimia 10 ya sehemu ya SMR kama chanzo kimojawapo cha kusaidia hali ya ukwasi kwenye uchumi”, amesema Dk Kijaji.
Soma zaidi:
- NMB yaingiza sokoni huduma tatu za kidijitali kwa mpigo
- BoT yashusha tena riba kwa benki za biashara Tanzania
Amesema BoT ilianzisha utaratibu wa kutoa mikopo ya muda maalum kwa mabenki pamoja na kununua fedha za kigeni kutoka kwenye soko la jumla la mabenki ili kuongeza ukwasi kwenye uchumi.
Amebainisha kuwa mzunguko wa fedha katika uchumi unaendana na malengo pamoja na mahitaji halisi ya shughuli za kiuchumi zilizopo kwa sasa.
Aidha, amesema Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania inatekeleza sera ya fedha inayolenga kusimamia mzunguko wa fedha unaoendana na mahitaji halisi ya uchumi kwa lengo la kudumisha utulivu wa mfumuko wa bei na hivyo kuweka mazingira mazuri ya ukuaji wa uchumi.