November 24, 2024

Rais Magufuli amshukia mkandarasi anayejenga barabara ya Mtwara-Mnivata

Amesema halidhishiwi na kasi yake ya ujenzi wa barabara hiyo tangu alipokabidhiwa mwaka 2017 mpaka leo haijakamilika.

Barabara ya Mtwara hadi Mnivata yenye kilomita 50 inayojengwa kwa kiwango cha lami na mkandarasi wa kampuni ya Dott Services Limited ya nchini Uganda. Picha|Mtandao.


  • Amesema mkandarasi huyo wa kampuni ya Dott Services Limited ya nchini Uganda hana rekodi nzuri ya utendaji na amekuwa akichelewesha miradi anayokabidhiwa.
  • Amesema halidhishiwi na kasi yake ya ujenzi wa barabara hiyo tangu alipokabidhiwa mwaka 2017 mpaka leo haijakamilika.
  • Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano yatakiwa kumsimamia kuhakikisha anakamilisha ujenzi ifikapo Agosti mwaka huu.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amekiri kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa barabara ya Mtwara hadi Mnivata yenye kilomita 50 inayojengwa kwa kiwango cha lami na mkandarasi wa kampuni ya Dott Services Limited ya nchini Uganda huku akitaka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuhakikisha ujenzi huo unamilika kwa wakati. 

Ujenzi wa barabara hiyo iliyopo mkoani Mtwara unagharimu Sh89.5 bilioni na ni sehemu ya barabara ya Mtwara-Newala-Masasi yenye kilomita 210 ambayo inaunganisha wilaya zote za mkoa huo ambapo kukamilika kwake kutafungua fursa nyingi za kiuchumi zilizopo katika mikoa ya kusini. 

Rais Magufuli ameonyesha masikitiko yake leo (Aprili 3, 2019) wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara hiyo ambapo amesema haridhishwi na kasi ya mradi huo ulioanza mwaka 2017 na mapaka sasa barabara iliyokusudiwa ya lami hajaikamilika. 

“Nimefurahi kuwa mradi huu umeanza kutekelezwa, sijafurahishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huu. Msema kweli ni mpenzi wa Mungu mradi hauendi vizuri,” amesema Rais. 

Amesema rekodi za mkandarasi anayejenga barabara hiyo si nzuri kwa sababu katika miradi mingine aliyopewa ikiwemo ujenzi wa barabara ya Same-Mkumbala mkoani Kilimanjaro hakukabidhi kwa wakati. 

“Lakini performance (utendaji) ya makandarasi huyu nataka mimi nieleze pamoja na kwamba amecheleweshewa certificate (vyeti) zake karibu nne na wamesema fedha nazo zimekuja bilioni 16 lakini rekodi ya mkandarasi huyu siyo nzuri. Dott company alifanya kazi kwenye barabara kutoka Same-Mkumbala alichelewa hivyo hivyo, nashangaa kwanini mlimpa kazi hapa,” amesema Rais. 

Tayari makandarasi huyo amepewa Sh16 bilioni kama malipo ya awali na anatakiwa kukamilisha kazi hiyo Agosti mwaka huu. 


Soma zaidi:


Kutokana na kusuasua kwa ujenzi wa barabara hiyo, Rais ameagiza mkandarasi kufanya kazi usiku na mchana kwasababu wananchi wamesubiri sana kupata barabara hiyo. 

Ameitaka wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasilianio kumsimamia mkandarasi huyo na kuhakikisha hapewi kazi nyingine mpaka amalize mradi huo hata kama ameshinda tenda kutokana na rekodi yake kutokuwa nzuri. 

Pia ameiagiza wizara hiyo kutenga pesa zaidi kwa ajili ya barabara hiyo ili ijengwe kwa kiwango cha lami hadi kufikia Masasi. 

Mtwara ni miongoni mwa mikoa ya kimkakati ambao ni kitovu cha shughuli za uchumi katika mikoa ya kusini, ambapo Serikali imeendelea kufanya maboresho ya miundombinu ikiwemo bandari na uwanja wa ndege wa Mtwara ili kufungua fursa mbalimbali za uwekezaji. 

Naye Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasilianoi, Mhandisi Isack Kamwelwe amesema barabara hiyo ina umuhimu mkubwa katika biashara ya kimataifa hasa kuunganisha na nchi ya Malawi.