October 6, 2024

Rais Magufuli akataa kuzilipa halmashauri ushuru wa korosho

Amesema zimeshindwa kusimamia zao hilo na kuwaacha wakulima wakilanguliwa kwa bei ndogo.

  • Amesema zimeshindwa kusimamia zao hilo na kuwaacha wakulima wakilanguliwa kwa bei ndogo.
  • Ameagiza Wakurugenzi wa Halmashauri wasiwasumbue wakulima kwa kuwakata makato ya tozo na ushuru. 
  • Serikali imesema itawalipa wakulima pesa wakulima wote licha ya muda uliowekwa kupita.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema Halamshauri za Wilaya katika mikoa inayolima korosho hazitapata ushuru wa mauzo ya msimu uliopita kwasababu zimeshindwa kusimamia maendeleo ya zao la korosho ikiwemo kusimamia bei nzuri kwa wakulima. 

Awali wakulima walikuwa wakikatwa Sh254 kwa kilo moja ya korosho kama tozo na ushuru wa Halmashauri. 

Novemba 17, 2018 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala mkoani Mtwara, Mussa Chimae alisema wakulima hao walikuwa wakikatwa Sh46.5 ya ushuru wa Halmashauri sawa na asilimia tatu ya bei elekezi, Sh20 ya mfuko wa elimu na makato mengine ya vyama vya ushirika na gharama walizojiwekea vijiji kwa ajili ya maendeleo yao. 

Rais Magufuli ametoa msimamo huo leo (Aprili 3, 2019) wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Mtwara hadi Mnivata ya kilomita 50, ambapo amesema Serikali haitazilipa halmashauri hizo pesa ya ushuru wa korosho kwa sababu bei iliyopangwa awali kabla Serikali haijaingilia kati ilikuwa inawaumiza wakulima. 

Amesema nia ya Serikali kununua korosho ilikuwa ni moja tu ya kuwakomboa wananchi waliokuwa wanapewa bei ya Sh1,500 kwa kilo ambapo waliopata bahati walikuwa wanalipwa Sh2,000 kwa kilo lakini Kangomba walikuwa wananunu mpaka Sh500 kwa kilo.

“Ndiyo maana tukapanga bei ya Sh3,300 ili wananchi wanyonge wakulima waweze kufaidika na korosho yao. Sasa huwezi Serikali ikanunua korosho kwa kilo Sh3,300 halafu ianze tena kulipia kodi kwenye halmashauri ambayo ilishindwa kununua korosho,” amesema Rais Magufuli.


Zinazohusiana:


Amesema sababu kubwa ni kuwa halmashauri hizo zimeshindwa kusimamia zao la korosho na zikitaka kupata ushuru huo ziwajibike katika kusimamia maslahi ya wakulima. .

“Kwa hiyo hakuna ushuru wa Halmashauri hata senti tano hampati, lazima tufike mahali tuambizane ukweli tu, mkitaka ushuru msimamie vizuri zao la korosho kwa kuwapa bei nzuri wakulima na ninyi mpate ushuru wenu.”. 

“Siwezi nikakusanya hela kutoka mikoa mingine nije niwalipe halmashauri ya huku ushuru, mkitaka ushuru simamieni vizuri zao la korosho muwalipe wananchi hawa bei nzuri,” amesema Rais.

Amebainisha kuwa Serikali haifanyi biashara na kitendo cha kununua korosho yote ya wakulima ilikuwa ni kuwasaidia wasilanguliwe na wanyabiashara binafsi, ambapo fedha hizo zilichukuliwa katika Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) na haiwezi tena kukopa ili kuzilipa halmashauri. 

Katika hatua nyingine, amezitaka halmashauri hizo zisiende kuwabughudhi wakulima kwa kuanza kuwadai ushuru huo kwa sababu zilikataa kununua korosho yao.

“Wananchi hawa wananyanyaswa, estimate (makadirio) ya bodi ya korosho ilikuwa Sh1,500 kwa kilo wakati wananchi hawa wamehangaika, serikali kwa huruma, Serikali inayosikiliza watu tukasema hapana hawa watu hamna kuonewa. Tukachukue fedha kupitia benki ya maendeleo ya kilimo, tukakopa ili tuje tulipe huku, leo tukope tena kuja kuwapa watu wa halmashauri? Hakuna,” amesisitiza Rais. 

Hata hivyo, Serikali imesema itawalipa fedha wakulima wote korosho itakapokamilisha uhakiki licha kuwa muda uliowekwa wa Machi 31, 2019 kupita.