Rais Magufuli ataja sababu kuu tatu upanuzi uwanja wa ndege wa Mtwara
Amesema mkoa wa Mtwara uko mpakani, una fursa nyingi za uwekezaji ambapo uboreshaji wa miundombinu ya usafiri ni muhimu
- Amesema mkoa wa Mtwara uko mpakani, una fursa nyingi za uwekezaji ambapo uboreshaji wa miundombinu ya usafiri ni muhimu
- Sababu nyingine ni kukiwezesha kiwanja hicho kupokea ndege kubwa za ndani na nje ili kuongeza kasi ya huduma za usafiri wa ndege nchini.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameeleza sababu kuu tatu za upanuzi na uboreshaji wa uwanja wa ndege wa Mtwara ikiwemo uchakavu wa miundombinu na fursa za uwekezaji zilizopo katika mkoa huo ambazo zikitumika vizuri zitasaidia kukuza uchumi.
Amesema mkoa wa Mtwara upo mpakani ambapo ni mkoa wa kimkakati unaoiunganisha Tanzania na nchi jirani za Msumbiji na Comoro ambazo zimekuwa na mafungamano ya kibiashara ya muda mrefu na Tanzania.
Rais Magufuli aliyekuwa akihutubia wananchi wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la ukarabati na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mtwara leo (Aprili 2, 2019) amesema uwanja huo ulijengwa mwaka 1952 na haujafanyiwa marekebisho kwa muda mrefu ambapo Serikali inapanua uwanja huo ili kurahisisha shughuli za uchumi.
“Serikali inapanua uwanja huu wa ndege kurahisisha shughuli za kiuchumi lakini uwanja huu umejengwa mwaka 1952 mimi bado sijazaliwa haiwezekani uwanja kama huu utuvushe kiuchumi ni vyema tukaufanyia marekebisho sasa,” amesema Rais Magufuli.
Amesema sababu nyingine ni kuwa mkoa wa Mtwara uko kimkakati na upo mpakani unaunganisha nchi na mataifa jirani ambayo tunafanya nayo biashara. Pia una fursa nyingi za uwekezaji ambazo zinahitaji miundombinu bora itakayovutia kuwekeza katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
“Sababu ya pili ni kama nilivyosema kuwa mkoa huu upo mpakani na pia una fursa nyingi za uwekezaji, wawekezaji wa utalii wengi watakuja mtwara ndio maana tumeamua kupanua uwanja huu,” amebainisha.
Kutokana na umuhimu wake katika mikoa ya Kusini, Serikali iliamua kujenga bandari ya Mtwara ili kurahisisha shughuli za ugavi n auchukuzi hasa usafirishaji wa mazao ya biashara ikiwemo korosho na saruji inayotoka katika kiwanda cha saruji cha Dangote kilichopo Mtwara mjini.
Amesema ununuzi wa ndege mpya nane na kufufuliwa kwa shirika la ndege la Tanzania (ATCL) nako kumechangia kuongezeka kwa safari za ndani ambazo zinahitaji miundombinu ya kisasa itakayowezesha ndege kutua katika viwanja vyote nchini ili kufungua fursa mikoani ukiwemo mkoa wa Mtwara ambao unasifika kwa upatikanaji wa gesi asilia.
“Sababu ya tatu kama mnavyofahamu serikali imeamua kufufua shirika lake la ndege kwa kununua ndege mpya nane ambapo sita tayari zimeshawasili, tumenunua ndege hizi kwa fedha za watanzania. haiwezekani ndege hizo ziwe zinatua kwenye viwanja vingine vikubwa zisifike hapa, ndio maana tumesema wananchi wa Mtwara lazima wafaidike na matunda ya jasho lao,” amesema Rais.
Rais John Magufuli akikata utepe kuashairia uzinduzi wa upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mtwara akiwa na viongozi mbalimbali wa Serikali. Picha| Michuzi blog.
Upanuzi wa uwanja wa Ndege Mtwara utagharimu Bilioni Sh50.4 bilioni ambapo unasimamiwa na Mkandarasi kutoka kampuni ya Beijing Construction Engineering Group (BCEG) ya nchini China.
Katika hatua nyingine, Rais amemtaka Mkandarasi aliyekabidhiwa kazi ya upanuzi wa uwanja huo kuhakikisha anakamilisha kazi kwa wakati na asipofanya hivyo hatua zitachukuliwa dhidi yake.
“Sasa nataka kumuambia huyu Mkandarasi atakapozitapa hizi fedha 10% ni Bilioni 4.5 na 15% ni Bilioni 7.5, ninyi mpeni hizo asilimia 15, ndani ya siku 5 mpeni hizo pesa! sasa asifanye kazi, haki ya Mungu atakoma, afanye kazi usiku na mchana,” amesisitiza Rais Magufuli.
Soma zaidi:
- Fastjet yafanya mabadiliko makubwa huduma za vyakula, mizigo
- Mkimbizi wa zamani wa Afghan azunguka Dunia kwa ndege
Kiwanja hicho cha ndege cha Mtwara kilijengwa kwa mara ya kwanza na kuanza kutoa huduma katika miaka 1952 kikiwa na barabara mbili za kurukia na kutua ndege, barabara kuu ya kuruka na kutua ndege ilikua imejengwa kwa kiwango cha lami yenye urefu wa mita 2,258 na upana wa mita 30 na barabara ndogo ya changarawe ilikua imejengwa kwa urefu wa mita 1,158 na upana wa mita 30.
Mpango kabambe ulioandaliwa umelenga kupanua kiwanja hicho kutoka daraja la 3C lasasa kwenda daraja la 4E ambalo litaweza kuhudumia ndege kubwa za ndani, kazi ambayo inafanyika kwenye mkataba wa sasa ni kupanua kutoka upana wa mita 30 hadi 45, njia ya ndege kwa urefu kutoka 2,258 hadi 2800 na kuboresha matabaka ya barabara.