Kwanini wafanyabiashara wanawekeza katika matumizi ya mitandao ya kijamii?
Ni nafuu na rahisi kuwafikia wateja wengi kwa wakati mmoja na inasaidia kuimarisha mahusiano ya kibiashara bila kuathiri umbali na mazingira ya muuzaji na mtumiaji wa bidhaa au huduma.
- Ni nafuu na rahisi kuwafikia wateja wengi kwa wakati mmoja na inasaidia kuimarisha mahusiano ya kibiashara bila kuathiri umbali na mazingira ya muuzaji na mtumiaji wa bidhaa au huduma.
- Ni njia mojawapo ya kuendana na mabadiliko ya teknolojia na sayansi yanayotokea duniani katika utendaji wa sekta mbalimbali za uzalishaji na manunuzi.
Ni ukweli usiopingika kuwa kutokana na kukua kwa teknolojia, matumizi ya mitandao ya kijamii katika shughuli mbalimbali yamepewa kipaumbele zaidi kuliko siku za nyuma.
Moja ya matumizi ya mitandao ya kijamii ni katika biashara ambapo wajasiriamali hasa vijana wanaomiliki simu janja hupendelea kutangaza biashara zao katika mitandao hiyo ili kuwafikia watu wengi kwa muda mfupi na kwa urahisi zaidi.
Kuna sababu kadha wa kadha zinazowafanya wajasiriamali wengi kuwekeza katika kutangaza biashara zao mtandaoni kutokana na tafiti iliyofanywa na mtandao wa three girls media umebainisha mambo mbalimbali yanayowasukuma wafanyabiashara kutumia mitandao ya kijamii kama njia mojawapo ya kutangaza huduma na bidhaa zao.
Urahisi na unafuu wa kuwafikia wateja
Moja ya umuhimu wa kutumia mitandao ya kijamii ni pamoja na unafuu na urahisi wa kuwafikia walengwa wa huduma au bidhaa yako kwa gharama ndogo tu za kifurushi za intaneti. Mitandao inakusaidia kuwafikia wateja popote walipo bila kuwafuata katika maeneo yao.
Matumizi ya mitandao ya kijamii ni fursa kwa wafanyabiashara kuwafikia wateja wao hata kama katika tofauti. Picha|Mtandao.
Ni fursa kwa wateja kuijua bidhaa kwa undani
Wateja hupata nafasi ya kujua bidhaa mpya zinapoingia sokoni na kuwapa fursa ya kujua kwa undani huduma au bidhaa kutokana na matangazo yanayowekwa kwenye mitandao ya kijamii. Hiyo inampa muda wa kutosha mtumiaji kufanya utafiti wa manufaa ya bidhaa kabla hajaitumia.
Soma zaidi:
- Namna huduma kwa wateja inavyoweza kukuza brand ya biashara
- Mambo ya kuzingatia unapoanzisha brand yako ya biashara
Inajenga mahusiano mazuri
Inajenga uhusiano mzuri kati ya wateja na wauzaji kutoka kampuni mbalimbali zinazotoa huduma na bidhaa bora zenye kuleta matokeo chanya kwa watumiaji.
Mahusiano hayo yanajengwa zaidi kupitia kubadilishana mawazo, elimu ya matumizi ya bidhaa na huduma. Ukaribu wa mteja na mtoa huduma au bidhaa haukwamishwi na umbali au maeneo waliyopo kwasababu wakati wowote wanaweza kuwasiliana kwa kutumia mtandao.
Ni dhahiri kuwa mitandao ya kijamii katika kipindi hiki ambacho dunia inashuhudia mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia katika shughuli mbalimbali za uzalishaji na maendeleo hauepukiki.
Mtu au kampuni yenye nia ya kukuza bishara yake ni lazima itakumbatia na kwenda sambamba na watumiaji wa mitandao ya kijamii ili kuwapata watu sahihi watakaonunua na kutumia bidhaa au huduma zake.
Wewe ni kijana mwenye ndoto za kuanzisha biashara basi mitandao ya kijamii ni muhimu katika mipango ya kutafuta soko na kuwafikia watu wengi kwa muda mfupi.