Binti wa kitanzania abuni pedi zinazoweza kutumika kwa zaidi ya miaka miwili
Ni uvumbuzi utakaowasaidia wanawake wasiokuwa na fedha kumuda taulo hizo za kike za kijisitiri.
- Pedi hizo unaweza kuzitumia mara nyingi zaidi bila kuchakaa na hufuliwa kirahisi tu.
- Historia halisi ya maisha yake ndio chanzo cha wazo hilo.
- Ni uvumbuzi utakaowasaidia wanawake wasiokuwa na fedha kumuda taulo hizo za kike za kijisitiri.
Dar es salaam. Licha ya Serikali na wadau wa maendeleo kufungua milango zaidi kwa watoto wa kike kupata elimu bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa taulo za kike (pedi) kujisitiri wakiwa katika siku zao.
Changamoto hiyo inawakumba zaidi wasichana wanaoishi vijijini ambao hulazimika kukaa nyumbani mpaka siku zao ziishe, wakati huo huo wakipitwa na vipindi vya masomo darasani jambo linaloathiri mwenendo wa ufaulu.
Utafiti uliofanywa na nukta.co.tz kwenye baadhi ya maduka Jijini Dar es Salaam unabainisha kuwa pedi zinakadiriwa kupatikana kwa bei ya Sh1,500 hadi Sh 2,000 kwa pakiti yenye pedi nne na saa zingine bei hiyo hutofautiana kutoka eneo moja hadi lingine.
Kutokana na changamoto hiyo ambayo pia aliipitia katika ukuaji wake, mwanadada Lucy Odiwa(35) ameibuka na wazo la kutengeneza pedi zinazoweza kutumika zaidi ya mara moja akiwa na lengo kubwa la kuhakikisha kuwa mtoto wa kike hakosi masomo kwa kisingizio cha kukosa pedi.
Baadhi ya wanafunzi waliofikiwa na pedi zinazoweza kutumika hadi miaka miwili. picha| women choce
“Nilipata mzunguko wangu wa hedhi nikiwa na miaka 16 huku nikiwa darasani. Kwa kuwa sikua na pedi ilinilazimu kuchukua soksi iliyokuwa imeanikwa na kuitumia kama mbadala wa pedi,” amesema.
Kwa kuwa alikuwa akisoma shule ya bweni, Odiwa hakuweza kupata pedi kirahisi hivyo alitumia soksi na vitambaa hadi pale mzunguko wake wa hedhi ulipoisha.
“Kutokana na historia hiyo, nilifikiria nini kinaweza kuwa tiba kwa wasichana wanaopitia hali kama niliyopitia awali ndivyo nilipata wazo la kutengeneza salama pads,” amesema Odiwa.
Katika maelezo yake, Odiwa amesema pedi hizo hutengenezwa kwa malighafi rafiki kwa msichana yeyote. Malighafi hayo ni vitambaa aina tatu ambavyo kila kimoja kina kazi yake ikiwemo kunyonya maji na kingine cha kuzuia kuvujisha unyevunyevu.
“Ni pedi ambazo haziwashi, hazitoi harufu kwa sababu malighafi zake ni rafiki na pia nirahisi kutumia ukilinganisha na pedi zingine,” amesema.
Muonekano wa pedi ambayo inaweza kutumika hadi miaka miwili. picha| women choice
Katika hali ya kawaida msichana hununua pedi kwa kukidhi mzunguko mzima kwa makadirio ya Sh7,000 lakini Odiwa amesema pedi hizo hupatikana kwa Sh5,000 kwa pakiti ambapo kila pakiti huja na pedi nne.
Ameeleza zaidi kuwa salama pads hazina kemikali yoyote ukilinganisha na pedi zilizopo dukani ambazo zina kemikali lakini watengenezaji hawajaweka bayana kemikali ambazo pedi hizo hutengenezewa na hivyo hupelekea baadhi ya watumiaji kupatwa na adha pindi wazitumiapo.
Tofauti na pedi nyingine, Salama pads zinaweza kutumika kwa kipindi cha miaka miwili na hadi mitatu kwa hazichakai na zinatumika zaidi ya mara moja. Hata hivyo, mafanikio hayo ni kulingana na usafi wa mtumiaji.
“Kipindi hicho cha kuisha ni kuchakaa tuu kwani hata nguo mpya huchakaa kulingana na muda. Pedi hiyo Inapofuliwa ni vyema ikaanikwa juani na hakuna haja ya kuona aibu kwani muonekano wake unavutia,” amesema Lucy.
Amesema kuwa pedi hizo ni kheri zikakauka kwa jua na kama mtu anaona shida kuianika hadharani basi anaweza kuzianika juani na kisha kuzifunika na khanga.
Miale ya jua husaidia kuua vimelea na kufanya pedi hiyo kuwa safi na salama.Na kupitia kuanikwa juani, mtu hulazimika kuifua kwa makini kwani hakuna apendaye kuanika kitu kichafu ama kiulicho fubaa, anaeleza.
Laura Laurence (22) amesema mbali na bei kuwa juu kidogo, pedi za madukani humuwasha mara kadhaa na kuna muda mwingine zinakua kubwa na zinamfanya kukosa uhuru kimavazi kwani inamlazimu avae magauni pekee.
“Saa zingine ninashindwa kuvaa suruali ya kubana kwani kama pedi ni kubwa inanikosesha uhuru wa kuvaa hivyo,” amesema.
Licha ya ubora na uzuri wa salama pads, Odiwa hajafanikiwa kuvuka mipaka ya mkoa wa Tanga katika utoaji wa huruma hiyo. Na hata katika mkoa huo wa Tanga, ameeleza kuwa wanaonufaika na bidhaa hiyo kwa sasa ni wanafunzi kwani ndio wenye uhitaji zaidi.
“Tunawapatia kwa mkopo chini ya usimamizi wa mwalimu wa afya na hata wanaoweza kununua wananunua,” ameeleza.
Hata hivyo, Lucy bado anatazamia kuongeza uzalishaji wa pedi hizo kwani zimepata uhitaji mkubwa ndani na nje ya nchi.
Ameeleza kuwa changamoto kubwa ni upatikanaji wa kitambaa cha kuzuia unyevunyevu kwani kinapatikana kwa shida.
Hapo awali amesema alikipata kwenye mtumba lakini hakuweza kukipata tena. Kwa sasa ameagizia kitambaa hicho nchini China ilihali akiwa na dhamira ya kufikia watu wengi zaidi na kuhakikisha tabu aliyoipata haiwapati wengine.
“Nimepata oda ya pedi 10,000 lakini siwezi kuzitengeneza kwa sababu malighafi hayo sio rahisi kuyapata. Nimeagiza malighafi kutoka China na natarajia kupata mzigo huo muda wowote kutokea sasa,” amesema Lucy.
Sambamba na uvumbuzi huo, Lucy amesema anajitahidi kuhakikisha kuwa elimu juu ya mzunguko wa hedhi inawafikia watu wote wakiwemo Wavulana na wanaume kwa kuwa wao nao wanapaswa kutambua hedhi sio swala la kuonea aibu kwa kuwa ni kheri kwa msichana.
“Ifike wakati katika familia kuwepo na bajeti nyumbani kwa ajili ya mzunguko wa hedhi kwani kina baba wengi hufikiria matumizi ya mtoto wa kike ni chakula na mavazi pekee,” amesema.
Kutokana na uvumbuzi huo, Lucy anajivunia kufundisha wasichana takribani 200 kuwa wasambazaji wa pedi hizo, kushinda tuzo ya SDH&Her za nchini uingereza, kuwa mshindi wa tatu wa mashindano ya wavumbuzi chipukizi ya SeedStars Dar es Salaam.
Kubwa zaidi analojivunia mwanadada huyo uwezo wa kuwakufikia wasichana takribani 40,000 ambao watahudhuria masomo siku zote bila kukosa kwa sababu tu za kuwa hedhini.