Siri ya sanamu ya Askari katikati ya jiji Dar es Salaam
Kabla ya sanamu hiyo kulikuwa na sanamu nyingine ya kigogo wa Kijerumani Meja Hermann von Wissmann iliyong’olewa baada ya Vita ya Kwanza ya Dunia.
- Ina miaka 92 toka ilipozinduliwa rasmi na Ni kumbukumbu ya askari waliokufa wakati wa vita ya kwanza ya dunia.
- Kabla ya sanamu hiyo kulikuwa na sanamu nyingine ya kigogo wa Kijerumani ya Meja Hermann von Wissmann.
Dar es Salaam. Inawezekana ni wakazi wachache wa jiji la Dar es Salaam wanapopita ilipo sanamu ya Askari kwenye makutano ya barabara ya Samora, Maktaba, Azikiwe na Makunganya wanafahamu kwanini sanamu ya Askari wa kiafrika ipo pale na maana yake.
Kwanini sanamu hilo la askari lipo katikati ya jiji likiwa na sare ya jeshi la kikoloni la King’s African Rifles akiwa ameshika bunduki yenye kisu na isiwe sanamu ya kiongozi yoyote mwingine nchini?
Naam! Unakumbuka hata Mbunge wa Ulanga Mashariki Goodluck Mlinga wakati akichangia mjadala wa bajeti bungeni mwaka 2016 alipendekeza sanamu hiyo ya askari iondolewe na iwekwe za watu wengine walioleta mchango kwa Taifa akiwemo Diamond.
Hata hivyo, mapendekezo ya wengi yakiwemo ya Mlinga huenda yasifanikiwe kwa kuwa sanamu hiyo ya Askari ni kumbukumbu muhimu ya kuwakumbuka askari wenyeji waliopigana wakati wa vita ya kwanza ya Dunia kuanzia mwaka 1914 hadi 1918.
Sanamu la Askari katikati ya Jiji la Dar es Salaam. Sanamu hili limekuwa ni moja ya vivutio vya vikuu kwa wageni wanaotembelea jiji hili. Picha|Jamii Forums.
Sanamu hiyo ilichongwa na Mwingereza anayeitwa James Alexander Stevenson na kuzinduliwa kwa mara ya kwanza Novemba 1927 na maelezo katika sanamu hiyo yaliandikwa na Rudyard Kipling.
Zinazohusiana:
- Lijue ghorofa la kwanza kujengwa Dar
- Atiman House: Moja ya maghorofa matano ya kwanza kujengwa Dar lililoficha historia lukuki
Ukisogelea sanamu hiyo kuna maandishi ya kumbukumbu kwa Kiingereza na Kiswahili pamoja na michoro ambayo angalau unaweza kubahatika kufahamu jambo kidogo kuihusu.
“Huu ni ukumbusho wa askari Waafrika wenyeji waliopigana katika Vita Kuu na ni ukumbusho pia kwa wapagazi ambao walikuwa miguu na mikono ya majeshi. Ni ukumbusho pia kwa watu wote waliotumika wakafa kwa ajili ya mfalme na nchi yao katika Afrika Mashariki kwenye Vita Kuu toka mwaka 1914 mpaka 1918. Ukipigania nchi yako japo umekufa watoto wako watalikumbuka jina lako,” yanayosemeka maelezo hayo.
Mbali na sanamu hiyo kuwepo kwa miaka 92 sasa toka izinduliwe rasmi lakini wengi wao huenda pia hawajui kuwa kabla ya hapo kulikuwa na sanamu nyingine iliyokuwepo pale kabla ya vita ya kwanza ya dunia.
Kabla ya sanamu ya askari huyo maarufu, ilikuwepo sanamu nyingine ya kigogo wa Serikali ya kikoloni ya Kijerumani Meja Hermann von Wissmann katika eneo hilo hilo.
Mtandao wa afrika-hamburg.de unaeleza kuwa sanamu hiyo ya kwanza ilizinduliwa rasmi jijini Dar es Salaam mwaka 1908 wakati huo barabara hiyo ikijulikana kama Wissmannstrasse/Bismarckstrasse.
Wissmann alikuwa gavana wa kijerumani Afrika ya Mashariki kuanzia mwaka 1853 – 1905. Sanamu hiyo ilibuniwa na Adolf Kürle nilizinduliwa miaka minne baada ya kifo cha Wissmann.
Kwa mujibu wa kitabu cha ‘Dar es Salaam – A history of Urban Space and Architecture’ gavana huyo ndiye aliyefanikiwa kushinda vita dhidi ya Abushiri bin Salim al-Harthi katika ukanda wa Pwani karne ya 19.
Baada ya Wajerumani kushindwa vita kuu ya kwanza ya dunia mwaka 1919 sanamu hiyo iliondolewa na kupelekwa Jijini London na kuhifadhiwa katika jumba la makumbusho ya vita (Imperial War Museum).
Kwa sasa sanamu lililopo la Askari limekuwa alama ya utambulisho wa jiji la Dar es Salaam na moja ya vivutio vya kitalii.