November 24, 2024

Rais Trump asitisha safari zote za ndege aina ya Boeing 737 Max 8

Amechukua uamuzi huo baada ya kuongezeka shinikizo la kimataifa kumtaka afuate nyayo za nchi nyingine duniani zilizozuia matumizi ya ndege hizo baada ya ajali iliyotokea Ethiopia.

  • Amechukua uamuzi huo baada ya kuongezeka shinikizo la kimataifa kumtaka afuate nyayo za nchi nyingine duniani zilizozuia matumizi ya ndege hizo.
  • Nayo kampuni ya Boeing imetangaza kusitisha safari za ndege hizo ili kuwahakikishia wateja wake usalama.
  • Mpaka sasa nchi 50 ikiwemo Marekani zimezuia mashirika yao ndani ya ndege kutumia ndege hizo.

Dar es Salaam. Rais wa Marekani, Donald Trump amesitisha mara moja kwa muda safari zote za ndege za kampuni ya Boeing aina ya Boieng 737 MAX 8, baada ya ndege kama hiyo ya Shirika la ndege la Ethiopia kuanguka wiki iliyopita na kuua watu wote 157 waliokuwemo ndani. 

Trump aliyekuwa akizungumza mubashara na Wanahabari katika Ikulu ya Marekani jana (Machi 13, 2019) amesema  uamuzi wa kusitisha ndege hizo unatokana na kuongezeka kwa shinikizo la kimataifa lililoitaka Marekani kuzipiga marufuku ndege hizo kuruka katika anga yake kama zilivyofanya nchi nyingine. 

Rais huyo amesema ndege ambazo ziko safarini zitazuiwa mara baada ya kutua katika viwanja vya ndege mpaka hapo mambo yatakapokuwa mazuri na ana uhakika kampuni ya Boeing itatoa majibu sahihi kutokana na ajali iliyotokea Ethiopia.

Baada ya marufuku hiyo ya  Trump, Shirika la Mamlaka ya Anga la Marekani (FAA) na kampuni ya Boeing zimetangaza kusitisha mara moja kurusha ndege hizo baada ya wachunguzi kubaini ushahidi mpya katika eneo ambako ndege ya shirika la ndege la Ethiopia ilianguka.

Katika taarifa yake, Boeing imesema imefanya mashauriano na FAA na bodi ya Taifa ya Safari (NTSB) na kuamua kusitisha mara moja kwa muda safari zake zote za ndege 371 za aina hiyo ili kuchukua tahadhari na kuhakikisha usalama wa watumiaji wa chombo hicho cha usafiri. 

Hata hivyo, FAA imeeleza kuwa katika ukaguzi wake umeonyesha hakuna matatizo ya mfumo wa utendaji kazi yaliyobainika katika ndege hiyo lakini uchunguzi zaidi unaendelea.


Soma zaidi: Shirika la ndege la Ethiopia limesitisha safari zote za ndege aina ya Boeing 737


Kampuni hiyo ya Marekani imesema imesitisha usafiri wa ndege zote 371 aina ya Boeing 737 Max 8 zinazofanya safari maeneo mbalimbali duniani. 

Ajali ya ndege iliyoanguka Ethiopia imetokea miezi mitano baada ya ndege ya aina hiyo ya Shirika la ndege la Indonesia, Lion Air kuanguka baharini na kuwaua watu 189. 

Marekani inaungana na nchi 50 ikiwemo China, Uingereza, India na Australia ambazo zimepiga marufuku mashirika ya ndani ya ndege ya nchi zao kutumia ndege hizo ikiwa ni hatua ya kuwalinda raia wao.

Nyongeza na mashirika ya habari ya kimataifa.