Kampuni yafungua mlango kununua chumvi ya wakulima Tanzania
Ni kampuni ya NeelKanth Salt Limited ya Mkuranga, Pwani inahitaji rasilimali ghafi ya chumvi ili kukidhi mahitaji yake ya kutengeneza chumvi bora kwa ajili ya watanzania.
- Kampuni ya NeelKanth Salt Limited ya Mkuranga, Pwani inahitaji rasilimali ghafi ya chumvi ili kukidhi mahitaji yake ya kutengeneza chumvi bora kwa watanzania
- Baadhi ya wakulima wamesema kwa sasa malighafi hiyo haipatikani kirahisi maana msimu wa manunuzi umepita.
Dar es Salaam. Watanzania wanaojihusisha na kilimo cha chumvi huenda wakafaidika na fursa ya soko ya zao hilo kutokana na kampuni ya NeelKanth Salt Limited inayotengeneza chumvi ya Neel kuonyesha nia ya kununua rasilimali ghafi ya chumvi kutoka kwa wavunaji wadogo wadogo ili kukidhi mahitaji yake ya uzalishaji nchini.
Tanzania chumvi inalimwa zaidi katika mikoa ya pwani ya kusini ikiwemo mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani na Kigoma ambapo wakulima hutegemea zaidi maji ya bahari, maziwa na visima kupata rasilimali hiyo muhimu kwa maisha ya binadamu.
Kampuni hiyo yenye kiwanda cha kutengeneza chumvi wilaya ya Mkuranga mkoa wa Pwani imetoa taarifa kwa umma leo (Machi 11,2019) ambapo imeeleza kuwa inahitaji kukidhi mahitaji ya uzalishaji na hivyo inawaalika wavunaji wadogo wadogo kuiuzia chumvi ghafi ili kutengeneza chumvi bora kwa ajili ya watanzania.
“Bidhaa namba moja ya chumvi nchini Tanzania, Neel Salt inatangaza kununua rasilimali ghafi ya chumvi iliyo bora kutoka kwa wavunaji wadogo wadogo ili kukidhi mahitaji yake,” inaeleza taarifa hiyo kwa umma.
Imeeleza zaidi kuwa fursa hiyo inawahusu zaidi wamiliki wa mashamba ya chumvi ambao wanapenda kuwa sehemu ya wauzaji kuwa wanapaswa kuwasiliana na kampuni hiyo.
Jinsi chumvi inavyovunwa kabla ya kuuzwa viwandani kwaajili ya hatua nyingine zaidi. Picha| tabiayanchi.blogspot.com
Kampuni hiyo bado haijaeleza inahitaji kiasi gani cha rasilimali hiyo na kwa muda gani. Juhudi za kuupata uongozi wa kampuni hiyo hazikufanikiwa kutokana na simu kuita kwa muda mrefu bila kupokelewa.
Hiyo ni fursa kwa wakulima wa zao hilo ambao wanategemea kama sehemu ya kujiingizia kipato? www.nukta.co.tz imeongea na baadhi ya wakulima wa mkoani Mtwara ambao wamekuwa na mawazo tofauti ambapo wamedai kuwa msimu wa kuuza malighafi hiyo umepita na kwa sasa haipatikana kirahisi.
“Msimu wa chumvi umeshapita yaani hapa mpaka mwezi wa tisa kipindi cha kiangazi ndio inapatikana kiurahisi,” amesema Adinour Mamboya mvunaji chumvi kutoka Kilwa Masoko.
Kutokana na mahitaji makubwa ya malighafi ya chumvi, kampuni za kutengeneza chumvi zimekuwa zikiagiza nje ya nchi ili kuendeleza viwanda VYAO.
Zinazohusiana:
- TADB yakusudia kujenga kiwanda cha kuchakata chai Iringa
- Chamwino kujenga kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi
Mamboya amesema uamuzi wa kiwanda hicho ni wa busara kwa sababu itakuwa mfano kwa kampuni kuthamini malighafi za ndani zinazotengenezwa na watanzania.
“Hizi kampuni kubwa mara nyingi wanabagua sana chumvi zetu na wananunua nje hivyo ushauri wangu wathamini vya ndani,” amesisistiza Mamboya.