October 7, 2024

Chati nne zilizoficha siri ya safari ya usawa wa kijinsia Tanzania

Chati hizo zinabainisha hali hali ya usawa wa kijinsia katika sekta mbalimbali za maendeleo ambazo zinagusa zaidi maisha ya wanawake na watoto.

  • Chati hizo zinabainisha hali halisi ya usawa wa kijinsia katika sekta mbalimbali za maendeleo ambazo zinagusa zaidi maisha ya wanawake na watoto.
  • Kuna kila sababu ya kufuatilia mwenendo wa safari ya usawa wa kijinsia wa 50 kwa 50 ifikapo mwaka 2030 ikiwemo katika sekta za fedha, kilimo na afya.
  • Wadau wa masuala ya kijinsia watakiwa kuongeza ushawishi ili kuongeza idadi ya wasichana wanaofika vyuo vikuu na vikao vya maamuzi.

 Dar es Salaam. Wakati wanawake wa Tanzania wakiungana na wenzao duniani kusherekea Siku ya Wanawake Duniani, kuna kila sababu ya kufuatilia mwenendo wa safari ya kufikia usawa wa kijinsia wa 50 kwa 50 ifikapo mwaka 2030.

Siku ya Wanawake Duniani (International Women’s Day) huadhimishwa Machi 8 kila mwaka ili kutathimini maendeleo ya wanawake katika jamii katika nyanja za siasa na uchumi.

Kwa kutambua hilo nukta.co.tz tunakuletea baadhi ya takwimu muhimu katika chati ama ‘Infographics’ nne zinazoelezea namna wanawake na wanaume wanavyoshirikishwa katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo ikiwemo sekta ya fedha, kilimo, afya na hata ajira nchini Tanzania. 

 

Kuna nini katika mashirika ya umma?

Licha ya kuwa Serikali na wadau wa maendeleo wamefanya jitihada mbalimbali kumuwezesha mtoto wa kike kupata elimu lakini idadi ya wanawake wanaoajiriwa katika mashirika ya umma kwa takwimu rasmi za mwaka 2014 bado ni ndogo. 

Ripoti ya Utafiti wa Nguvukazi wa mwaka 2014 (Integrated Labour Force Survey 2014) iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaeleza kuwa wanawake waliokuwa wameajiriwa katika mashirika ya umma (parastatals) walikuwa asilimia 18 tu kati ya watumishi wote. Hii ina maana kuwa ni wastani wa mtumishi mmoja tu kati ya watano katika mashirika hayo alikuwa mwanamke.

Hata hivyo, kilimo na shughuli za nyumbani zimeendelea kuwa kuwabeba wanawake licha ya kuwa hawafaidiki sana na sekta hizo kwa kuwa baadhi wanatumia dhana duni kulimia na shughuli za nyumbani huwa na ujira mdogo kuliko kwenye mashirika.

 Wanawake waishio vijijini na changamoto za uzazi

Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania mwaka 2015-2016 unathibitisha kuwa wanawake wanaoishi vijijini, wanaoishi katika kaya maskini sana na wasiosoma wanazaa watoto wengi ukilinganisha na wale wanaoishi mjini au waliobahatika kupata elimu.

Hali hiyo imekuwa ikiwaweka katika hatari ya kupata matatizo ya kiafya ikiwemo vifo kutokana na changamoto za upatikanaji wa huduma bora za afya katika maeneo yao. 

Safari bado ndefu 50 kwa 50 elimu ya juu Tanzania

Wakati wanawake wakisherehekea mafanikio waliyopata, wanapaswa kuongeza ushawishi kuwawezesha wasichana wengi kufika elimu ya juu ili kupata fursa ya kuingia katika sekta rasmi inayohitaji ujuzi na maarifa kutekeleza majukumu ya kikazi. 

Kwa mujibu wa takwimu za Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) zilizochapishwa kwenye kitabu cha Takwimu za Mwaka 2016 (Tanzania in Figures 2016) ambazo hutolewa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), kati ya mwaka 201/2011 hadi 2015/2016 udahili wa wanafunzi wa kike vyuo vikuu umedumu kwa wastani wa asilimia 35.4, sawa na theluthi tu ya wanafunzi wote wanaodahiliwa.


Zinazohusiana:


Uchambuzi wa takwimu hizo uliofanywa na nukta.co.tz unabainisha kuwa wanaume waliodahiliwa vyuo na vyuo vikuu ni takriban mara mbili zaidi ya wanawake licha ya kuwa katika ngazi za chini za elimu kama msingi na sekondari idadi yao huwa karibu sawa. 

Kazi kubwa imefanyika katika elimu ya msingi na sekondari, ni wakati wa Serikali na wadau kuongeza nguvu ili kuweka mazingira rafiki yatakayowasaidia wasichana wengi kupata elimu ya juu na kutumia ipasavyo fursa zilizopo za kiuchumi, kijamii, kisiasa na teknolojia.

 

Taasisi za fedha zimewaacha nyuma wanawake

Changamoto za umiliki wa rasilimali kama ardhi zinazowakabili wanawake nchini zimewafanya wakose dhamana ya kupata mikopo katika taasisi za fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli zao. 

Shirika la Chakula Duniani (FAO) linaeleza kuwa wanawake wanachangia zaidi ya asilimia 40 ya nguvu kazi katika sekta ya kilimo lakini mikopo haiwafikii kwa kiwango cha kuridhisha, jambo linalorudisha nyuma juhudi zao za kujikwamua kiuchumi na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa familia na Taifa. 

Iwapo wanawake wangepata fursa sawa za huduma za kifedha huenda wangekuwa na maendeleo sawa na wanaume au hata kuwazidi kabisa.