Poland yaangazia kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji Tanzania
Uwekezaji huo utasaidia kuendeleza ardhi ya kilimo na kufungua milango ya ajira kwa vijana.
Kilimo cha umwagiliaji kikiboreshwa kinaweza kuwa mkombozi kwa wakulima wa Tanzania. Picha|Mtandao.
- Uwekezaji huo utasaidia kuendeleza ardhi ya kilimo na kufungua milango kwa vijana.
- Tanzania ina hekta 29.4 milioni lakini ni asilimia 1.6 tu ndiyo imeendelezwa huku wakulima wengi wakilima kienyeji.
Dar es Salaam. Huenda mauzo ya mazao ya Tanzania kwa nchi ya Poland yakaongezeka, baada ya nchi hiyo kuonyesha nia ya kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji ili kutumia vizuri ardhi iliyopo na kuongeza uzalishaji wa mazao na ukuaji wa uchumi.
Kwa mujibu wa kanzi data ya biashara ya Umoja wa Mataifa (United Nations COMTRADE) inaeleza kuwa mauzo ya Tanzania nchini Poland kwa mwaka 2017 yalikuwa Dola za Marekani 11.05 milioni (takriban 26.1 bilioni) huku tumbaku ikiongozwa kwa asilimia 92.5 ya mauzo yote yaliyofanyika katika nchi hiyo mwaka 2016.
Uwekezaji huo katika sekta ya kilimo cha umwagiliaji, uliwekwa wazi na Balozi wa Poland nchini Tanzania, Krzysztof Buzalski alipofanya mazungumzo na uongozi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIC) jijini Dar es Salaam, ambapo amesema Tanzania na Poland zinategemea sana kilimo kama shughuli ya kiuchumi, hivyo nchi yake inaona ni wakati muafaka kuisadia Tanzania kwa ujuzi ilionao wa miaka 30 katika sekta ya kilimo.
“Kilimo cha umwagiliaji kinawapunguzia mzigo wakulima wa kusubiri mvua za msimu na mabadiliko ya hali ya hewa na kuwawezesha kuongeza mavuno,” amesema Balozi Buzalski wakati akizungumza na wanahabari baada ya mkutano na NIC.
Hata hivyo, amebainisha kuwa uwekezaji huo unahitaji umakini katika kuchagua njia ya kuutekeleza kwa sababu utahusisha wadau mbalimbali kutoka serikalini, sekta binafsi na watafiti wa nchi zote mbili.
“Hii ni moja ya njia ambazo Poland inaweza kusaidia kuinua uchumi wa Tanzania ambapo ni hatua muhimu ya kuimarisha ushirikiano wetu,” amesema.
Soma zaidi: Wakulima washauriwa kutumia teknolojia ya kisasa kilimo cha umwagiliaji
Tanzania na Poland ambayo inapatikana bara la Ulaya zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu hasa katika sekta za kilimo na maji ambapo nchi hiyo imekuwa ikitoa fedha na wataalam kusaidia katika maeneo hayo.
Uwekezaji huo unaoangaziwa na Poland unaweza kuwa ni matunda ya ziara ya kikazi aliyofanya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Dk Kitila Mkumbo maeneo mbalimbali ya nchi hiyo mwaka jana ikiwemo kutembelea kampuni ya maji safi na taka ya Krakow.
Kwa mujibu wa Mpango Kabambe wa NIC (NICMP-2002) unaeleza kuwa Tanzania ina hekta 29.4 milioni zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji ambazo zinaweza kutoa fursa mbalimbali ikiwemo ajira kwa wananchi.
Hata hivyo, ni asilimia 1.6 ya ardhi hiyo imeendelezwa, jambo linalotoa changamoto kwa wananchi na wawekezaji kuchangamkia fursa hiyo kuwekeza katika matumizi ya teknolojia ya kisasa kuendeleza kilimo cha umwagiliaji nchini ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa ikiwemo ukosefu wa mvua.