October 7, 2024

Balozi Mahiga azungumzia sheria za uwekezaji Tanzania

Amesema mfumo mzuri wa maamuzi na sheria utawahakikishia wawekezaji na wafanyabiashara mazingira mazuri ya kuendesha shughuli zao.

  • Amesema mfumo mzuri wa maamuzi na sheria utawahakikishia wawekezaji na wafanyabiashara mazingira mazuri ya kuendesha shughuli zao. 
  • Amehimiza kuwepo na mtandao mpana wa wasaidizi wa kisheria ili kuongeza wigo wa upatikanaji haki kwenye jamii.

Dar es Salaam. Waziri mpya wa Katiba na Sheria, Balozi Dk Augustine Mahiga amesema katika moja ya mambo atakayoshughulikia katika wizara hiyo ni kutatua changamoto za kisheria na maamuzi ili kuwahakikishia wawekezaji mazingira mazuri ya ufanyaji biashara nchini. 

Kauli hiyo ya Dk Mahiga ameitoa ikiwa ni siku tatu tangu ateuliwe na Rais John Magufuli kuongoza wizara hiyo yenye dhamana ya kusimamia masuala yote ya haki na sheria nchini akichukua nafasi ya Profesa Palamagamba Kabudi ambaye ameteuliwa kuongoza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Dk Mahiga, aliyekuwa akizungumza na wanahabari leo (Machi 6, 2019) Jijini Dar es Salaam baada ya kufungua mkutano wa Mtandao wa Huduma ya Msaada wa Kisheria Ukanda wa Afrika Mashariki (EARLAN), amesema kukiwa na mfumo mzuri wa kisheria kutawawezesha wawekezaji na wafanyabiashara kufanya shughuli zao na kulipa kodi kwa Serikali.

“Ni siku tatu tu tangu niingie ofisini lakini naamini ni kuwa na mfumo mzuri wa kisheria, mfumo mzuri wa maamuzi kwamba wawekezaji wanahakikishiwa mazingira mazuri ya kibiashara…hayo ni moja ya majukumu yangu,” amesema Dk Mahiga.

Balozi Mahiga, ambaye amefanya kazi kwa zaidi ya miaka 30 katika jumuiya za kimataifa, amebainisha kuwa uwepo wa mfumo mzuri wa sheria unasaidia si tu wa wekezaji bali upatikanaji wa haki mbalimbali na kupunguza matatizo katika jamii. 

Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dk Augustine Mahiga akiwa na wanachama wa EARLAN wakati wa kusaini mkataba wa mtandao huo jijini Dar es Salaam leo. Picha| Daniel Samson.

Wakati akizindua mtandao huo, amesema ni muhimu ukapewa msukumo wa aina yake kwa sababu bado watu wengi hawana elimu ya sheria jambo linalowafanya wakose haki zao za msingi na zile za kimataifa. 

“Mkutano huu una maana kwa sababu umewakusanya wataalamu wa sheria wa Afrika Mashariki na Somalia ukizungumzia changamoto za kisheria za makundi mbalimbali ya kijamii na jinsi ya kuwafikia katika maeneo yao,” amesema.


Soma zaidi: Sekta binafsi yazungumzia Kairuki kuteuliwa kusimamia uwekezaji


Mkutano huo unaofanyika kwa siku tatu mpaka Machi 8, 2019, umetoa fursa kwa wataalam wa sheria kutoka nchi za Afrika Mashariki kutia saini ya mkataba wa mtandao ili kuhakikisha kunakuwa na mfumo mzuri wa utawala utakaowezesha mtandao huo kufanya shughuli zake kisheria katika nchi wanachama. 

Nchi zinazounda mtandao huo ni Kenya, Somalia, Rwanda, Sudan Kusini, Burundi, Uganda na mwenyeji Tanzania.

Pia unakusudia kuunda chombo maalum cha kufuatilia mwenendo wa utendaji wa wasaidizi wa sheria katika wanachama kwa kuhimiza mabadiliko ya kisheria na kisera ili kuhakikisha msaada wa kisheria unakuwa sehemu ya upatikanaji wa haki.

“Malengo makubwa ya mtandao huu ni kuhimiza na kulinda haki ya kupata msaada wa kisheria pale unapohitajika kwa watu,” amesema Mwenyekiti wa mtandao, Caroline Amondi ambaye pia Mkurugenzi wa Huduma za msaada wa kisheria nchini Kenya.