November 24, 2024

Sababu zinazofanya upate ugumu kujifunza lugha ya pili kama Kiingereza

Wanasayansi wanasema ugumu wa kusoma lugha ya pili unajitokeza zaidi mtu anapovuka miaka 10.

  • Wanasayansi wanasema ugumu wa kusoma lugha ya pili unajitokeza zaidi mtu anapovuka miaka 10.
  • Wengine wanasema kuzungumza kwa ufasaha lugha ya pili kunategemea njia inayotumika kumfundisha mwanafunzi.
  • Wewe unayetaka kujifunza lugha ya pili unashauriwa kujifunza kwa vitendo zaidi kwa kukaa karibu na jamii ya watu wanaozungumza lugha husika.

Maisha ya mwanadamu wakati wote yametawaliwa na kujifunza mambo mapya. Kujifunza ni pamoja na kwenda shule, kusoma vitabu, kufahamu mazingira yanayomzunguka, matendo na mapito ya watu wengine katika maisha yao ya kila siku. 

Lakini yapo baadhi ya mambo ambayo yatakupa ugumu kuyajua kwa ufasaha kama utaanza kujifunza baada ya kuvuka hatua ya utotoni yaani kuwa mtu mzima.

Baadhi ya tafiti zinaeleza kuwa kujifunza lugha ya pili (second language) siyo rahisi hasa kwa watu wenye umri zaidi ya miaka 10. 

Utafiti uliopewa jina la Kipindi kigumu cha kujifunza lugha ya pili (A critical period for second language acquisition) uliofanywa na watafiti kutoka Chuo cha Saikolojia cha Boston cha nchini Marekani unaeleza kuwa kuna uwezekano mdogo kwa watu wanaojifunza lugha ya pili au mpya kuongea kwa ufasaha kama wazawa wa lugha hiyo ikiwa wataanza kujifunza baada ya umri wa miaka 10. 

Lakini haimaanishi kuwa haiwezekani kabisa kujifunza na kuandika lugha hiyo kwa sababu stadi za lugha zinaeleweka zaidi kwa watoto wenye umri mdogo.

“Ni kwamba unakuwa nyuma ya wakati kwa sababu uwezo wako wa kujifunza unaanza kupungua ukiwa na umri wa miaka 17 au 18,” anaeleza Mtafiti Profesa Joshua Hartshorne, ambaye alishiriki katika utafiti huo. 


Zinazohusiana:


Utafiti huo ulitumia njia maalum kupata matokeo. Walitumia jaribio la dakika 10 la lugha ‘Which English’ ambapo washiriki walitakiwa kukisia lugha zao za asili, lahaja na za nchi za nyumbani kwa kutumia maswali ya misamiati ya Kiingereza. 

Baada ya jaribio, washiriki waliulizwa kuhusu lugha za asili, lini walijifunza lugha zingine mahali pengine au walipokuwa wanaishi. Takribani watu 670,000 walifanya jaribio hilo, jambo lililowapa watafiti data kubwa za wazungumzaji wazawa na wasio wazawa wa umri tofauti wa Kiingereza.

Uchambuzi wa majibu ya washiriki  na makosa yao uliwasaidia watafiti hao kupata hitimisho la  mchakato wa kujifunza lugha katika maisha ya mwanadamu.

Ugumu wa kujifunza lugha ya pili unatoka wapi? 

Profesa Hartshorne anaeleza kuwa bado hajathibitishwa kwanini kujifunza lugha ya pili kunapungua mtu anapokaribia kuwa mtu mzima. 

Anasema maelezo sahihi yanaweza kujumisha mabadiliko ya mnyumbuko wa ubongo, mtindo wa maisha ambao unahusiana na kazi au chuo au hata kutokuwa tayari kujifunza vitu vipya. 

Pia, mtu anapokuwa mtu mzima kwa sehemu huogopa kujiona mjinga au kudharaulika ikiwa watu watajua hajui jambo fulani.  

Baadhi ya wanasayansi wanaamini kuwa dirisha la kujifunza lugha linafunga muda mfupi baada ya mtu kuzaliwa, lakini wengine wanasisitiza kuwa hutokea wakati wa kubarehe. Ukilinganisha na makadirio ya umri wa miaka 17 au 18 ambapo uwezo wa kujifunza lugha mpya huanza kupungua huenda jambo hilo likawa na ukweli japo si kwa asilimia 100.

Kadri siku zinavyoenda Kiswahili kimeendelea kuwa lugha ya kwanza miongoni mwa vijana wengi wa Watanzania huku Kiingereza au lugha za makabila zikiwa lugha ya pili. Kiswahili ni miongoni mwa lugha za asili ya Afrika zinazozungumzwa zaidi. Picha|Africa-facts.org.

Kuna ukweli kiasi gani katika jambo hilo?

Mhadhiri wa Idara ya Lugha za Kigeni na Isimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Faraja Lugome amesema hakubaliani na dhana ya ugumu unaojitokeza wakati wa kujifunza lugha ya pili hasa kwa watu wazima ambapo anasema hali hiyo inatokana na aina ya njia inayotumika kumfundisha mwanafunzi. 

Lugome ameiambia nukta.co.tz kuwa zipo njia mbalimbali za kufundisha lugha ikiwemo njia ya lugha za kigeni (Foreign language teaching approach) ambayo inategemea na mwanafunzi anayefundishwa, umri na mazingira anayoishi. 

“Ukifundisha lugha kwa ‘approach’(njia) tofauti bila kujua mahitaji na umri wa mwanafunzi anayefundishwa hapo lazima ufanisi unapungua na anayejifunza anaona kuna ugumu.”

“Umri ukishaongezeka tunatakiwa kufundishwa lugha kama lugha za kigeni kwa hiyo na njia ya kufundisha lugha za kigeni ni tofauti na kufundisha lugha ya pili.” 

Hata hivyo, kwa watu wanaopenda kujifunza lugha ya pili hapaswi kukata tamaa kwa sababu hakuna lisilowezekana katika kupata maarifa mapya. 


Namna ya kuvishinda vikwazo

Lugome anaeleza kuwa ili lugha ya pili  ieleweke vizuri na kwa haraka, anayejifunza anatakiwa kuishi katika jamii ya watu wengi wanaozungumza lugha husika na kujizoeza kuzungumza lugha husika ili kutambua makosa na kujirekebisha.

“Unapofundisha lugha kama ‘second language’ (lugha ya pili maana yake mzungumzaji katika jamii anayotoka huyo mtu, wazungumzaji ni wengi ukilinganisha kati ya Kiswahili, lugha za asili na Kiingereza; Kiswahili kinafundishika kwa urahisi zaidi kwa sababu wazungumzaji ni wengi,” amesema.

Lakini pia unapaswa kusikiliza radio, televisheni za lugha husika ili kujifunza namna misamiati inavyotamkwa na kujua inatumika katika mazingira gani.

Picha ya mwanzo kwa hisani ya phillys7thward.org.