October 7, 2024

Kiwanda cha kutengeneza transfoma kuongeza gawio serikalini

Ni kile cha Tanelec kilichoko jijini Arusha kimefanikiwa kutoa gawio la Sh500 milioni kwa mwaka 2018 kutokana na faida iliyopatikana baada ya Serikali kuzuia uagizaji wa vifaa vya umeme nje ya nchi.

Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani na wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati, George Simbachawene (Katikati) wakisikiliza maelezo ya utendaji wa kiwanda cha Tanelec kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanelec, Zahir Saleh walipotembelea kiwanda hicho leo jijini Arusha. Picha|Wizara ya Nishati.


  • Ni kile cha Tanelec kilichoko jijini Arusha kimefanikiwa kutoa gawio kwa Serikali la Sh500 milioni kwa mwaka 2018.
  • Kinazalisha transfoma 14,000 kwa mwaka zaidi ya mahitaji ya Tanzania ya transfoma 10,000 baada ya Serikali kuzuia uagizaji wa vifaa vya umeme nje ya nchi. 
  • Waziri Dk Kalemani amesema Serikali ilisitisha kuagiza nje vifaa ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya umeme.
  • Kimepewa changamoto ya kuongeza uzalishaji na kujitanua kimasoko hadi katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Dar es Salaam. Kiwanda cha kuzalisha transfoma cha Tanelec kilichoko jijini Arusha kimefanikiwa kutoa gawio kwa Serikali la Sh500 milioni kwa mwaka 2018 na kinategemea kuongeza kiasi cha gawio hilo kwa miaka inayokuja kulingana na upatikanaji wa faida. 

Mkurugenzi Mkuu wa Tanelec, Zahir Saleh amesema kuwa kiwanda hicho kilichoanzishwa mwaka 1981 kwa sasa kinazalisha transfoma 14,000 zenye  uwezo wa kilovoti 50 hadi 5,000 kwa mwaka.

Pia kinafanya matengenezo ya transfoma kutoka nchi mbalimbali za Afrika kama Rwanda, Burundi na Kenya.

Saleh alikuwa akizungumza leo (Machi 5, 2019) mbele ya Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani na wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati, George Simbachawene walipotembelea kiwanda hicho ili kukagua masuala mbalimbali ikiwemo uwezo wa uzalishaji wa transfoma.

Uamuzi wa Serikali kuzuia kuagiza vifaa vya umeme nje ya nchi umekinufaisha kiwanda hicho kwani kabla ya uamuzi huo walikuwa wakizalisha transfoma 7,000 kwa mwaka lakini sasa uzalishaji umeongezeka mara mbili zaidi, jambo lililosaidia kuongeza faida na ajira kwa vijana. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Nishati, awali waliajiri wafanyakazi 30 lakini kwa sasa wafanyakazi walioajiriwa ni 70 na kwa mwaka huu wataajiri  wafanyakazi wengine 40.


Soma zaidi:


Waziri Dk Kalemani amesema Serikali ilichukua uamuzi wa kusitisha kuagiza nje vifaa vya umeme ili kuvifufua viwanda vya ndani na kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya umeme ambayo ilikuwa inachukua muda mrefu kukamilika kutokana na uhaba wa vifaa.

Amesema kuwa upatikanaji wa transfoma nje ya nchi unaweza kuchukua hadi miezi 12 wakati transfoma zinazozalishwa ndani ya nchi zinachukua muda mfupi kufika katika eneo zinapohitajika.

“Uagizaji wa transfoma nje ya nchi ni gharama kubwa kwani transfoma moja kutoka nje ya nchi inauzwa kwa takriban Sh9 milioni wakati zinazozalishwa nchini ni takribani Sh 6.5 milioni,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Kulinganana taarifa hiyo, mahitaji ya transfoma nchini ni 10,000 kwa mwaka ambapo Tanelec wanazalisha ziada ya transfoma 4,000 ambazo zinatoa fursa ya kuuzwa nchi za jirani ambazo zina mahitaji ya vifaa vya umeme. 

Baadhi ya wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wamemtaka Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda hicho kuongeza uzalishaji na kuwa mbunifu kuangalia pia masoko mengine ya transfoma na si kulenga miradi ya umeme ya ndani ya nchi pekee.