October 7, 2024

Mawaziri wa fedha Afrika wakutana Cameroon kujadili hatua za kukuza uchumi

Mkutano huo umeandaliwa na kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC) na unafanyika kwa siku tano ambapo mawaziri wanajadili sera na matumizi mazuri ya rasilimali za Taifa ili kuondokana na umasikini.

  • Mkutano huo umeandaliwa na kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC) na unafanyika kwa siku tano ambapo mawaziri wanajadili sera na hatua za kuchukua kuinua uchumi wa Afrika.
  • Maadhimio ya mkutano huo yatawasilishwa katika mkutano wa Umoja wa Afrika (AU) utakaofanyika Julai mwaka huu kwa hatua zaidi.

Mawaziri wa fedha wa nchi za Afrika wanakutana katika mkutano wa siku tano katika jiji la Yaounde, Cameroon kujadili utekelezaji wa sera na hatua zinazohitajika kuleta matokeo chanya ya ukuaji wa uchumi katika bara hilo. 

Mkutano huo ulioandaliwa na kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC) kwa kushirikiana na taasisi ya Ujengaji Uwezo ya Afrika (ACBF) unafanyika kuanzia Machi 4-8, 2019 ambapo unalenga kujadili majukumu ya jumuiya za kikanda, sekta binafsi na mabadiliko ya kiungozi yanavyoweza kuchangia katika upatikanaji wa mafanikio ya kiuchumi. 

Mkutano huo umegawanyika katika sehemu mbili; kikao cha wataalam wa sera, uchumi na kile cha mawaziri ambacho kitakuwa jukwaa muhimu la kujadili umuhimu wa sera na uwezo wake katika  kusaidia kulipeleka bara hilo mbele.

“Afrika ina asilimia 30 ya rasilimali zote za dunia, wakati huo huo tunashuhudia umasikini ukikua. Ndiyo maana nchi zote za Afrika zimeamua kuja hapa Cameroon kujadili jinsi ya kwenda mbele na kufanya mabadiliko katika uchumi wetu,” alinukuliwa Waziri wa Fedha wa Cameroon, Louis Motaze mbele ya wanahabari jana wakati akiongoza kikao cha mawaziri.


Soma zaidi: uchumi wazidi kuimarika Tanzania:BoT


Amesema nchini Cameroon wanafikiri mabadiliko ya kiuchumi yanatakiwa yaongozwe na mabadiliko ya matumizi ya rasilimali za Taifa ili kutengeneza ajira nyingi kwa vijana na kupitia mkutano huo anaamini watatoka na maazimio yatakayosaidia uchumi wa Afrika kukua kwa haraka. 

Maadhimio yatakayofikiwa katika mkutano huo yatawasilishwa katika mkutano wa Umoja wa Afrika unaotarajiwa kufanyika Julai, 2019.