Safari ya mwisho ya Ruge Mutahaba duniani akiacha alama lukuki
Ruge Mutahaba amezikwa kijijini kwao mkoani Kagera akiacha kumbukumbu ya miradi na matamasha lukuki yakiwemo Malkia wa Nguvu, Fursa na Fiesta.
Familia ya Ruge ikiweka shada la maua kwenye kaburi la kijana wao.Picha| Mtandao.
- Ruge Mutahaba amezikwa kijijini kwao mkoani Kagera akiacha kumbukumbu ya miradi na matamasha lukuki yakiwemo Malkia wa Nguvu, Fursa na Fiesta.
- Zitto Kabwe amesema Ruge ameonyesha sekta binafsi ikipewa nafasi inaweza.
- Malkia ya nguvu mradi ulioathiri maisha ya wanaweke wengi na kuleta uchachu wa mabadiliko.
Dar es Salaam. Hatimaye safari ya mwisho duniani ya Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group (CMG) Rugemalila Mutahaba imehitimishwa leo baada ya kuzikwa kijijini kwao mkoani Kagera akiacha kumbukumbu ya miradi na matamasha lukuki yakiwemo Malkia wa Nguvu, Fursa na Fiesta.
Majira ya saa 10 jioni jeneza la kigogo huyo liliingizwa kaburini taratibu katika kijiji cha Kiziru wilayani Bukoba na kuwaacha waombolezaji akiwemo mama yake mzazi wakibubujiikwa na machozi na vilio.
Muda wote wakati wa hatua hiyo ya maziko wazazi wa Ruge, aliyefahamika kwa kuwainua wengine kuchangamkia fursa za maisha, walikuwa wakitokwa na machozi.
Hata wakati baba yake marehemu Ruge akienda kuweka mchanga kaburini akisindikizwa na rafiki yake Profesa Rwekaza Mukandala, Mama yake alikuwa akilia muda wote na kushindwa kabisa kwenda kutimiza kitendo ambacho hufanywa kabla ya kaburi kufunikwa.
Mazishi hayo, yaliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo mawaziri, wabunge, wakuu wa mikoa na wilaya, viongozi wa dini, wasanii na mamia ya wakazi wa mjini Bukoba, yamefanyika baada ya utoaji salamu za rambirambi na heshima zao za mwisho kwa mwili wa Ruge katika viwanja vya Gymkhana na kisha kulepekwa kijiji kwao kwa mazishi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia uwekezaji Angellah Kairuki amesema Ruge alikuwa mmoja wa vijana aliyetoa mwanga wa matumaini kwa vitendo kwa kuwaonyesha mengi yanawezekana kwa kufanywa na wananchi na makundi mbalimbali hususan vijana.
“Kwa hakika msimamo wake uthubutu wake, upendo, uthabiti na kujiamni vilikuwa tunu ambazo ndizo zilimwezesha kufanya yote aliyoyaamini,” amesema Kairuki na kuongeza kuwa kila mtu aliyekutana na marehemu ni shuhuda kuwa alisukumwa na ajenda ya maendeleo aliyotamani kila mmoja awe nayo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia uwekezaji Angellah Kairuki akitoa salamu za Serikali katika mazishi ya Ruge Mutahaba leo Bukoba. Picha|Clouds Fm.
Katika salamu za rambirambi kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana chama hicho (UVCCM) Kheri James amesema msiba huo umekuwa ni pigo kwa kuwa alikuwa ni mtumishi wa vijana na Taifa.
“Katibu Mkuu anatukumbusha vijana wote nchini leo ameondoka Ruge mmoja aliyefanya mambo ya faida kwa watu zaidi ya milioni 100 jukumu letu sisi ni kujiuliza vijana gani waliobaki watachukua mikoba ya Ruge na kufanya zaidi ya pale alipoishia,’’ amesema James.
Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT- Wazalendo Zitto Kabwe amesema Ruge ameonyesha sekta binafsi ikipewa nafasi inaweza ikafanya kazi na serikali na asasi zisizo za kiserikali na watu mbalimbali.
‘’Kwa hakika Ruge ameonyesha kwa kiasi gani sekta binafsi inaweza kufanya kwenye jamii na viongozi wa Serikali waliopo hapo wanapaswa kujifunza kutoka kwa marehemu,” amesema Zitto na kueleza kuwa aliyoyafanya kwa vijana nchini yanapaswa kuendelezwa bila kujali itikadi.
Zinazohusiana :
Mambo ya kukumbwa kwa Rugemalila Mutahaba
Ruge, ambaye sasa ambaye amepewa jina la “Jasiri muongoza njia” aliasisi matamasha na miradi mbalimbali nchini iliyoleta tija na fikra mpya kwa watu wengi hususan vijana wa leo.
Miongoni mwa miradi au matamasha hayo ni kongamano la kibiashara la kuchangamkia fursa zilizopo katika jamii la Fursa ambalo hufanyika kila mwaka sambamba na tamasha la burudani la Fiesta ambalo hutoa nafasi kwa wasanii chipukizi na manguli katika kufanya shoo nchi nzima.
Mkurugenzi Mtendaji wa Clouds Media Group (CMG) Joseph Kusaga, wakati wa kumwaga Ruge katika viwanja vya Kharimjee jijini hapa, alieleza kuwa Ruge ndiye mwasisi wa Fiesta, moja ya matamasha maarufu ya burudani yaliyodumu nchini kwa muda mrefu.
“Ruge tunayasheherekea maisha yake hapa ametumia miongo miwili iliyopita kuhakikisha tasnia inaendelea katika mwelekeo unaoendana na nyakati akiongoza uzalishaji wa vipindi vya radio, TV na burudani, kuanzisha na kuongoza matukio makubwa ya kiburudani kuyataja machache tu ukiingalia Fiesta ambayo ipo miaka 17,” alisema na kuongeza;-
“Fiesta imekuwa tamasha kubwa zaidi la muziki Afrika Mashariki na Kati likitoa nafasi ya kukuza na kuonyesha vipaji na ajira kwa vijana. Unataja vipi Fiesta bila kumtaja Ruge. Ruge ndiye aliyekuwa kinara kabisa wa Fiesta.”
Mwakilishi wa washindi wa Malkia wa Nguvu ambaye alitoa salamu za rambimrambi Dk Elizabeth Kilili amesema Tanzania imepata pigo kubwa kwa kuwa Ruge alikuwa sura ya Ujasiliamali na mfano kwa vijana wengi na kuwasaidia vijana wanafanikiwa.
“Leo nimesimama.. kama msemaji wa Malkia ya nguvu mradi ulioathiri maisha ya wanaweke wengi na kuleta uchachu wa mabadiliko katika jamii ya watanzania tunzo za Malikia wanguvu zilikuwa ni uvumbuzi wake Ruge mtuhaba toka mwaka 2016 ilipo zinduliwa,” amesema Dk Kilili.
Malkia wa Nguvu imetoa fursa kwa kuwahamasisha wanawake na kujulikana kwa kazi zao ndani nje ya nchi na kuheshimika kupitia michango yao katika Taifa kwa kada za iana zote za wajasiriamali, wanasayansi, wakulima, walemavu na elimu.
Mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group (CMG) Rugemalila Mutahaba ukiwekwa kaburini. Picha|Mtandao