Rais Magufuli awashangaa wanaohoji uzoefu wa mawaziri wapya aliowateua
Mawaziri hao ni Profesa Palamagamba Kabudi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Balozi Augustine Mahiga wa Katiba na Sheria ambao wamebadilishana wizara jana Machi 3, 2019.
- Mawaziri hao ni Profesa Palamagamba Kabudi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Balozi Augustine Mahiga wa Katiba na Sheria ambao wamebadilishana wizara jana Machi 3, 2019.
- Amesema amefanya uteuzi huo ili kuboresha utendaji kazi na kuhakikisha mpango ya Serikali inaenda mbele.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri aliyofanya jana ni ya kawaida na yanalenga kuboresha utendaji kazi wa Serikali huku akiwashangaa baadhi ya watu wanaohoji uzoefu wa mawaziri wapya aliowateua.
Mawaziri walioteuliwa ni Profesa Palamagamba Kabudi ambaye ataiongoza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Balozi Dk Augustine Maiga aliyehamishiwa katika Wizara ya Katiba na Sheria.
Baada ya uteuzi huo uliofanyika Machi 3, 2019, baadhi ya watu kupitia mitandao ya kijamii walihoji uzoefu na taaluma walizonazo mawaziri hao ukilinganisha na unyeti wa majukumu waliyokabidhiwa.
Rais Magufuli aliyekuwa akizungumza leo (Machi 4, 2019) wakati akiwaapisha makamishna wa Jeshi la Polisi na mawaziri hao, amesema mabadiliko aliyoyafanya ni ya kawaida kwasababu ni yeye anayejua ni wakati gani amuweke mtu fulani katika nafasi fulani.
Amesema lengo kubwa la mabadiliko hayo ni kuboresha utendaji wa kazi wa Serikali ili kuhakikisha mipango ya Serikali inaenda mbele.
Hata hivyo, Rais Magufuli amewashangaa wale wanahoji uzoefu wa mawaziri hao huku akisema wapo mawaziri wengi kwenye wizara lakini hawana na uzoefu wa taaluma zinahitajika katika wizara husika.
Akizungumzia Dk Mahiga kukabidhiwa Wizara ya Katiba na Sheria amehoji, “nilikuwa naangalia magazeti wengine wanasema huyu siyo mwanasheria kwani unaenda kufundisha sheria pale?.”
Soma zaidi: Rais Magufuli amteua Kabudi wizara ya mambo ya nje
Amesema wizara hiyo ina watendaji wengi wenye taaluma ya sheria ikiwemo Jaji Mkuu wa Tanzania, Katibu na Naibu Katibu Mkuu, ambapo kupelekwa kwa Dk Mahiga ambaye ni Mwanadiplomasia kutasaidia kuboresha utendaji wa kazi.
“Kwa hiyo ni logic (mantiki) ya kawaida ambayo nimefikiria, experience (uzoefu) yetu ya mzee Mahiga ukilinganisha na utaalamu wa wanasheria walioko pale mambo yataenda vizuri nina imani kubwa kwasababu ni mchapakazi, muadilifu ana matarajio makubwa,” amesema Rais.
Katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, amesema ameteua Prof Kabudi ili akaongeze nguvu kwasababu ni muwazi na atatoa mchango mkubwa katika diplomasia ya kimataifa.
“Kwenye wizara ya mambo ya nje nafikiri inahitaji watu kama Kabudi kusukuma sukuma kidogo na ndiyo maana niliamua kumpeleka pale ni mtaalamu wa sheria ili diplomasia iliyopo pale ikaungane na sheria, nafikiri mambo yanaweza yakaenda vizuri,” amesema.
Amewataka mawaziri hao kuendelea kufundishana kazi katika wizara zao ili kuhakikisha mipango ya serikali inaenda mbele.
Mawaziri wote wawili ni Wabunge wa kuteuliwa na Rais ambapo wamedumu katika wizara zao za awali kwa miaka miatu na miezi miwili kabla ya kubadilishana wizara jana.
Profesa Palamagamba Kabudi ambaye ataiongoza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akiapa leo (Machi 4,2019) mbele ya rais John Magufuli. Picha|Mtandao.
Akizungumzia majukumu aliyokabidhiwa, Balozi Dk Mahiga amesema ametumia zaidi ya miaka 30 kufanya kazi katika jumuiya za kimataifa ambapo heshima aliyopewa kuongoza Wizara ya Katiba na Sheria itampa fursa ya kutulia nyumbani kujifunza zaidi kuhusu nchi na katiba ambayo ndiyo kitovu cha amani na utulivu.
Amesema wizara aliyokuwa akiiongoza imejitahidi kutangaza sera na siasa za nchi hasa za kujenga uchumi wa viwanda ifikapo 2025 licha ya changamoto kadhaa za vitendea kazi na mbadiliko ya wafanyakazi ambazo anaamini Prof Kabudi atazishughulikia.
Naye Prof Kabudi amesema kazi ya kwanza aliyonayo katika wizara mpya ni kufanya mabadiliko na mabadiliko hayo yanaanza na watu waliopo kwenye wizara kubadilika ili kuhakikisha diplomasia ya Tanzania kimataifa inaeleweka vizuri.
Amebainisha kuwa Dk Mahiga ameweka msingi mzuri na yeye akishirikiana na watendaji wa wizara hiyo watahakikisha jina la Tanzania halichafuliwi na watu wenye nia mbaya.
Hafla hiyo ya kuwaapisha makamishna na mawaziri ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, dini na taasisi za umaa ikiwemo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge, Job Ndugai na Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma.