October 6, 2024

Soya ya Tanzania inaweza kunufaika na vita ya kibiashara kati ya Marekani na China?

Vita hiyo imeathiri usafirishaji wa mazao ya biashara ikiwemo soya inayotumika kutengeneza bidhaa za mafuta na ilidhaniwa kuwa nchi kama Tanzania ingefaidika na vita hiyo lakini huenda ikawa tofauti.

  • Imedumu kwa muda wa miezi saba sasa baada ya nchi hizo kuwekeana vikwazo vya ushuru na  usafirishaji wa bidhaa katika nchi zao pande zote zikitafuta namna ya kuimaliza.
  • Tanzania imeshindwa kunufaika kutokana na uzalishaji mdogo wa soya inayohitajika zaidi China.
  • Waziri Hasunga aahidi kuongeza bajeti ya utafiti na uzalishaji wa mazao ikiwemo soya.

Dar es Salaam. Kumekuwa na mjadala juu ya vita ya kibiashara inayoendelea baina ya Marekani na China na jinsi nchi za Afrika ikiwemo Tanzania zinavyoweza kufaidika baada ya China kusitisha uagizaji wa bidhaa za kilimo ikiwemo soya ikiwa ni hatua ya kujibu mapigo.  

Vita hiyo ambayo imedumu miezi saba sasa, ilianza mapema mwaka jana baada ya Rais Donald Trump kutangaza viwango vya ushuru wa ziada kwa bidhaa  za elektroniki, teknolojia ya juu na vifaa vya kompyuta vya kuhifadhia data zinazoingia kutoka China.

Baada ya China kusitisha uagizaji wa soya toka Marekani, ilidhaniwa kuwa mataifa ya Afrika yangefaidika na fursa ya kuizuia nchi hiyo soya ambayo ni mtengenezaji  mkubwa wa mafuta ya mbegu duniani.

Baadhi ya wataalamu wa uchumi wamesema Afrika bado haina nguvu ya kusafirisha soya nje ya bara hilo kwa sababu  inakabiliwa na matatizo ya mabadiliko ya hali ya hewa na usalama mdogo wa chakula.

Utafiti wa ushindani wa kilimobiashara katika nchi za Afrika wa mwaka 2017 uliotolewa na Shirika la Chakula Duniani (FAO), umeeleza kuwa soya inayozalishwa Afrika ni asilimia tano tu ya soya yote inayopatikana duniani.

“Ulimaji wa maharage ya soya umejikita zaidi kwenye nchi nne; Marekani, Brazil, Argentina na China na zinazalisha asilimia 90 ya soya yote duniani. Asia ukiondoa China, na  Afrika zinachangia asilimia tano ya uzalishaji wote,” inaeleza sehemu ya utafiti huo.

Katika hali hiyo, Marekani ina nafasi kubwa ya kutumia soko ililopoteza China na kuzigeukia nchi za Afrika ili kujiweka katika nafasi nzuri kibiashara.


Soma zaidi: 


Uzalishaji wa soya  unashika nafasi ya pili kwa mazao nchini Marekani na soko lake linategemea zaidi nchi za bara la Asia na Mashariki ya Mbali ambazo ndiyo waagizaji wakubwa duniani. 

Kulingana na takwimu za Idara ya Kilimo ya Marekani za Aprili 19, 2018, China ilizuia manunuzi ya tani 62,690 za soya  kutoka Marekani ambazo zingesafirishwa Agosti, 2018.

Katika kipindi hicho cha Agosti, nchi za Amerika ya Kusini zilikuwa zinakamilisha mavuno ya soya na kufaidika na soko kubwa la kusafirisha zao hilo nchini China.

Soya ikiwekewa mikakati mizuri inaweza kuwa sehemu ya utengenezaji wa bidhaa mbalimbali ikiwemo mafuta ya kula. Picha| Mtandao.

Hali ya uzalishaji Soya Tanzania

Kitabu cha Uchumi wa Taifa cha mwaka 2017, kimebainisha kuwa soya inazalishwa kwa kiwango kidogo nchini ukilinganisha na mazao ya mbegu za mafuta ya alizeti, karanga, ufuta na mawese.

Mathalani, mwaka 2017 wakulima walizalisha tani 6,135 sawa na asilimia 0.09 kati ya tani 6.6 milioni za mazao yote ya mafuta katika kipindi hicho.

Soya hulimwa katika mikoa mbalimbali ikiwemo Kagera, Ruvuma, Mbeya, Rukwa na Arusha ambapo kwa mujibu wa kijitabu cha kilimo cha Soya kilichotolewa na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), soya iliingia Tanzania mwaka 1907 na ilianza kulimwa kibiashara kuanzia 1939 hadi 1947 huko Bukoba mkoa wa Kagera. 

Hata hivyo, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga amesema Serikali inaangalia uwezekano wa kuongeza bajeti ya utafiti wa mazao ya kilimo ili kuongeza uzalishaji, usambazaji katika masoko ya ndani na nje ya nchi na kuchochea ukuaji wa viwanda. 

Hasunga amesema tafiti hizo zinaenda sambamba na miradi ya kuzalisha mbegu bora kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo, ambapo jana (Februari 25, 2019) amezindua mradi wa miaka minne wa ‘AVISA’ unaosimamiwa na taasisi ya kimataifa ya kilimo (IITA) unaolenga kuinua uzalishaji wa maharage ya soya, kunde, karanga na nafaka kama uwele, ngano na ulezi katika nchi za Afrika. 

Huenda juhudi hizo zikasaidia kuongeza uzalishaji wa soya na kuifanya Tanzania kuwa msafirishaji mkubwa wa bidhaa za soya duniani kama ilivyo kwa China na Marekani.