Ole wenu vijana mnaowapa mimba wanafunzi wa kike-Majaliwa
Amewataka watafakari kabla ya kutenda kwa sababu wakibainika wamewapa mimba mabinti wanaosoma, adhabu yake ni miaka 30 jela.
- Amewataka watafakari kabla ya kutenda kwa sababu wakibainika wamewapa mimba mabinti wanaosoma, adhabu yake ni miaka 30 jela.
- Wazazi na walezi waowaozesha wanafunzi wa kike nao watahadharishwa.
- Amesema watoto wa kike wanatakiwa kuheshimiwa katika jamii ili watimize malengo yao kielimu.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza viongozi na wazazi wilayani Siha mkoani Kilimanjaro washirikiane kuhakikisha watu wote waliowapa mimba wanafunzi wanasakwa na kufikishwa kwenye vyombo vya dola.
Amesema katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba 2018, jumla ya wanafunzi wa kike 57 katika wilaya hiyo walikatisha masomo baada ya kupata mimba na hadi sasa kesi zilizofunguliwa ni sita tu.
Majaliwa aliyekuwa akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Isanja, Sanya Juu wilayani Siha jana (Februari 24, 2019) amesema Serikali imeweka sheria kali ya kumlinda mtoto wa kike lengo ni kumuwezesha amalize masomo yake ili aweze kujikwamua kiuchumi na aondokane na utegemezi, hivyo ni marufuku kuwakatisha masomo.
“Jambo hili halipendezi, kesi sita tu ndio zimefikishwa mahakamani. Hakikisheni wahusika wote waliowapa mimba wanafunzi wanatafutwa popote walipo, wakamatwe na wachukuliwe hatua kali za kisheria,” amesema Majaliwa.
Katika taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu inaeleza kuwa watoto wa kike wanatakiwa kuheshimiwa katika jamii na Serikali itatoa adhabu kali ya kifungo cha miaka 30 jela kwa mtu atakayekatisha elimu ya mtoto wa kike iwe kwa kumuoa, kumpa ujauzito na hata ukikutwa naye nyumbani kwako au nyumba ya wageni.
“Tukikukuta na binti wa shule katika kona isiyoeleweka tunakukamata na kukuchukulia hatua za kisheria. Ole wenu vijana, mkibainika mmewapa mimba mabinti wanaosoma, adhabu yake ni miaka 30 jela, sasa tafakari kabla ya kutenda,” amesema Majaliwa.
Kwa mujibu wa Sheria ya Elimu sura 353 marejeo ya mwaka 2002 inatoa adhabu ya kifungo kisichopungua miaka 30 kwa mtu yeyote atakayempa mimba mwanafunzi wa shule ya msingi na sekondari.
Zinazohusiana:
- SIKU YA MTOTO WA KIKE DUNIANI: Wasichana waache kulialia, kujificha katika mwamvuli wa uanamke
- Safari bado ndefu kufikia 50 kwa 50 elimu ya juu Tanzania
Hatua hizo za kisheria hazitawaacha salama pia wazazi na walezi watakaowaozesha watoto wa kike ambao bado ni wanafunzi na kwa upande wa wazazi watakaomsindikiza mtoto kwenda kuoa mwanafunzi ambapo wote watachukuliwa hatua za kisheria.
“Kuna taarifa nimezipata kuwa baada ya watoto kupewa mimba wazazi au walezi mnamalizana na wahusika kwa kupeana ng’ombe. Sasa tukikukamata unamalizana na mtu aliyempa mimba mwanafunzi na wewe tunakufunga,” amesema Majaliwa.
Majaliwa aliyekuwa akihitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Kilimanjaro, alitumia fursa hiyo kuwataka wanafunzi wote hususani wa kike wasome kwa bidii ili watimize ndoto zao na wasikubali kushawishika kwa sababu watashindwa kuendelea na masomo yao.
Nayo Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, inaeleza kuwa wazazi na walezi wana wajibu mkubwa wakuhakikisha kwamba watoto wanapelekwa kwenye chanjo, wanapatiwa huduma za afya, wanaandikishwa na kwenda shule, wanafuatiliwa maendeleo yao shuleni, wanasikilizwa na kupewa miongozo na matunzo.
Mimba kwa wanafunzi wa kike pia huhatarisha afya zao ikiwemo kuvuja damu nyingi na kifo. Picha| Mtandao.
Wakati Serikali ikipambana na watu wanaowapa mimba wanafunzi wa kike, bado imewaweka kando wasichana ambao tayari wamepata mimba kwa sababu hawaruhusiwi kurudi shuleni baada ya kujifungua watoto.
Juni 22, 2017 akiwa ziarani mkoa wa Pwani, Rais John Magufuli alitoa agizo la kutokuwaruhusu wanafunzi wa kike waliopata mimba kurudi shuleni akidai kuwa hawezi kusomesha watu ambao wameamua kuwa wazazi kabla ya muda wao.
Agizo la Rais liliibua mjadala mpana wa kitaifa ikizingatiwa kuwa wakati huo mashirika ya kijamii likiwemo la HakiElimu yalikuwa yanaitaka Serikali kuharakisha kupitia na kupitisha miongozo ya watoto wa kike waliojifungua warejee shuleni na kuendelea na masomo.