October 6, 2024

Unayotakiwa kuyafanya kabla hujavuka miaka 30

Jenga nidhamu ya matumizi mazuri ya fedha, mawasiliano, fanya unachokipenda na ikiwezekana tembelea maeneo mbalimbali ili kupanua uelewa wako wa maisha.

  • Wewe bado ni kijana mwenye ushawishi na una muda mwingi wa kufanikiwa zaidi hata pale unaposhindwa unaweza kuanza tena na kufanikiwa maana huna cha kupoteza.
  • Jenga nidhamu ya matumizi mazuri ya fedha, mawasiliano, fanya unachokipenda na ikiwezekana tembelea maeneo mbalimbali ili kupanua uelewa wako wa maisha.

Kufikisha miaka 30 ni kipindi cha mabadiliko makubwa kwenye maisha ya mtu na taaluma yake. Ni kipindi ambacho malengo ya wengi kitaaluma na familia huanza kuwa wazi na shauku ya kufika sehemu fulani kimaendeleo huongezeka zaidi. 

Vijana wengi hasa wa kiume huwaza kutoka nyumbani na kuanza maisha yao binafsi ili kujiandaa kujenga familia.  Kwa lugha nyingine ni muda wa kuachana na mambo ya kitoto na kuingia katika majukumu ya mtu mzima.

Katika mazingira kama hayo unatakiwa kufanya nini ili kufanikisha safari yako ya mafanikio? 

Jifunze kutoka kwa wenzako

Kadri unavyozidi kukua katika taaluma yako kabla hajafika miaka 30 unatakiwa  kujifunza siyo tu kwa wale waliokuzidi, bali hata kutoka kwa wale tulionao kwenye ngazi moja. 

Hii itakuhakikishia ujenzi wa msingi wa maisha kwa sababu utapata mbinu nyingi za kuzikabili changamoto zinazoweza kuibuka wakati ukitekeleza mipango yako. Wao watakufunza uzoefu walionao katika maisha ambao unaweza kuwa msaada kwako. 

Uzoefu pia unaweza kuupata toka kwa makampuni au watu waliofanikiwa kimaisha kama wafanyabiashara wakubwa. Jitahidi kufanya kazi sehemu mbalimbali ikiwemo viwandani au kwenye shule hata kama ni kazi za muda mfupi au za masaa machache.

“Ishi maisha kwa kiwango kikubwa kwa kadiri unavyoweza na pokea kila uzoefu unaoupata pale unapokuja,” anasema Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya  atmail.com, Zach Johnson katika moja ya nukuu zake. 

Marafiki na watu wenye mawazo yanayolingana na mipango watakusaidia kufanikisha ndoto zako. Picha|K15 Photos.

Nidhamu katika matumizi ya pesa

Kuwa na nidhamu katika matumizi yako ya fedha, weka bajeti na hakikisha unaifuata. Acha kutumia pesa bila mipango.

Weka akiba ya kila pesa unayoipata. Jifunze kuweka akiba na utoke nyumbani kwenda kujitegemea mwenyewe. Hakikisha unalipa madeni yote unayodaiwa mapema mara upatapo pesa ili kuzuia yasikuandame kiasi cha kushindwa kulipika na achana na hisia kuwa kuna watu unawajibika kwao. 

Fanya biashara na uwekezaji wa miradi

Kama hutaki kuajiriwa lakini unataka kufanya biashara, jitahidi uanze kuifanya kabla hujaoa au kuolewa. Utakuwa muoga sana na hutakuwa na uthubutu wa kutosha pale tu utakapoanza kuwa na familia na maendeleo ni ya muhimu kuanzia mwanzo wa taaluma yako.

Mwanzilishi na Afisa Mtendaji Mkuu wa wa kampuni ya  Inspiring Rare Birds ya nchini Australia, Jo Burston alipoulizwa ni kitu gani kijana afanye kabla hajafika miaka 30 alisema jitahidi uanzishe biashara hata kama ni ndogo kwa sababu utakapoweza kujifunza mbinu hizi mapema utajifunza namna ya kupata hasara kwa gharama ndogo. 

Kumbuka msingi mzuri wa ujuzi wa biashara na fedha utakusaidia kufanikiwa baadaye. 


Soma zaidi: bajeti inavyookoa matumizi mabaya ya pesa ngazi ya familia


Jenga tabia njema na maadili mazuri

Tabia inajengwa kuanzia kwenye matumizi mazuri ya muda, maadili ya kazi, kujiwekea mipaka ya kazi au maisha, mazoezi, kula vizuri au kuwa na nidhamu na fedha zako binafsi. Maadili ndiyo msingi wako mkuu wa kufanikisha maisha.

Pale unapokutana na mazingira yasiyotabirika kwenye maisha, maadili mazuri uliyojijengea kwa muda mrefu ndiyo yatakayokusaidia. Anza mapema nayo yatakuwa pamoja na wewe katika vipindi vyote vya maisha yako. Jifunze kukabiliana na kupanda na kushuka kimaisha. Maisha ndiyo haya haya wasikilize wakubwa wako katika kujijenga vyema kimaadili. 

Tunza mawasiliano

Jitahidi kutunza mawasiliano ya watu muhimu unaokutana nao katika shughuli mbalimbali za kikazi au biashara. Fanya vyovyote inavyowezekana ili kutunza mawasiliano yako siku zote. Mawasiliano ni muhimu maana hujui ni wakati gani utahitaji msaada kutoka kwa mtu fulani.

Mawasiliano yanaimarisha urafiki na undugu. Tafuta marafiki wenye tija kwako na hakikisha unawasiliana nao mara kwa mara ili kutengeneza mtandao mzuri wa maendeleo. 

Lakini mawasiliano ni pamoja na ujuzi wa mazungumzo na kuzungumza mbele za watu kwa kujiamini na ujasiri na kabla ya kuzungumza fikiria kwanza na fahamu kwa undani unachokisema.

Wekeza nguvu yako kujenga mawasiliano imara na endelevu na watu wa karibu yako ambao watakusaidia kufanikiwa zaidi. Picha|K15 Photos.

Fanya unachokipenda

Kila kijana ana kusudi lake la kuishi duniani. Tambua kile unachokipenda na lenga kuwa bora duniani katika kile unachokifanya kwa kupenda kujifunza zaidi kwa nadharia na vitendo.

Tafuta mwalimu au mtu ambaye amewahi kupita kwenye njia unayotamani kupita. Kuwa mbunifu, mwaminifu na heshimu muda unaoutumia pamoja naye kwasababu anajifunza kutoka kwako pia. 

Kadri umri unavyoongezeka ndivyo sababu za kutokufanya jambo fulani huongezeka na mwisho wa siku utakuja kujuta kwa kutokujaribu mapema. 

Tembelea maeneo mbalimbali

Hakuna kitu kizuri kinachofungua macho kama kusafiri kwenda sehemu mbalimbali ili kupanua uelewa wako na kuboresha mbinu zako za mawasiliano kutoka kwa watu wengine wa tamaduni tofauti. Hii inawezekana hata kama mfuko wako bado ni mdogo. Unachokipata hicho kitumie kufika hata maeneo ya karibu ujifunze mapya. 

Uzoefu wa kidunia hauna gharama. Inakusaidia kufahamu mambo chanya kwenye ulimwengu halisi wa watu. Kuna watu wapo Dar es Salaam miaka 10 sasa hawajawahi kufika hata Bagamoyo au Mkuranga ambako kuna maisha tofauti na anapoishi kwa sasa.

 Hata hivyo, wewe bado ni kijana mwenye nguvu nyingi, mwenye ushawishi na una muda mwingi wa kufanikiwa zaidi hata pale unaposhindwa unaweza kuanza tena na kufanikiwa maana huna cha kupoteza.