November 24, 2024

Maajabu manne barabara ya Sokoine Dar

Kandokando mwa barabara hiyo kunapatikana majengo manne yaliyoishi zaidi ya miaka 100 ambayo yamekuwa kivutio kwa watalii wengi wanaotembelea jiji hilo.

  • Kandokando mwa barabara hiyo kunapatikana majengo manne yaliyoishi zaidi ya miaka 100.
  • Kati ya majengo hayo, mawili ni miongoni mwa maghorofa ya kwanza kujengwa katika jiji hilo likiwemo la ‘Old Boma’.
  • Bodi ya Utalii yashauriwa kuwekeza nguvu katika kuhamasisha utalii wa malekale ili kuongeza mapato yatokanayo na utalii.

Dar es Salaam. Kwa wananchi wanaoishi katika Jiji la Dar es Salaam basi barabara ya Sokoine itakuwa sio jambo geni kwao kwa sababu imekuwa kiungo muhimu kwa wasafiri wanaofanya shughuli zao katikati ya jiji. 

Barabara hiyo, inayounganishwa na barabara kama Morogoro, KIvukoni na mitaa ya Gerezani na Bandari, imeficha siri nyingi za kihistoria katika jiji hilo linalokua kwa kasi kwa sasa kimiundombinu likiwa na wakazi zaidi ya milioni tano. 

Ukuaji huo wa kasi umefanya jiji hilo kuwa na jengo lefu zaidi Afrika Mashariki na Kati la ‘PSPF Twin Towers’ lenye urefu wa mita 147 sawa na ghorofa maarufu la 88 on field liliopo jijini Durban, Afrika Kusini.

Licha ya fahari hiyo, barabara ya Sokoine ambayo iko pendezoni mwa bahari ya Hindi nayo haitasahaulika katika historia kutokana na kuwa na majengo ya mwanzo kabisa kujengwa Dar es Salaam ambayo yameishi zaidi ya miaka 100.

Nukta inakuletea orodha ya majengo manne miongoni mwa majengo yaliyoishi zaidi ya miaka 100 jijini hapa ambapo yanaendelea kutumika hadi sasa kwa shughuli mbalimbali za kijamii na kiserikali. 

Ghorofa la Old Boma

‘Old Boma’ ni ghorofa la kwanza kujengwa jijini Dar es Salaam ambapo lilijengwa mwaka 1860 kwa ajili ya wageni wa Sultani Majid bin Said wa  Zanzibar karibu na Ikulu yake ambayo ilishapotea kwenye ramani baada ya kubomolewa. Wakati huo Dar es Salaam ilikuwa ikifahamika kama Mzizima. 

Ghorofa hilo lenye muonekano wa zamani lipo kando kando ya makutano ya barabara ya Sokoine na barabara ya Morogoro karibu na Chuo Cha Mabaharia Tanzania (DMI).

Msimamizi wa  Kituo cha Urithi wa Ubunifu wa Majengo jijini Dar es Salaam (DARCH) kilichopo chini ya Hamalshauri ya Jiji la Dar es salaam Gwamaka Mwakalinga ameiambia Nukta kuwa Wajerumani walipokuja baada ya mgawanyo wa Bara la Afrika mwaka 1886 na baada ya kukutana na ‘resistance’ (upinzani) kubwa kutoka kwa Waarabu wakati wa vita ndipo walipoamua kujenga ukuta wa kuzunguka jengo hilo na kulipa jina la Old Boma lilipoanza.

Ghorofa hilo linatumika kama ofisi za DARCH na kuvutio cha watalii wanaokuja kutembelea jiji hilo.

Jengo la Atiman House

Jengo lingine lenye miaka zaidi ya 100 katika barabara hiyo ya Sokoine ni Atiman House ambalo nalo limeficha historia muhimu kwa taifa hili. Jengo hilo lenye ghorofa moja liko mita 300 tu kutoka lilipo ghorofa la kwanza kujengwa katika jiji hilo la  ‘Old Boma’.

Atiman House ni miongoni mwa majengo matano yaliyojengwa na Sultani Majid bin Said kabla ya kifo chake mwaka 1870.

Ghorofa hilo la rangi nyeupe na madirisha membamba likisadifu mtindo wa kizamani, kwa sasa lipo mkabala na kituo cha mabasi ya yaendayo haraka (DART) cha Posta ya Zamani.

Linamilikiwa na shirika la Wamisionari wa Afrika ambapo linatumika kama makao makuu ya shirika hilo Tanzania. 

Atimani House linalomilikiwa na Shirika la Wamisionari wa Afrika  lilijengwa mwaka 1866 ikiwa ni miaka sita tu tangu lilipojengwa ghorofa la kwanza jijini hapa la Old Boma liko karibu na kituo cha mabasi ya yaendayo haraka (DART) cha Posta ya Zamani. Picha| Mtandao.

Kanisa la Kilutheri la Azania Front

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) la Azania Front nalo ni miongoni mwa majengo yaliyopo katika barabara ya Sokoine ambapo lilijengwa mwaka 1898 na Wamisionari wa Kijerumani.

Kanisa hilo ni moja ya vivutio vikubwa vya  utalii kwa watu wanaotembelea Jiji la Dar es Salaam kwa mara ya kwanza likiwa na miaka 121 mpaka sasa. 

Azania Front ambalo pia hutumika kwa ibada linatazamana na bahari ya Hindi upande wa kushoto ambao hutumika kuingilia linapakana na hoteli maarufu ya New Afrika.

Paa la jengo hilo limepambwa kwa vigae vya rangi nyekundu na kuta zake ni nyeupe.

Monekano wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) la Azania Front lililopo pembezoni mwa barabara ya Sokoine Jijini Dar es Salaam. Picha|Mtandao.

Kanisa Katoliki  la Mtakatifu Joseph

Hili ni kanisa Katoriki lililojengwa na Wamisionari wa Kijerumani kuanzia 1897 hadi mwaka 1902.

Jengo hilo ambalo hadi sasa lipo ingawa limefanyiwa ukarabati wa mara kwa mara toka lilipoanza kujengwa. Mwaka 1898 mwezi Mei ndipo jiwe la msingi lilipowekwa.

Kanisa hilo hadi sasa linatumika na waumini wa kanisa katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salam  lina umri wa miaka 122. Kama ilivyo kwa Azania Front, kanisa hilo linatazamana na bandari ya Dar es Salaam upande wa mbele huku likiwa limezungukwa na maghorofa marefu ya jiji.

Kanisa Katoliki  la Mtakatifu Joseph lililopo pembezoni mwa barabara ya Sokoine jijini Dar es Salaam. Picha|Mtandao.

Wadau wa malikale wanaeleza kuwa majengo hayo ni alama muhimu katika historia ya Tanzania hivyo yanatakiwa kutunzwa vyema kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Urithi wa Ubunifu wa Majengo jijini Dar es Salaam (DARCH)  Aida Mulokozi ameiambia Nukta kuwa wanafanya jitihada kubwa katika kuhakikisha majengo hayo yanabaki salama kwa kuwa yana historia kubwa.

”Tushirikiana na Serikali na tunawaeleza umuhimu wa kihistoria wa majengo hayo ili yasibomolewe  kwa sasabu kwa kiasi kikubwa Serikali ndiyo wamiliki na pia huwa tunawaeleza ni  jinsi gani majengo hayo yakatavyoweza kuleta faida katika sekta ya utalii.

”Pia tunatoa elimu  kwa umma juu ya umuhimu wa majengo hayo ya zamani kwa wananchi kupitia maonyesho na matembezi ya miguu katika jiji la Dar es Salaam ili mtu ajionee mwenyewe hayo majengo na kuyashika kwa mkono,” amesema Mulokozi.

DARCH wanatekeleza mradi wa utunzaji wa majengo ya zamani Dar es Salaam wakishirikiana na Chama cha Wasanifu majengo Tanzania (Architects Association of Tanzania) , Geothe Institut ,Chuo Kikuu cha Ardhi na chuo Kikuu kutoka ujeruma (Technical Univesrtty )  pamoja na Serikali.

Mulokozi, ambaye anasema ushirikiano huo umefanya watumie jengo kama la Old Boma kama njia za kukuzua aina hii ya utalii 

“Utalii wa asilii kama wa mbuga za wanyama na milima unajulikana kwa kiasia fulani na fikiria pia serikali kupitia taasisi zake sasa zinge weka  mkazo utalii huu wa majengo ambao bado haujuilikani sana maana ni watu wachache sana wanao jua historia nzuri ya mji kama wa Dar es Salaam,” amesema kigogo huyo wa Darch akiishauri Bodi ya Utalii ya Tanzania (TTB) kuanza kufikiria kuweka jitihada katika aina hii ya utalii.