Fursa zilizojificha uzalishaji wa michikichi Tanzania
Michikichi inafungua mlango kwa wakulima kupata kipato na uzalishaji wa mafuta ya mawese na kupunguza tatizo la uagizaji mafuta ya kula nje ya nchi.
- Michikichi inafungua mlango kwa wakulima kupata kipato na uzalishaji wa mafuta ya mawese na kupunguza tatizo la uagizaji mafuta ya kula nje ya nchi.
- Wakulima watapata tija ya kutengeneza ajira na kuboresha maisha ya familia zao.
- Ni njia nyingine ya kuendeleza sekta ya viwanda vidogo vidogo na wajasiriamali.
Dar es Salaam. Licha ya zao la michikichi kuwa fursa ya kuondoa changamoto ya uagizwaji wa mafuta ya kula nje ya nchi, bado uzalishaji wa zao hilo umekuwa wa kusuasua.
Tanzania ni miongoni mwa nchi duniani zenye mazingira mazuri ya uzalishaji wa michikichiki lakini inakadiriwa kuwa inaagiza tani zisizopungua 400,000 za mafuta ya mawese kila mwaka hasa kutoka Malaysia ili kufidia pengo la uhaba wa mafuta, licha ya uwezo wa uzalishaji wa mbegu zingine za mafuta.
Kwa mujibu wa kitabu cha Hali ya uchumi wa Taifa cha mwaka 2017, uzalishaji wa mazao ya mbegu za mafuta ya alizeti, karanga, ufuta, mawese na soya uliongezeka hadi tani 6.6 milioni kutoka tani 6.3 milioni mwaka 2016, sawa na ongezeko la asilimia 5.8.
Katika kiwango hicho cha mazao ya mafuta kilichozalishwa, mawese yalichangia tani 42,277 tu kwa mwaka 2017 sawa na asilimia 0.64 ya uzalishaji wote wa bidhaa hiyo. Hata hivyo bado kiasi hicho hakitoshelezi mahitaji yote ya ndani.
Mratibu wa Utafiti wa Kilimo kwa mikoa ya Tabora na Kigoma, Dk Filson Kagimbo amesema michikichi iliyopo sasa ina uwezo wa kuzalisha tani 1.6 ya mawese kwa hekta moja ambao ni uzalishaji mdogo na hauna tija.
Licha ya changamoto za uzalishaji wa zao hilo ikiwemo upatikanaji wa pembejeo, mbegu bora na soko, uzalishaji wa mawese umekuwa ukiongezeka kila mwaka jambo linalotoa matumaini kwa Serikali na wadau wa zao hilo kuweka mikakati ya kuongeza uzalishaji.
Hali ya hewa ya Tanzania inaruhusu michikichi kustawi kwa wingi hasa katika mikoa ya Kigoma, Mbeya (Wilaya ya Kyela) na Pwani ambayo ina hali ya kitropiki hasa joto la wastani na mvua za kutosha.
Kutokana na fursa zilizopo katika zao la michikichi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo kuwawezesha watafiti wa kituo cha utafiti cha zao la michikichi cha Kihinga mkoani Kigoma kuongeza uzalishaji wa mbegu bora za zao hilo.
Majaliwa aliyekuwa akikagua shughuli za uzalishaji wa mbegu za michikichi katika kituo hicho katika ziara yake ya kikazi mkoani Kigoma Februari 17, 2019, amesema Serikali imeamua kulifufua zao hilo kwa lengo la kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula nchini, ambapo kwa mwaka inatumia zaidi ya Sh600 bilioni kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi.
“Wizara ya kilimo iwawezeshe watu wa utafiti ili waendelee na shughuli hiyo kwa kasi, iwaongeze watumishi kituoni hapa na ongezeni nguvu kwenye zao la michikichi kama yalivyofanya mataifa mengine ya Costa Rica na Malaysia,” amesema Majaliwa katika taarifa iliyotumwa na kitengo cha mawasiliano cha ofisi yake.
Amesema wakulima wa zao hilo wanahitaji kupata mafanikio, hivyo kituo hakina budi kuongeza nguvu ya uzalishaji wa mbegu bora ili wafikie malengo na pia amewashauri washirikiane na taasisi binafsi zinazozalisha mbegu.
Miche ya michikichi inachukua muda wa miezi 18 kutoka hatua ya uchavushaji hadi kusambazwa kwa wakulima.
Kwa mujibu wa Dk Kagimbo, kituo hicho cha utafiti wa michikichi kitatoa mbegu bora zinazolenga kumuongezea tija mkulima kwa kuwa zitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani nne kwa hekta, pia wanaendelea kuangalia vinasaba vya mbegu vilivyopo ili wazalishe mbegu bora zaidi.
Wakati wadau wa zao hilo wakiwaza kusambaza mbegu bora, hawana budi kuwasaidia zaidi wakulima kutumia teknolojia ya kisasa ili kuongeza eneo la uzalishaji ikizingatiwa kuwa bado Tanzania ina eneo kubwa la kulima zao hilo.
Soma zaidi:
- Kigoma kinara wa usajili mashamba Tanzania bara
- Tanzania ni miongoni mwa nchi 11 zinazowekeza kwenye utafiti wa GMO Afrika
- Wakulima washauriwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kilimo cha umwagiliaji
Kwa mujibu wa Ripoti ya mwaka ya utafiti wa sekta ya kilimo (AASS 2016/17) iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaeleza kuwa eneo lililopandwa miti ya michikichi mwaka 2016/2017 lilikuwa hekta 9,742 lakini ni asilimia 79.2 tu ya miti hiyo ilivunwa.
Hii inadhihirisha kuwa licha ya jitihada za wakulima kulima zao hilo bado hawafaidiki inavyotakiwa na zao hilo kutokana na kukosa mbinu bora za kulima na masoko ya uhakika hapa nchini.
Hata hivyo, mabonde ya Rufiji mkoani Pwani na Kilombero (Morogoro) yanatajwa kuwa maeneo mapya ya kuendelezwa kwa ajili ya kwa kilimo cha michikichi, jambo litakalosaidia kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kula nchini.
Mafuta ya mawese pia yanafungua fursa ya uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo vya kutengeneza sabuni na kutoa ushindani kwa wajasiriamali wanaozalisha bidhaa hiyo nchini.
Wilayani Kyela, tayari wajasiriamali kama Nuru Njumbo ameanza kutengeneza sabuni hizo lakini ameileza Nukta kuwa changamoto inayowakabili ni upatikanaji wa mawese kwa wakati kutokana na uzalishaji mdogo wa zao hilo.