October 6, 2024

Wachimbaji wadogo wa madini watahadharishwa ujio mvua za masika

Mvua hizo zitanyesha katika mikoa yenye shughuli nyingi za uchimbaji madini ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga.

  • Mvua hizo zitanyesha katika mikoa yenye shughuli nyingi za uchimbaji madini ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga.
  • Ongezeko la maji katika udongo linaweza kusababisha maporomoko ya ardhi na vifo kwa wachimbaji wadogo.

Dar es Salaam. Wakati mwelekeo wa msimu wa mvua katika maeneo yanayopata vipindi viwili vya mvua kwa mwaka ukiratajiwa kuanza Machi mwaka huu, wachimbaji wadogo wa madini  wametahadharishwa kuchukua tahadhari dhidi ya maafa yanayoweza kutokea. 

Wachimbaji wadogo wa madini wamekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya madini hasa katika kukuza pato la Taifa linatokana na uchimbaji wa madini mbalimbali yakiwemo ya Tanzanite na dhahabu lakini bado wanakumbwa na changamoto za usalama.

Kwa mujibu wa Wizara ya Madini, katika robo ya kwanza ya mwaka 2018 baada ya Serikali kujenga ukuta wa Mererani ili kudhibiti utoroshaji wa madini ya Tanzanite, ilifanikiwa kukusanya mrabaha wa kiasi cha Sh618.6 milioni kutoka kwa wachimbaji wadogo ambapo unazidi kiasi kilichokusanywa miaka mitatu iliyopita.

Katika taarifa ya uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa msimu wa mvua katika kipindi cha Machi hadi Mei 2019, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeeleza kuwa wadau wa maendeleo wakiwemo wachimbaji wa madini wanapaswa kuchukua hatua ili kujikinga na maafa yanayoweza kutokea katika kipindi hicho. 

“Shughuli za uchimbaji madini katika migodi midogo midogo zifanyike kwa kuzingatia tahadhari zinazotolewa kwani ongezeko la maji katika udongo linaweza kusababisha maporomoko ya ardhi,” ameeleza Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agness Kijazi katika taarifa hiyo.

Katika kipindi cha Machi hadi Mei, 2019, mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya ukanda unaopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka nchini. 

Hiyo ina maana kuwa maeneo mengi yatapata mvua nyingi na huenda wachimbaji wa madini wakaathirika kutoka na migodi kujaa maji na vifusi kutitia wakati wakiendelea na shughuli zao. 

Dk Kijazi amesema hali hiyo inasababishwa na mifumo ya hali ya hewa hasa mabadiliko ya upepo na joto la bahari ambayo yana mchango mkubwa katika upatikanaji wa mvua Tanzania bara.


Soma zaidi: 


Maeneo ambayo yanatarajia kupata mvua nyingi ni pamoja na mkoa wa Kagera na kusambaa katika mikoa ya Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga ambapo mvua hizo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi.

Mikoa hiyo inatumiwa zaidi na wachimbaji wadogo kujipatia kipato kutokana na biashara ya madini. Ili kuhahakikisha wanakuwa salama ni muhimu kufuatilia kwa karibu taarifa za hali ya hewa katika kipindi chote cha mvua.

Januari 7 mwaka huu wachimbaji watano wadogo wa madini ya dhahabu katika mgodi wa Sekenke Moja wilayani Iramba walifukiwa na kifusi cha udongo wakiwa ndani ya shimo ambapo watatu waliokolewa huku wengine wakipoteza maisha. 

Matukio kama haya yamekuwa yakitokea maeneo mbalimbali nchini hasa wakati wa mvua na kugharimu uhai wa watu. Tahadhari ya mabadiliko ya hali ya hewa inasaidia kupunguza athari zinazoweza kutokea katika maeneo ya uchimbaji.