Daladala zatakiwa kupisha ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka Gerezani
Ujenzi huo unahusisha miundombinu ya barabara ya Kilwa kuanzia katikati ya Jiji la Dar es Salaam hadi Mbagala Rangitatu.
Adha ya foleni bado inawatesa wakazi wa jiji la Dar es Salaam, lakini Serikal inaendelea na jitihada mbalimbali za kupunguza tatizo hilo. Picha|Mtandao.
- Wamiliki wote wa daladala waliokuwa wanatoa huduma katika kituo hicho wanatakiwa kukamilisha kazi ya kuhamisha daladala zao ifikapo Februari , 2019.
- Miundombinu hiyo inahusisha barabara ya Kilwa kuanzia katikati ya Jiji la Dar es Salaam hadi Mbagala Rangitatu.
Dar es Salaam. Wakala wa mabasi yaendayo haraka (DART) umetoa taarifa ya kuwataka wamiliki wote wa daladala wanaotumia kituo cha Gerezani Kariakoo wametakiwa kuondoka katika kituo hicho ifikapo Februari 9, 2019 ili kupisha ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka awamu ya pili.
Awamu ya kwanza ya mradi wa mabasi yaendayo haraka ulihusisha barabara ya Morogoro yaani kuanzia Kimara hadi Kivukoni jijini hapa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa leo (Februari 6, 2019) na DART kwa umma imeeleza kuwa iko katika hatua za kuanza ujenzi wa miundombinu hiyo inahusisha barabara ya Kilwa kuanzia katikati ya Jiji la Dar es Salaam hadi Mbagala Rangitatu; na barabara ya Kawawa kuanzia Magomeni, barabara ya Chang’ombe, Mgulani hadi makutano ya barabara ya Kilwa, na eneo la Mgulani JKT.
“Kwa kuwa eneo la Gerezani linatarajiwa kukabidhiwa kwa mkandarasi kwa ajili ya kuanza ujenzi wa miundombinu hiyo, wamiliki wote wa daladala waliokuwa wanatoa huduma katika kituo cha Gerezani wanatakiwa kukamilisha kazi ya kuhamisha daladala zao ifikapo tarehe 9 Februari 2019.” imesomeka taarifa hiyo.
Hiyo ina maana kuwa watumiaji na madereva wa daladala katika maeneo yaliyotajwa wana siku mbili kutekeleza agizo hilo ili kupisha ujenzi wa miundombinu hiyo inayokusudia kupungua adha ya foleni kwa wakazi wa jiji hilo linalokuwa kwa kasi barani Afrika.
Soma zaidi: Njia za kuepuka foleni kali ya Dar es Salaam kwa kutumia teknolojia
Aidha, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), imetoa utaratibu utakaotumika kwa safari za daladala zinazotumia kituo cha Gerezani ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa SUMATRA leo imeeleza kuwa daladala zote zinazoturnia barabara ya Kilwa kwenda Gerezani kwa sasa zitaenda kituo cha Machinga Complex kupitia barabara ya Msimbazi-Uhuru-Shaurimoyo na kurudi zilikotoka kupitia Barabara ya Lindi na Shaurimoyo.
Pia daladala zote zinazotumia barabara ya Chang’ombe kwenda Gerezani zitaenda eneo la mtaa wa Lindi kupitia barabara ya Shaurimoyo-Lindi na kurudi zilikotoka kupitia barabara Lindi na Shaurimoyo.
Aidha, daladala zote zinazoturnia barabara ya Nyerere na Uhuru kwenda Gerezani, kwa sasa zitaelekea Mnazi Mimoja na kurudi zilikotoka kupitia barabara ya Nyerere na Uhuru.
Kwa maelezo zaidi juu ya utaratibu huo mpya unatakiwa kuwasailiana na ofisi ya SUMATRA na DART.
Ujenzi huo wa barabara ya mabasi yaendayo haraka, unakuja siku chache tangu Serikali itangaze rasmi kuanza mchakato wa ujenzi wa daraja la juu la Gerezani na zaidi ya miezi mitano tangu kuzinduliwa kwa daraja la juu la Mfugale (Mfugale flyover) ambalo limesaidia kupunguza adha ya foleni katika makutano ya barabara ya Mandela na Nyerere huku ujenzi wa daraja lingine la juu la Ubungo ukiendelea.
Kukamilika kwa barabara hiyo huenda kutasaidia kupunguza foleni ya magari na adha ya usafiri kwa wananchi wanaotoka Mbagala Rangitatu na kuja katika ya jiji na kuongeza kasi ya shughuli za biashara katika maeneo hayo.