November 24, 2024

CCM yazidi kuongeza umiliki wa vyombo vya habari Tanzania

Mwenyekiti wa chama hicho Rais John Magufuli amesema Africa Media Group inayomiliki vituo vya Channel Ten, Magic FM na Classic FM ni mali ya CCM.

  • Mwenyekiti wa chama hicho Rais John Magufuli amesema Africa Media Group (AMGL) ni mali ya CCM.
  • Ameeleza kuwa uongozi wa chama hicho kikongwe nchini utaangalia namna wa kuitafutia kampuni hiyo mtaji.
  • AMGL inamiliki vyombo maarufu vya habari vya utangazaji vikiwemo Channel Ten, Magic FM na Classic FM.

Dar es Salaam. Ni rasmi sasa kampuni ya habari ya Africa Media Group (AMGL) imeingia kwenye orodha ya vitega uchumi vya Chama cha Mapinduzi (CCM) baada ya Rais John Magufuli kueleza kuwa ni mali ya chama hicho kikongwe nchini.

Kampuni ya AMG inamiliki vyombo maarufu vya habari vya utangazaji vikiwemo Channel Ten, Magic FM na Classic FM.

Umiliki huo sasa unaifanya CCM kuongeza umiliki wa soko katika tasnia ya habari nchini baada ya kumiliki magazeti ya Uhuru, Mzalendo na kituo cha redio cha Uhuru FM.

Katika ziara yake ya kushtukiza katika ofisi za kampuni hiyo, Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa CCM amesema kuwa baada ya kuchukua kampuni hiyo, chama hicho kitakaa hapo baadaye kuangalia namna bora ya kuiwezesha kimtaji.

“Najua mnatambua tumekuwa na uongozi mpya, mabadiliko madogo, baada ya kujua rasmi kwamba chombo hiki Africa Media Group ni mali ya Chama cha Mapinduzi (CCM),” amesema Dk Magufuli katika ziara hiyo ya kuazimisha miaka 42 ya kuanzishwa kwa CCM.

“Siku za nyuma kulikuwa na matatizo fulani ambayo  yamekuwa solved (yamEshatatuliwa) kwa asilimia 100.”

Dk Magufuli amewaeleza wafanyakazi wa kampuni hiyo, iliyoanzishwa mwaka 1999, kuwa katika mabadiliko hayo ya umiliki na kiungozi “hakuna atakayepunguzwa kazi.”

Kampuni hiyo, kwa mujibu wa Rais Magufuli, ina wafanyakazi 99. Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa juu wa CCM kuelezea umiliki wa kampuni hiyo kubwa ya habari nchini.

Katika mazungumzo hayo na wafanyakazi wa AMGL, Dk Magufuli amesema kuwa watahakikisha vituo vya kampuni hiyo vinafikika nchi nzima na kupatikana kimataifa.

“Huwezi kuwa chombo cha kibiashara halafu kiwe kinaonekana Dar tu ni ‘contradiction’ (mkanganyiko),” amesema Rais Magufuli na kuongeza,

“Taarifa ni ‘business’ (biashara)…mtu akileta tangazo lake ahakikishiwe atakuwa na uhakika kuwa linaonekana mpaka Burundi.”


Soma pia: Hisa za Serikali kampuni ya Airtel Tanzania zaongezeka


Miongoni mwa hatua za awali ambazo Rais amezieleza katika kuiboresha kampuni hiyo ni kuwanunulia vifaa vya kisasa, kuboresha maslahi ya wafanyakazi zikiwemo bima za afya na kuwapatia mtaji.

Miongoni mwa ahadi za awali ni kuwapatia Sh200 milioni za vifaa vya kisasa zikiwemo kamera kwa awamu mbili za Sh100 milioni.

“Tutakaa sisi kwenye chama na viongozi, na Katibu Mkuu (Dk Bashiru Ally) amekuwa ananibrief, tuangalie ni namna gani kutoa mtaji wa kutosha kwa ajili ya kusaidia hiki chombo,” amesema.

CCM inachukua umiliki wa AMG wakati tasnia ya vyombo vya habari ikipitia katika kipindi kigumu kutokana na kushuka kwa mapato yatokanayo na matangazo kulikochagizwa na mabadiliko ya teknolojia ya dijitali yaliyofanya watangazaji kuangazia njia nafuu za mtandaoni kujitangaza.