October 6, 2024

Una mpango wa kutembelea mbuga za wanyama? Zingatia haya

Hakikisha unabeba maji ya kunywa, mafuta ya kujikinga dhidi ya wadudu, miwani, kofia na nguo nyepesi zisizong’aa.

  • Hakikisha hauvai nguo zinazong’aa maana zinawavutia wanyama na wadudu kama mbung’o.
  • Wadau wanashauri ujipange kama utapenda kuweka kambi mbugani ili uweze kufurahia safari yako.
  • Hakikisha dereva anatakaye kutembeza mbugani ana uzoefu na leseni inayomruhusu kazi hiyo

Dar es salaam. Kusafiri kwenda maeneo ya utalii ni jambo la kufurahisha hasa kama unapenda uoto na mandhari ya dunia nje ya maeneo ya mji au kujua historia ya vitu mbalimbali.

Pia ni moja ya njia ya kubadilisha hali ya hewa na kujitengenezea kumbukumbu za maisha zitakazodumu katika kizazi kijacho.

Tanzania ina vyote hivyo kuanzia mito, milima, mabonde, mbuga na maeneo mengi ya historia ambayo ni kivutio kikubwa kwa watalii wa ndani na nje. 

Kama una mpango wa kutembelea mbuga za wanyama hivi karibuni ili kupata furaha ya moyo, vipo vitu muhimu unavyotakiwa kubeba ili kukuhakikishia usalama wa afya yako na kukulinda na hatari yoyote inayoweza kutokea wakati wa matembezi. 

Kwa kuliona hilo Nukta tunakuletea vitu vya kubeba unapokuwa mbugani ili uweze kufurahia safari yako na kuifanya iwe ya pekee.

Aina, rangi za nguo

Nguo zinatakiwa ziwe za kawaida zitakazokufanya kufurahia mizunguko ya mbugani kama pensi na shati. Unashauriwa kuvaa nguo nyepesi ili kupunguza uzito wa kuupa mwili nafasi ya kuapata hewa. Lakini kama unatembelea mbuga zenye baridi kali unaweza kuvaa suruali pamoja na sweta au koti.

Ni vema uvae nguo zisizong’aa kwa sababu zinavutia baadhi ya wadudu kama mbung’o ambao wanaleta madhara ya kiafya, jambo linaloweza kuharibu maana zima ya wewe kwenda kutembelea mbugani.

“Nashauri wakija mbugani kutokuvaa nguo kama ya rangi ya bluu na nyeusi au rangi zinazong’aa zinawavutia wanyama na wadudu kama mbung’o,” ameeleza Mbena

Mbena ameiambia Nukta kuwa watalii wajitahidi kuvaa nguo zilizopoa kama za kaki na viatu vya kutumbukiza ili waweze kujikinga dhidi ya wadudu, mimea na wanyama katika miili yao.  

Kumbuka kofia na miwani

Hivi ni vitu muhimu vya kubeba unapotembelea mbugani ili kujikinga na jua au vumbi linaweza kuwa na athari kwa macho na nywele. Ni vema kuchagua miwani inayoweza kuendana na hali ya hewa ya eneo husika. 

Hakikisha ukiwa mbugani usivae nguo zitakazowavutia wanyama au wadudu hatarishi wanaoweza kukuletea madhara ya kiafya na kuharibu furaha yako. Picha| Hotstar

Vinywaji na vitafunwa

Wataalam wanashauri kubeba vinywaji kama soda au maji kwa ajili ya kukupoza na kiu. Vinywaji hivyo vitawasaidia wale wanaotembea masafa marefu au kupanda milima ambapo wanahitaji nguvu ya kukamilisha matembezi yao.  

“Wasisahau kubeba vinywaji na vitafunwa inaweza kuwa biskuti, korosho au keki kwa ajili ya kula wawapo mbugani, safari ni furaha na inaenda na kuwepo kwa chakula,” amesema Afisa Mawasiliano Mwandamizi wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), Catherine Mbena.


Zinazohusiana:


Mafuta na dawa za kuua wadudu hatarishi

Njia nyingine ya kujikinga na wadudu hatarishi kama mbu, mbung’o na nzi ni kubeba dawa kuua wadudu ambazo tunazitumia zaidi majumbani kupulizia maeneo yenye wadudu. Ikiwezekana beba mafuta yaliyotengenezwa maalum kukabiliana na wadudu ambao ambao wanashambulia nguzi ya mwili wako. 

Hema linatakiwa kuwa na nafasi itakayokusaidia kupumzika na kuona eneo la mbuga vizuri. Picha|mbuganicamps.com

Matumizi ya mahema

Muungozaji wa watalii, Makarious Judica anasema kwa watu wanaopenda kuweka kambi mbugani ni vema wabebe vitu muhimu kama vyakula, mashuka, mahema na viti vya kukalia ili waweze kufurahia vizuri.

Judica ambaye pia ni Mwanasheria anasema, “hakikisha unakuwa na dereva ambaye anajua maeneo ya utalii mwenye leseni ya kuwaendesha watalii, uweze kujifunza mengi.”

Hata hivyo, raha ya kutembea ni kujenga kumbukumbu hivyo usisahau kubeba kamera au simu ili kupata video na picha mnato zitakazoendeleza furaha yako hata ukiwa nyumbani.