October 6, 2024

Wakulima kuwezeshwa kuuza pamba kwa bei wanayotaka

Hatua hiyo itafikiwa baada ya Serikali kukamilisha mchakato wa uwekezaji katika zao hilo ikiwemo kujenga viwanda vya kuchakata pamba hapa nchini.

  • Hatua hiyo itafikiwa baada ya Serikali kukamilisha mchakato wa uwekezaji katika zao hilo ikiwemo kujenga viwanda vya kuchakata pamba hapa nchini. 
  • Imesema haiwapangii wakulima bei ya kuuza pamba bali huratibu upatikanaji wa bei nzuri inayoweza kuwanufaisha wafabiashara na wakulima  baada ya mavuno. 

 Dar es Salaam. Wakulima wataanza kufaidika na fursa ya kuuza pamba kwa bei wanayotaka, baada ya Serikali kukamilisha mchakato wa uwekezaji katika zao hilo ikiwemo kujenga viwanda vya kuchakata pamba hapa nchini. 

Pia imesema haiwapangii wakulima bei ya kuuza pamba bali huratibu upatikanaji wa bei nzuri inayoweza kuwanufaisha wafabiashara na wakulima baada ya mavuno. 

Naibu wa Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa aliyekuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), Gimbi Masaba bungeni Januari 29, 2019 ambaye alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuwaachia wakulima wauze pamba kwa bei kubwa wanayotaka. 

Gimbi amesema Serikali imekuwa ikiwapangia wakulima wa pamba bei ndogo wakati wa mavuno bila kuzingatia gharama walizotumia kipindi cha uzalishaji. 

Akijibu swali hilo, Bashungwa amesema suala la kupanga bei haliamuliwi na Serikali peke yake bali hufanyika kwa kuwashirikisha wakulima kupitia vyama vya ushirika kwa kuzingatia vigezo mbalimbali vya kitaalam. 

“Upangaji wa bei ya pamba huzingatia vigezo mbalimbali ikiwemo bei pamba nyuzi, katika soko la dunia, kiwango cha kubadilishia fedha, bei ya mbegu za pamba, gharama za usafirishaji, uchambuaji na uwiano kati ya nyuzi na mbegu,” amesema Bashungwa. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba, Marco Mtunga (watatu kulia) kuhusu zao la pamba lililostawi vizuri wakati alipotembelea shamba darasa  katika kijiji cha Kilyaboya wilayani Kwimba Februari 16, 2018. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.

Sheria ya Pamba namba 2 ya mwaka 2001 inaipa Bodi ya Pamba jukumu la kukaa na wawakilishi wa wakulima na kampuni za kununua pamba kukubaliana bei elekezi inayozingatia hali ya pamba.

Hata hivyo, Bashungwa ambaye ameingia katika wizara hiyo hivi karibuni baada ya Rais John Magufuli kufanya mabadiliko madogo ya baraza la Mawaziri, amesema bado wakulima hao wana nafasi ya kupanga bei wanayoitaka hapo baadaye wakati Serikali itakapokamilisha uwekezaji wa viwanda vya kuchakata pamba nchini. 

“Fursa ya wakulima wa pamba kuuza bei wanayotaka itaongezeka kwa kuwa Serikali inaendelea kuhamasisha uwekezaji katika tasnia ya pamba hasa kuongezeka viwanda vya kuchakata pamba hapa nchini,” amesema. 

Amebainisha kuwa Septemba 2018 wakulima wa mkoa wa Simiyu waliuza pamba kwa Sh1,200 kwa kilogramu moja juu ya bei elekezi kutokana na mabadiliko ya pamba katika soko la dunia. 


Zinahusiana: 


Pamba inategemewa zaidi na wakulima wa mikoa ya Simiyu, Mwanza, Shinyanga, Geita, Tabora, Mara, Kagera, Singida, Kigoma na Katavi, ambapo ni miongoni mwa mazao saba ya biashara yanayoingiza fedha nyingi za kigeni. 

Mathalani mwaka 2017, pamba iliingiza fedha za kigeni Sh80.2 bilioni ikiwa juu kidogo ya katani iliyoingiza Sh57.7 bilioni na nyuma ya Chai.

Januari 18, 2019, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliitaka Bodi ya Pamba ifanye kazi kwa karibu na wakulima na Wakuu wa Mikoa inayolima pamba ili kuhakikisha msimu huu zao hilo linafikia malengo ya uzalishaji.

“Lego letu mwaka huu 2019 ni kuzalisha tani zisizopungua 600,000. Wote mmeeleza kuwa wakulima wako kazini, pamba inalimwa, mnachosubiria ni dawa za kuuza wadudu waharibifu, na Bodi imeeleza kuhusu upatikanaji wa dawa hizo,” alisema Majaliwa.