October 6, 2024

Ukanda maalum utalii wa fukwe kuipaisha Tanzania kimataifa

Utalii huo utahusisha fukwe kutoka Bagamoyo hadi Tanga na Ziwa Victoria katika eneo la Chato ili kuisaidia Serikali kupata watalii milioni nane ifikapo 2025.

  • Utalii huo utahusisha fukwe kutoka Bagamoyo hadi Tanga na ZIwa Victoria katika eneo la Chato. 
  • Fukwe hizo zitajengewa miundombinu muhimu ikiwemo barabara, gati la boti, maeneo ya wazi yatakayokuwa na huduma za kijamii. 
  • Utasaidia kufanikisha mikakati ya Serikali ya kupata watalii milioni nane ifikapo 2025.

Dar es Salaam. Huenda Tanzania ikapata watalii milioni nane ifikapo 2025, baada ya Serikali kuanza mchakato wa kuanzisha ukanda maalum wa utalii wa fukwe kutoka Bagamoyo hadi Tanga unakusudia kufungua fursa mbalimbali za shughuli za utalii.

Utalii huo pia utahusisha fukwe ya Ziwa Victoria katika eneo la Chato ambapo inapatikana Hifadhi ya Taifa ya Burigi na eneo la Kilwa mkoani Mtwara. 

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla ameandika katika ukurasa wake wa Twitter juzi (Januari 27, 2019) kuwa ikiwa Tanzania inataka kufaidika na sekta ya utalii kuna kila sababu ya kukuza aina mbalimbali za utalii zitakazosaidia kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchini kila mwaka.   

“Ili tufikie lengo la watalii milioni nane mwaka 2025, tunahitaji kukuza aina nyingine zaidi za utalii; utalii wa fukweni, utalii wa michezo, utalii wa utamaduni na utalii wa mikutano. Pia kufungua sakiti nyingine mpya zaidi za utalii; Kusini, Magharibi na Kaskazini Magharibi,” ameandika Kigwangalla.

Kwa mujibu wa Kigwangalla, fukwe zilizopo maeneo mbalimbali nchini hasa pwani ya bahari ya Hindi hazijatumika ipasavyo kutoa fursa kwa wananchi  na Serikali  kufaidika na rasilimali hiyo. 

Fukwe za bahari na maziwa ni rasilimali muhimu kuvutia wawekezaji kuja nchini. Picha| Muungwana.

Hata hivyo, wanakusudia kuziboresha fukwe hizo kwa kutengeneza maeneo ya kupumzika, kuboresha usafiri wa boti na huduma za uongozaji watalii kulingana na jiografia ya nchi. 

Sambamba na hilo ni kuwa na gati la boti za kitalii na barabara kubwa zitakazounganishwa na fukwe hizo ili kuondoa changamoto ya usafiri ambayo imekuwa ikiathiri shughuli za utalii hasa wakati wa masika. 

“Tuna Watanzania wapatao milioni 55, tunahitaji kuendeleza products (bidhaa) zitakazowavutia watanzania na wana Afrika Mashariki, Kati na SADC yote. Tunahitaji ‘theme park’ (eneo la wazi) pia kuendeleza fukwe, klabu za starehe za kimataifa, kushusha gharama za usafiri wa anga, kurahisisha visa,” ameandika.

Ukanda huo utasaidia kufungua milango ya ajira kwa wananchi wanaozalisha bidhaa za asili zitakazokuwa zinauzwa kwa watalii wa kimataifa ambao wanapendelea kutembelea fukwe.


Zinazohusiana: 


Akizungumzia suala la fukwe ya Ziwa Victoria, amesema ni eneo muhimu kwa utalii ikizingatiwa kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa uwanja wa ndege wa Chato na reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, jambo litakalosaidia kukuza utalii Kaskazini  Magharibi mwa Tanzania. 

“Ndege zitatua Chato kwa sababu kuna potential (rasilimali). Kuna hifadhi nzuri zaidi pale. Kuna ziwa. Kuna ardhi nzuri (horticulture). Kuna dhahabu. Kuna samaki. Ndege zitasaidia usafirishaji wa watalii, wafanyabiashara na wawekezaji. Tutajenga na ukumbi wa mikutano,” amefafanua. 

Chato ni eneo la kimkakati kwa sababu liko karibu na mapori ya akiba ya Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika ambapo Serikali inakusudia kuyaunganisha ili kuunda hifadhi moja ya Taifa.  

Kulingana na takwimu za Wizara ya Maliasili na Utalii, sekta hiyo inachangia takriban asilimia 17.2 ya Pato la Taifa (GDP) na takribani robo ya mapato yote ya fedha za kigeni. Pia inachangia zaidi ya asilimia 10 ya ajira zote nchini.