November 28, 2024

Bajeti inavyookoa matumizi mabaya ya fedha ngazi ya familia

Orodhesha mapato na matumizi kabla ya kuanza kutumia pesa.

  • Orodhesha mapato na matumizi kabla ya kuanza kutumia pesa.
  • Weka akiba kwa ajili ya dharura na maendeleo ya baadaye.

Katika maisha huwezi kukwepa vitu viwili yaani mapato na matumizi. Lakini changamoto inayojitokeza ni kuzipangilia vizuri pesa ili zikidhi mahitaji yako binafsi na familia. 

Matumizi mazuri ya mapato yanayotokana na mshahara au faida ya biashara hutegemea zaidi jinsi unavyopanga bajeti yako. 

Kwanini upange bajeti kwa kila pesa inayoingia mfukoni mwako? Kuna ulazima wa kufanya hivyo kwasababu itakusaidia kujua maeneo muhimu ya kuyapa kipaumbele na kutunza pesa kwa ajili ya dharura au mipango ya baadaye ya maendeleo. 

Wengi wanaingia katika matatizo au kutokujua pesa yao inatumikaje kwasababu hawana utaratibu wa kupanga bajeti. Ufanye nini kuwa na matumizi mazuri ya pesa?

Fahamu kipato chako

Hatua ya kwanza itakayokusaidia kuwa na matumizi mazuri ya pesa ni kujua kila mwezi unaingiza kiasi gani kulingana na vyanzo vya mapato yako. Jumlisha mapato yako yote kujua kiasi halisi ambacho kinaingia mfukoni mwako ili kukuwezesha kuanza mchakato wa matumizi na kuweka akiba.


Zinazohusiana: 


Fuatilia matumizi yako kila mwezi

Hapa unatakiwa kuorodhesha matumizi yako yote ikiwemo kodi ya nyumba, ada za watoto, usafiri, chakula, umeme, maji. Hakikisha matumizi yote unayotarajia kufanya mwezi husika yanajulikana hata kama ni madogo kiasi gani, itakusaidia kufanya ulinganifu wa kipato chako. 

Acha mazoea ya kutumia pesa bila mipango utakwama mahali hasa wakati una uhitaji mkubwa wa pesa. Pia kujua unatumia kiasi gani kila mwezi itakusaidia kuepuka matumizi yaliyo nje ya bajeti. Ili ufanikiwe unahitaji ya  nidhamu ya matumzi ya pesa. 

Hakikisha matumizi yako hayazidi kipato unachopata kila mwezi ili kuepuka madeni. Picha| diplomatmagazine.nl

Tarajia yasiyotarajiwa

Kuna wakati mwingine unaweza kupata dharura kama kuumwa au msiba ambao unahitaji pesa. Ndiyo maana unashauriwa katika bajeti yako weka pesa ya dharura au weka utaratibu wa kutunza pesa kila inapobidi. 

Wataalamu wa masuala ya fedha wanashauri uweke angalau akiba ya asilimia 10 ya mapato yako kila mwezi. 

Punguza matumizi

Kama unajikuta kila mwezi unatumia zaidi ya mapato unayoingiza kwenye kibubu chako, angalia namna ya kupunguza baadhi ya matumizi ambayo hayataathiri mwenendo wa maisha yako. 

Mfano kila mwezi umejiwekea utaratibu wa kununua nguo au kutembelea vivutio vya utalii, unaweza kuacha mpaka mambo yatakapokunyookea. Na pesa hiyo ikatumika kushughulikia mambo ya msingi.

Punguza matumizi yasiyo ya lazima na peleka pesa yako kwenye mambo ya msingi ili maisha yaende. Picha| GOBankingRates

Tumia teknolojia

Zipo programu tumishi mbalimbali (Apps) kama Quicken na Mint zinaweza kukusaidia kutengeneza bajeti binafsi. 

Huduma kama hizo zinapatikana mtandaoni zinasimamia na kufuatilia mwenendo wa mapato na matumizi yako na pale inapohitajika kukushauri kulingana unavyozitumia. Kwa sehemu kubwa utendaji wa Apps hizo hutegemea utashi na utayari wa mtumiaji kujiwekea nidhamu na kuwa mkweli kwa maisha yake mwenyewe.

Hata hivyo, mafanikio ya bajeti yanaanza kwa kubadilisha mtazamo na tabia zisizofaa za matumizi ya pesa. Bajeti ni kila kitu kwenye maisha. Mafanikio yanategemea jinsia unavyopanga mipango yako.