October 6, 2024

Wadau wa elimu watoa neno udanganyifu matokeo kidato cha nne 2018

Wamesema vitendo hivyo siyo ishara nzuri kwa maendeleo ya Taifa kwasababu vinaibua changamoto za weledi katika soko la ajira.

Wanafunzi wakiwa kwenye chumba cha mtihani. Lakini katika miaka ya hivi karibuni vitendo vya udangajifu vimeshamiri hasa katika mitihani ya kidato cha nne, jambo linaibua maswali mengi juu ya elimu nchini. Picha|Mtandao.


  • Wamesema vitendo hivyo siyo ishara nzuri kwa maendeleo ya Taifa kwasababu vinaibua changamoto za weledi katika soko la ajira.
  • Sababu kuu ya udanganyifu ni maandalizi hafifu kwa wanafunzi kuwawezesha kujibu mtihani.
  • Washauri uboreshaji wa mbinu za kufundishia na kuongeza udhibiti kwenye vyumba vya mitihani.

Dar es Salaam. Wakati matokeo ya kidato cha nne mwaka 2018 yakionyesha ufaulu umeongezeka kwa asilimia 78.38, matokeo hayo yanaibua mwaswali mengi kutokana na ongezeko la vitendo vya udangajifu vilivyosababishwa matokeo ya baadhi ya wanafunzi kufutwa na wengine kuzuiliwa. 

Matokeo hayo yanaonyesha kuwa ufaulu umeongezeka kwa asilimia 1.29 ukilinganisha na ufaulu wa asilimia 77.0 wa mwaka 2017.  

Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Dk Charles Msonde aliyekuwa akitangaza matokeo hayo leo (Januari 24, 2019) jijini Dodoma amesema jumla ya watahiniwa 426,988 walisajiliwa kufanya Mtihani wa Kidato cha Nne 2018  ambapo kati hayo watahiniwa 322,965 wamefaulu. 

Ubora wa ufaulu kwa kuangalia madaraja waliyopata watahiniwa wa Shule umeongezeka ukilinganisha na miaka miwili iliyopita, japokuwa katika kipindi chote hicho haujazidi asilimia 50 ya watahiniwa wote.

“Aidha, takwimu zinaonesha kuwa idadi ya watahiniwa waliopata ufaulu mzuri wa daraja la I – III imeongezeka ambapo mwaka wa 2016 ilikuwa ni asilimia 27.60, mwaka 2017 asilimia 30.15 na mwaka 2018 imekuwa ni asilimia 31.76 (wanafunzi 113,825),” amesema Dk Msonde.

Pamoja na kuwa ufaulu umeendelea kuimarika, matokeo hayo yanaonyesha kuwa ufaulu wa masomo ya Physics, Basic Mathematics, Commerce na Book-keeping upo chini ya asilimia hamsint. 

Dk Msonde amesema watafanya uchambuzi wa kina wa matokeo hayo kwa kila somo na kutoa machapisho ya uchambuzi huo yatakayowasilishwa kwa wadau wa elimu, zikiwemo shule zote za sekondari nchini kwa lengo la kuwawezesha walimu kutumia taarifa za uchambuzi katika kuboresha ufundishaji na ujifunzaji shuleni.

Matokeo hayo yanaibua maswali mengi kuhusu kushamiri kwa vitendo vya udangajifu katika vyumba vya mitihani, jambo linalosababisha wanafunzi kufutiwa matokeo kila mwaka. 

Maswali hayo yanajikita zaidi kutathimini hatua zinazochukuliwa kuwaandaa wanafunzi kujibu mitihani bila kuwa na fikra za kutumia njia zisizo halali kufaulu ili kujipatia nafasi ya kuendelea mbele kimasomo.

Katika matokeo ya mwaka 2018, NECTA imefuta matokeo ya watahiniwa 252 waliobainika kufanya udanganyifu ambapo wawili waliandika matusi katika sktripti zao. 

Idadi hiyo ya wanafunzi waliofutiwa matokeo ni sawa na kusema shule sita zenye watahiniwa wasiozidi 40 hawataendelea na masomo ya kidato cha tano mwaka huu.

Ukilinganisha na matokeo ya mwaka 2017, utagundua kuwa vitendo vya udangajifu wa mitihani vimepungua kidogo lakini huenda idadi hiyo ikaongezeka zaidi baada ya NECTA kukamilisha uchunguzi wa matokeo yaliyozuiliwa ya wanafunzi 381 wa shule za St. Mathew na St. Marks za jijini Dar es Salaam. 

Licha ya kuwa vitendo vya udanganyifu vinaendelea kudhibitiwa lakini baadhi ya wanafunzi na walimu wanabuni njia mpya kila siku ili kutimiza malengo yao yaliyo kinyume na miongozo ya mitihani.

Wachambuzi wengine wa masuala ya elimu wanasema udangajifu wa mitihani sio ishara nzuri kwa Taifa hasa katika sekta ya elimu inayotegemewa kuzalisha wahitimu wenye uwezo na weledi wanaohitajika katika soko la ajira na maendeleo. 

Zipo sababu mbalimbali ambazo zinachagiza wanafunzi na walimu kujiingiza katika udanganyifu ikiwemo wanafunzi kukosa maarifa ya msingi na maandalizi hafifu kuwawezesha kujibu mtihani na hivyo kutafuta njia ya mkato kufikia mafanikio ya elimu.


Zinazohusiana:


Mhadhiri wa Shule Kuu ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DUCE), Dk Luka Mkonongwa ameiambia www.nukta.co.tz kuwa ushindani wa kibiashara wa shule kupata matokeo mazuri nao unachangia shule au wanafunzi kuingia katika tamaa ya kushiriki  vitendo hivyo. 

“Jambo lingine linalojitokeza kwenye shule binafsi zimekaa kibiashara zaidi, wao huwa wanapenda kuona shule zao ziko ngazi fulani kwahiyo kipindi cha mitihani watafanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba shule inafaulisha,” 

Amesema wakati mwingine motisha zinazotolewa kwa walimu zinawashawishi kutumia njia zisizo halali kuwafaulisha wanafunzi wao ili kujipatia motisha kubwa kutoka kwa wamiliki wa shule baada ya matokeo kutoka. 

Katika kuhakikisha vitendo hivyo vinadhibitiwa, Serikali imeshauriwa kuongeza usimamizi wa mitihani na kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji ili kuwawezesha wanafunzi kupata maarifa yatakayowawezesha kujibu mtihani.

Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini kampasi ya Dar es Salaam (TUDARCO), Richard Ngaiza amesema mikakati ya kuwaandaa wahitimu ni muhimu ianze ngazi ya shule za msingi kwa wanafunzi kufundishwa maadili mema yanayotakiwa katika elimu ili kujenga kizazi kinachozingatia taaluma katika shughuli za maendeleo.