Epuka haya unapofanya biashara mtandaoni
Mambo hayo ni pamoja na kuweka maudhui ya upotoshaji dhidi ya wateja yasiyoendana na biashara yako.
- Mambo hayo ni pamoja na kuweka maudhui ya upotoshaji dhidi ya wateja, yasiyoendana na biashara yako.
- Lenga zaidi kutoa taarifa, kuelimisha, kuburudisha na kuwaleta pamoja wateja wako.
Una mpango wa kuipeleka biashara yako mtandaoni mwaka huu wa 2019? Au tayari unatumia mitandao ya kijamii kuwafikia wateja wako? Unapaswa kufahamu mambo ya msingi ya kuzingatia kabla ya kuweka maudhui yanayoelezea biashara yako mtandaoni.
Ufahamu huo utakusaidia kuelewa ni aina gani ya maudhui ya kibiashara yanayowavutia watumiaji wa mitandao ili kujiweka katika nafasi ya kupata faida uliyokusudia.
Epuka kuweka mambo haya mtandaoni mwaka 2019 ili kuinusuru biashara yako:
Mabandiko hasi kuhusu wateja wako
Hata kama mteja wako amekuudhi kiasi gani, epuka kumjibu vibaya au kuweka mabandiko ‘posts’ hasi dhidi yake kwasababu anaweza kuchafua jina la biashara kwa watu wengine wanaofuatilia mtandao wako.
Muhimu ongea na wateja wako kwa lugha ya upole huku ukizingatia taaluma na misingi ya biashara yako.
Kuwa makini wakati ukiweka maudhui ya kibiashara mtaondaoni ili kujiepusha kuwatusi wateja. Picha| Opinionmeter
Maudhui yasiyoendana na biashara yako
Jaribu kuzuia maudhui yasiyo rasmi ambayo yatahamisha malengo ya biashara yako. Njia rahisi ni kutenga muda au siku ambayo unaweza kujiachia na wateja wako kwa mazungumzo yasiyo rasmi.
Mfano unaweza kuitenga siku ya jumamosi kama ‘Siku ya Utani’ ambayo itakuwa inarejea posts zako zilizopita.
Soma zaidi:
- Namna huduma kwa wateja inavyoweza kukuza brand ya biashara
- Mambo ya kuzingatia unapoanzisha brand yako ya biashara
Maudhui ambayo hayajahaririwa
Ni kweli mitandao ya kijamii ni jukwaa lisilo rasmi. Hiyo haimaanisha kuwa weledi na taaluma ya kuandika isizingatiwe. Hakikisha kabla hujabonyeza kitufe cha kuruhusu maudhui yawafikie wateja wako, soma mara mbili ikiwezekana mpe mtu mwingine naye apitie ili kuondoa makosa.
Makosa madogo madogo ya herufi au sentensi yanaweza kuigharimu biashara yako. Umakini wa kuandika unaenda sambamba na huduma au bidhaa unazouza.
Kuzitangaza na kuzisifia bidhaa kupita kawaida
Dhumuni la mitandao ya kijamii ni kujenga ushawishi, kuimarisha ‘brand’ ya biashara, mahusiano na wateja wako. Fikiria zaidi kutoa taarifa, kuelimisha, kuburudisha na kuwafanya wateja kuwa sehemu ya biashara yako.
Matangazo ya bidhaa huwachosha wafuasi lakini waonyeshe umuhimu wa kutumia bidhaa yako bila kuwasurutisha kuitumia.
Ufanye mtandao wako kuwa sehemu ya watu kupata suluhisho ya changamoto wanazozipata ili kuongeza uungwaji mkono wa biashara yako. PIcha| wired.com
Mabandiko ya upotoshaji
Epuka kuweka mabandiko yasiyo na ukweli kuhusu bidhaa, huduma au washindani wako ili tu kujipatia wafuasi wengi na faida.
Upotoshaji utakuondolea kuaminiwa na wateja, ikigundulika kuwa matokeo yaliyokusudiwa hayajatokea utawafanya wengi wakimbie na kutafuta bidhaa zingine.
Pia kama umetumia maudhui ya mtu au taasisi isiyo yako ni vema kunukuu chanzo cha taarifa hiyo unayoweka mtandaoni.
Hata hivyo, mitandao ya kijamii ni njia tu ya kuikuza biashara yako. Muhimu ni kuzingatia ubora wa bidhaa, vifungashio na mazingira unapofanyia biashara yako.