October 6, 2024

Vitenge vinapotumika kuongeza nakshi ofisini

Wabunifu wanatumia kama mapambo ya taa, viti ili kuongeza mvuto na kuendeleza utamaduni wa Afrika.

Muonekano wa vitenge unaongeza mvuto kwa ofisi na wafanyakazi kutimiza majukumu yao kwa weledi. Picha| Daniel Samson.


  • Wabunifu wanatumia kama mapambo ya taa, viti ili kuongeza mvuto na kuendeleza utamaduni wa Afrika.
  • Vitenge ni ajira kwa vijana wabunifu waliojikita kutumia rasilimali zinazowazunguka.
  • Wabunifu wameenda mbali zaidi na kutumia vitenge kupamba na kuongeza naksi kwenye magari.

Mara nyingi ubunifu  hutafsiriwa kuwa ni kitu fulani kinachoonekana chenye mchango wa wazi katika jamii au matumizi ya njia bora zaidi kutatua changamoto ambazo zipo lakini hazijapatiwa ufumbuzi. 

Lakini inaelezwa kuwa ili dhana hiyo itimilike ni mpaka bidhaa, huduma, teknolojia inayotumika kutatua changamoto husika iwe adimu katika masoko ya kiuchumi na jamii. 

Tumezoea kuona vitenge vikitumika kwa watu kushona mitindo mbalimbali ya mavazi ili kujisitiri na wengine kudumisha na kuendeleza utamaduni wa Afrika. Lakini ni nadra kuona vitenge vikitumika kama sehemu ya kupendezesha ofisi. 

Hapo ndipo dhana ya ubunifu inakuja yaani kutumia rasilimali iliyopo kwa matumizi mengine ili kuleta tija katika eneo la kazi.

Kampuni ya uwekezaji wa kampuni zinazochipukia (Startups) ya Seedspace ya jijini Dar es Salaam inayojishughulisha kuendeleza ubunifu na ujasiriamali wa teknolojia imefanikiwa kutumia vitenge kama sehemu ya mapambo ya ofisi yake. 

Inatumia vitenge kama mapambo ya taa zilizofungwa ukutani na kuzungushiwa kifaa maalum ambacho kimefunikwa na kitenge, ikiwa ni ubunifu wa kunogesha mvuto kwa wageni wanaofika ofisini hapo. 

Muonekano wa ofisi ni pamoja na kuziwekea taa nakshi na urembo wa aina yake. Picha| Daniel Samson.

Meneja wa Seedspace Tanzania, Innocent Mallya amesema walifanya tafiti mbalimbali kuhusu muonekano unaovutia wa ofisi wakagundua kuwa vitenge vinaweza kuwa sehemu nzuri ya kupendezesha ofisi. 

“Inapendeza kutumia vitenge, tumezoea ofisi nyingi unakuta malighafi nyingi ni tofauti na vitenge. Kwahiyo sisi tumeamua kuwa tofauti na ofisi nyingi,” amesema Mallya.

Kutokana na muonekano mzuri, watu mbalimbali wamekuwa wakitumia ofisi hiyo kupiga picha ili kuwa na kumbukumbu zenye hisia  za Afrika ambazo siyo rahisi kupatikana katika ofisi nyingi.

Wameenda mbali zaidi na kutengeneza vizimba vya kupumzikia ambapo viti vyake vimefunikwa kwa aina mbalimbali ya vitenge. Kwa watu wanaotaka kufanya kazi katika mazingira tulivu na kujiona waafrika, hapo ni mahali sahihi.

Eneo tulivu lenye makochi ya vitenge ni kivutio kwa watu kujisomea na kupata maarifa. Picha| Daniel Samson.

Vitenge ni ajira, kitambulisho cha Afrika

Licha chimbuko la kampuni hiyo kuwa nchini Switzerland lakini iliamua kutokutumia fenicha au mapambo yenye asili ya Ulaya badala yake wameendeleza utamaduni wa Afrika.

“Tuliamua kutumia vitenge kwa sababu tulitaka kutengeneza mazingira ya Afrika kujiwakilisha wenyewe katika space (vituo) zetu zote. Kwa mfano tunatumia vitenge hapa Tanzania na maeneo mengi kama Ivory Coast na Nigeria kwa hiyo vitenge vinawakilisha mavazi ya Afrika,” amesema Mallya.


Zinazohusiana: Wabunifu wa huduma za ofisi kuwawezesha wanawake wajasiriamali Dar


Mallya anasema wanatumia fursa ya kutoa ajira kwa vijana wa Tanzania ambao wana uwezo wa kutengeneza mapambo na makochi kwa kutumia vitenge ikiwa ni hatua ya kuendeleza ubunifu katika jamii.

“Pia kuwapatia ajira watu mbalimbali ambao ni wabunifu licha ya kuwa materials (malighafi) tulinunua China lakini fabrication (utengenezaji) tukafanyia hapa Tanzania na kuna sehemu nyingi ambazo vijana wapo wanafanya hizi kazi,” amesema

Hata hivyo, wabunifu wanazidi kuvipa thamani vitenge kwa sababu matumizi yake yanaongezeka kila siku. Huko Uganda vinatumika kupamba viti vya magari ili kuongeza mvuto wa watumiaji wa magari binafsi.

Wewe unavitumiaje vitenge ili kujitofautisha na wengine ikiwa ni njia ya kuendeleza ubunifu?